28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

TCU yatoa sifa mpya kujiunga vyuo vikuu

Profesa Joyce Ndalichako
Profesa Joyce Ndalichako

Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza utaratibu mpya kwa watahiniwa wa mwaka mpya wa masomo wa 2016/2017 wanaochukua shahada, huku wanafunzi wengi wakiwa hatarini kukosa nafasi kwa kukosa sifa na vigezo.

Utaratibu huo mpya umekuja ikiwa ni miezi miwili sasa tangu kutumbuliwa kwa watendaji wa tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa na kusababisha kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Sifa hizo ziliwekwa mapema wiki hii katika tovuti ya TCU na kurudiwa jana. Taarifa hiyo inaonyesha kutolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Eliuta Mwageni.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu jana, Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku, alithibitisha taarifa ya utaratibu huo mpya.

Mkaku alisema utaratibu huo umetolewa baada ya mwaka jana kutumika mfumo wa wastani wa pointi (GPA) ambao Januari, mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, aliagiza ufutwe na kurudishwa ule wa madaraja (division) uliotumika siku zote.

“Mfumo wa udahili uliotumika mwaka jana ulikuwa ni GPA na mwaka huu utatumika mfumo wa divisheni, ndiyo maana utaratibu huo ukawekwa,” alisema Mkaku.

Moja ya sifa zinazotakiwa katika udahili wa mwaka huu wa masomo (2016/2017), ni wahitimu wa kidato cha sita waliomaliza kabla ya mwaka 2014 kuwa na ufaulu wa (D mbili) pointi 4.0.

Mchanganuo ulionyesha kuwa pointi hizo zinatokana na ufaulu wa A = 5; B= 4; C= 3; D = 2; E = 1.

Taarifa hiyo ilionyesha kuwa ili wahitimu wa kidato cha sita kwa mwaka 2014 na 2015 wawe na sifa za kudahiliwa, watatakiwa kuwa na alama za ufaulu wa (C mbili ) pointi 4.0 kupitia mchanganuo wa A = 5; B+ = 4; B = 3; C= 2; D = 1.

Pia tovuti hiyo ilionyesha kuwa wahitimu waliomaliza kidato cha sita kwa mwaka huu, watahitajika kuwa na ufaulu wa alama (D mbili) 4.0 kupitia mchanganuo wa A = 5; B = 4; C= 3; D= 2; E = 1.

Mbali na sifa hizo, watakaodahiliwa ni wale ambao pia watakuwa  na utambulisho wa sifa za kielimu za kidato cha nne ambazo ni kuanzia alama nne za D na kupanda juu katika mchanganuo wa alama za ufaulu wa B+, ikiwa A =75-100, B+ = 65-74, B=50-64, C=40-49, D=35-39, F= 0-38.

Sifa nyingine zinazotakiwa ni wenye cheti cha NVA daraja la tatu pamoja na ufaulu wa si chini ya alama nne za D za kidato cha nne au sifa nyingine zinazokaribiana na hizo, ikiwa ni pamoja na zinazotambuliwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) au Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Pia watahiniwa hao watatakiwa kuwa na angalau GPA ya 3.5 kwa stashahada (NTA) daraja la sita au wastani wa B kwa cheti cha ufundi (FTC) katika mchanganuo wa alama A=5, B=4, C=3 na D=2 au wastani wa daraja la B+ kwa wenye stashahada za ualimu, au wastani wa daraja la B+ kwa kitengo cha afya kama tabibu wa magonjwa ya binadamu na nyingine au cheti na stashahada nyinginezo.

Sifa nyingine zinazoangaliwa katika udahili huo ni kuwa na ufaulu wa daraja la pili kwa wenye stashahada zisizokuwa za NTA.

Pamoja na hayo, TCU ilisema hakutakuwa na usajili wa mafunzo ya awali pamoja na yale ya UQF6 yaliyozuiwa kuanzia mwaka wa masomo wa 2016/2017.

Taarifa ya tovuti hiyo iliendelea kusema kuwa maombi yote ya usajili wa wanafunzi hao wanaotaka kuchukua shahada yanatakiwa kupitia TCU pekee.

“Kwamba tume hiyo imeamua kuwa kuanzia mwaka 2016/2017, maombi yote ya usajili kwa makundi yote yanayoanzia aya ya 3.0 kwenda juu wataunganishwa na TCU pekee na walio chini ya hapo hawatahusika na tume hiyo,” ilisema taarifa hiyo.

Pia TCU ilisema taarifa hiyoni kwa mujibu wa kipengele cha 5(1)(c)(i) cha katiba ya vyuo vikuu, kifungu cha 346 cha sheria nchini.

“Msingi wa kubadili viwango vya kujiunga na elimu ya juu ni kutokana na kuwepo maoni kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya uwezo wa wahitimu wanaojiunga na vyuo vikuu mbalimbali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mei, mwaka huu, Profesa Ndalichako aliwasimamisha kazi Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, kwa kushindwa kuisimamia tume hiyo kutokana na kuwapo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa, kisha wakadahiliwa katika vyuo vikuu na kupata mkopo.

Wengine aliowasimamisha kazi ni Mkurugenzi wa Ithibati na Udhibiti Ubora, Dk. Savinus Maronga, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kiishweko na Ofi sa Msimamizi Mkuu wa Taarifa, Kimboka Stambuli.

Pia Mei mwaka huu, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idrisa Kikula, alitangaza kuwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya stashahada ya ualimu ambao hawakuwa na sifa.

Alipozungumzia sakata hilo Juni, mwaka huu wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Dk. John Magufuli, aliwaita wanafunzi hao kuwa ni vilaza, na kwamba idadi kubwa ya waliofukuzwa hawakuwa na sifa stahiki za  kudahiliwa kusoma kozi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles