BEI YA MAFUTA YASHUKA

0
1383Na MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ambayo imeshuka.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany, alisema jana kuwa bei ya jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote yaliyoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, imepungua ikilinganishwa toleo la Agosti Mosi.

Taarifa hiyo pia ilisema kwa mwezi huu, bei ya rejareja ya petroli imepungua kwa Sh 10 kwa lita (asilimia 0.43).

Kwa   dizeli, bei ya rejareja imepungua kwa Sh 19 kwa lita (asilimia 0.83) na mafuta ya taa kwa Sh 24 kwa lita (asilimia 1.05).

“Mabadiliko haya ya bei yanatokana na kupungua kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia Julai mwaka huu ikilinganishwa na  bei ya Juni mwaka huu, iliyotumika katika bei ya kikomo ya petroli iliyotangazwa Agosti mwaka huu.

“Bei ya jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli katika Mkoa wa Tanga, imebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Agosti Mosi mwaka huu.

“Ifahamike kuwa kabla ya Agosti mwaka huu shehena ya mwisho ya mafuta ya petroli na dizeli katika bandari ya Tanga ilipokelewa Mei mwaka huu.

“Mamlaka inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo ya mafuta kwa eneo husika, inapatikana pia kupitia simu za kiganjani kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo.

“Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi  nchini.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015, bei ya   petroli itaendelea kupangwa na soko.

“Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi ya bidhaa za mafuta.

“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za   petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hiyo isivuke bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na kanuni (formula) iliyopitishwa na Ewura,”ilisema taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.

“Wauzaji wa petroli wanatakiwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita,”ilisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here