TMA, WADAU WAJADILI HALI YA HEWA KIUCHUMI

0
903

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wadau mbalimbali kuzungumzia utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua unaoanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu katika baadhi ya maeneo.

Maeneo hayo ni yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ya kaskazini mwa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kufungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema mkutano umelenga kuwajengea wadau uelewa wa masuala ya hali ya hewa na utayari wa taarifa zitakazotolewa.

“Utabiri umekamilika, hivyo tumekutana na wadau waweze kuona ni athari gani ambazo zinaweza kupatikana kutokana na utabiri huu na kutoa mapendeko kukamilisha taarifa kamili ya hali ya hewa nchini.

“Mkutano huu ni sehemu muhimu ya ushirikishwaji wa wadau katika kujenga na kuimarisha utoaji na matumizi ya huduma za hali ya hewa katika jamii,” alisema Dk. Kijazi.

Alisema mkutano huo umehusisha wadau wengi zaidi kupitia utekelezaji wa miradi unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kwa nchi wanachama katika kuhakikisha kuwapo huduma bora na usalama wa chakula.

“Kuongezeka kwa wigo wa ushirikishwaji wa wadau ni jambo linalokwenda sambamba na dhamira na dira ya Mamlaka ya Hali ya Hewa ya kuhakikisha huduma za hali ya hewa zinatolewa kwa ubora unaokidhi mahitaji ya wadau katika kiwango cha juu,” alisema.

Alisema ushirikishwaji huu wadau ni sehemu ya utekelezaji wa mfumo wa kutoa huduma ya hali ya hewa uliozinduliwa hivi karibuni (National Framework for Climate Services -NFCS) ambao utaboresha huduma za kutoa hali ya hewa nchini.

Dk. Kijazi pia alieleza majukumu ya mamlaka yake kuwa ni kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu (msimu) na pia hutoa tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa yanayoweza kusababisha majanga.

Mratibu wa Kilimo Himilivu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika usalama wa chakula kutoka FAO, Diomedes Kalisa, alisema kikao kilikuwa cha mafanikio kwa vile wadau wote muhimu walikuwapo, hali inayoonyesha utayari wa wadau katika kupokea taarifa za hali ya hewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here