TRA: Wafanyabiashara fanyeni makadirio ya kodi mapema

0
1838
Afisa Mwandamizi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rahel Shoo (kulia) akimuelimisha mfanyabiashara wa duka wa eneo la Mpemba Stendi mjini Tunduma mkoani Songwe, Simon Mabuba kuhusu umuhimu kuwa na Mashine ya Kodi ya Kielektroniki (EFD) wakati wa Kampeni ya Elimu ya Kodi ya Mkoa kwa Mkoa inayoendelea mkoani humo.

MWAMNDISHI WETU-SONGWE

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Songwe imewataka wafanyabiashara wa mkoa huo kufika katika ofisi zao kufanyiwa makadirio ya kodi ya robo ya kwanza ya 2020 kabla ya Machi 31 ambayo ni tarehe ya mwisho.

Akizungumza wakati wa kampeni ya Elimu ya Kodi ya mkoa kwa mkoa inayoendelea mkoani Songwe, Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi wa TRA makao makuu, Julius Mjenga amesema wanawakumbusha wafanyabiashara kuwa hiki ni kipindi cha wafanyabiashara kufanyiwa makadirio ya kodi ikiwa ni pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za biashara na umuhimu wa kutoa na kudai risiti.

Amesema katika kampeni hiyo wamewasisitizia wanunuzi kudai risiti kabla ya kuondoka dukani baada ya kuhudumiwa ili kuepuka kupata adhabu kutokana na kutokudai risiti.

“Hivi sasa kuna adhabu kwa watu ambao wananunua bidhaa alafu anashindwa kudai risiti na kwamba lengo la kufanya hivyo ni ili kutengeneza kizazi ambacho kitajua umuhimu wa kudai risiti ambazo zisipodaiwa ni kuchangia kuikosesha serikali mapato,” alisema Mjenga.

Amesema pia wamewafundisha wafanyabiashara hao kuhusu kodi ya majengo, kodi ya Ongezeko la Thamani pamoja na kodi zuio.

Amesema katika kuhakikisha wanafanikisha lengo la kampeni hiyo, kesho watakutana na wafanyabiashara wa wilaya ya Ileje ambao nao watawafundisha masuala mbalimbali ya kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here