23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

JPM ampa kazi Mrema

mremahuyo

AGATHA CHARLES NA VERONICA ROMWALDI, DAR ES SALAAM

AHADI ya Rais John Magufuli aliyoitoa kwa Augustino Mrema wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 akiwa Himo, Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, kuwa asipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo atamtafutia kazi nyingine hatimaye imetimizwa.

Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa Rais Magufuli amemteua Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) uteuzi wake umeanza jana, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mstaafu Eusebia Munuo ambaye muda wake umemalizika.

Rais Magufuli alimuahidi kazi Mrema Oktoba mwaka jana alipokuwa kwenye kampeni za kutafuta kura za urais kwa wananchi wa Jimbo la Vunjo, ambalo Mrema alikuwa mbunge wao kabla ya kuangushwa katika uchaguzi uliopita na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi.

Katika kampeni hizo Rais Magufuli alinukuliwa akisema: “Kama mtaichagua CCM, Mrema nitamtafutia kazi… Mzee Mrema sitamwacha kutokana na rekodi yake ya utendaji kazi katika nchi hii.”

Mrema naye aliwahi kumpigia debe Dk. Magufuli, licha ya kwamba chama chake kilikuwa kimemsimamsisha mgombea urais ambaye alikuwa Macmillan Lyimo.

Kwa maneno yake mwenyewe, Mrema alimmwagia sifa Magufuli akisema ndiye anayepaswa kuwa rais.

“Jamani rais wetu ni Magufuli, naomba wote tumchague mchapakazi, ametujengea barabara nyingi katika jimbo letu,” alisema Mrema.

Aprili mwaka huu, Mrema alikumbushia ahadi yake hiyo kupitia vyombo vya habari kwa kumwomba Rais Magufuli ampatie kazi ili wasaidiane kupambana na ufi sadi katika Serikali hii ya awamu ya tano.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Mrema nyumbani kwake Sinza ili kuzungumzia uteuzi huo, lakini hakupatikana kutokana na kuwa shambani kwake Mlandizi, mkoani -Pwani.

Akizungumza kwa simu jana ikiwa ni saa chache baada ya taarifa za uteuzi huo, Mrema alisema Rais Magufuli amethibitisha kuwa yeye ni muungwana na mkweli.

“Nimepokea kwa furaha uteuzi huu wa Rais Magufuli. Nipo huku Mlandizi saa hizi (jana saa 10 jioni), nimekuja shambani kwangu, nafanya shughuli za ukulima na ufugaji pia.

Nimefurahi mno, nampongeza kwa uungwana wake.

“Wakati wa kampeni mwaka jana akiwa kule jimboni Vunjo, aliwaeleza wananchi kuwa ikiwa wanataka kiongozi makini anayewafaa wanichague, alisema Mrema ni jembe na aliwaambia kuwa ikiwa hawatanichagua yeye atanipa kazi.

“Baadhi ya watu waliposikia kauli ile walifanya njama, wakafanikiwa kuniangusha… sikuchaguliwa kuwa Mbunge wa Vunjo, watu hao walipoona nimeanguka ubunge wakawa wanasema Rais Magufuli alinidanganya na kwamba hatanipa kazi.

“Hata hivyo mvumilivu hula mbivu, hatimaye Rais Magufuli leo (jana) ametekeleza ahadi yake… amethibitisha kuwa ni mkweli, muungwana na anaishi kwa maneno yake.

“Kweli katika kipindi changu cha uongozi niliweza kuitumikia nchi na tukafanikiwa kupunguza vitendo vya uhalifu.

Kazi aliyonipa rais inalingana na uzoefu na ujuzi wangu wa muda mrefu nilionao, ameniweka mahali ambapo sitamwangusha, nitamfanyia kazi nzuri sana na sitawaangusha Watanzania, nitawatumikia vizuri sana,” alisema.

Mrema alisema baada ya uteuzi huo kazi yake ya kwanza itakuwa ni kwenda kutembelea magereza yote nchini.

“Nitazungumza na wafungwa kuona namna gani tutaweza kutumia sheria ya parole. Parole maana yake ipo sheria ambayo inaruhusu wafungwa waliojirekebisha ambao hawana makosa makubwa kuweza kukamilisha vipindi vyao vya magereza nje, nitatembelea magereza nitaongea nao kama nilivyokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, nilikuwa natembelea magereza na wahalifu na kuzungumza nao.

“Nilikuwa nikiwaeleza kufungwa hakumaanishi kuwa hawana manufaa tena, kwa hiyo nikawa nawaambia washirikiane na Serikali, na sasa nitawaambia washirikiane na rais, kwa sababu wafungwa wamefungwa, lakini bunduki, silaha zipo nje, kwa hiyo wanajua nani wanazo na mtandao ule wanaujua, nitazungumza nao wanipe majina, nitawaondoa gerezani watakwenda kutusaidia kuzikamata hizo silaha na kutuonyesha wahalifu wazoefu walioko uraiani wanaotutesa,” alisema Mrema.

Mrema alisema atapendekeza kwa Rais Magufuli awapunguzie vifungo vyao, badala ya kukaa gerezani kwa muda wote waliohukumiwa, sehemu ya kifungo chao wamalizie nje ya magereza.

“Kwa hiyo mimi nina hakika nitasaidia sana, magereza yetu yamejaa na parole imewekwa kusaidia kupunguza magereza yasiwe na wafungwa wengi kupita kiasi, na hawa watu tutajenga urafi ki ili wajue kufungwa si mwisho wa maisha, kumbe wanaweza kutusaidia kwa kushirikiana na Serikali kukomesha uhalifu uliopo uraiani huku,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles