24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

TFF iwe macho na upangaji matokeo Daraja la Kwanza

UPANGAJI wa matokeo katika medani ya soka ni moja kati ya mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya mchezo huo duniani, huku yakizidi kushika kasi katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa kiasi kikubwa, upangaji wa matokeo katika mchezo wa soka ni kama laana, kwa kuwa humkosesha  haki mwenye uwezo wa kushinda na kumpa  fursa asiye na uwezo kushinda. Jambo hili kwa namna moja huchangia kurudisha nyuma maendeleo ya mchezo wa soka.

 Lakini suala la upangaji wa matokeo linatajwa kuanza muda mrefu na limekuwa likiota mizizi kadiri miaka inavyosonga, huku ikidaiwa kuwa suala hilo limekuwa likihusishwa na uchezaji wa kamari (betting).

Miaka takribani 12 iliyopita, timu ya Juventus ya Italia, ilishushwa Daraja la Pili (Serie B) kutokana na kuhusishwa katika upangaji wa matokeo.

Pamoja na suala la upangaji wa matokeo katika mchezo wa soka kutokea katika mataifa mbalimbali, Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limekuwa makini na likifuatilia kwa ukaribu suala hilo licha ya kuwa limekuwa likifanywa kwa usiri mkubwa.

Tanzania ambayo ni nchi mwanachama wa Fifa, suala hilo la upangaji wa matokeo limewahi kutokea mwaka 2016 ambapo timu tatu za Geita Gold (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora zilikutwa na hatia ya upangaji wa matokeo katika michezo ya Ligi Daraja la Kwanza na kupewa adhabu ya kushushswa daraja hadi Ligi Daraja la Pili.   

Licha ya adhabu zilizochukuliwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF za kuzishusha daraja timu hizo, bado kumeonekana kuwepo na viashiria vya upangaji wa matokeo katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza msimu huu kati ya Rhino Rangers ya Tabora na Dodoma FC ya Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyotolewa Februari 9, mwaka huu na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo, limepata taarifa za tukio la rushwa ya upangaji wa matokeo katika mchezo huo.

TFF bado inaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka husika za uchunguzi nchini ili kubaini ukweli wa jambo hilo ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa taratibu.

MTANZANIA tunaungana na TFF katika kuhakikisha kuwa suala la upangaji wa matokeo linadhibitiwa katika soka ili kuendeleza mchezo huo na kuleta haki miongoni mwa timu shiriki katika ligi hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Ligi Kuu.

Tunaamini kuwa TFF kwa kushirikisha vyombo vinavyohusika, vitalipatia ufumbuzi suala hilo kabla halijaleta athari katika mchezo wa soka kama ilivyokuwa katika miaka mitatu iliyopita kwa timu kushushwa daraja.

Lakini pia TFF inapaswa kufuatilia kwa ukaribu zaidi michezo yote ya Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini viashiria vya rushwa ya upangaji wa matokeo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles