29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

TCRA kuharibu simu, laini za watuma SMS za kitapeli

Na BENJAMIN MASESE

-MWANZA

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema imeunda kikundi maalumu kinachoshirikisha watoa huduma za mawasiliano ili kuharibu simu za matapeli wanaotuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS).

Kauli hiyo imetolewa jana na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo, katika mkutano wa wadau wa sekta ya mawasiliano, uliolenga kupokea kero na mapendekezo juu ya utendaji wa mamlaka hiyo.

Mihayo alisema suala la SMS za utepeli kutumwa kwa watu limekuwa sugu, hivyo TCRA na kampuni za mawasiliano, walikaa na kuunda kikundi cha kushughulikia namba za simu zinazotuma ujumbe wa utapeli.

“Moja ya malalamiko sugu katika suala la mawasiliano ni watu kutumiwa ujumbe wa utapeli, wametapeliwa sana, wapo wanaolalamika kupata ujumbe usiku na kusababisha mgogoro katika ndoa, lakini kama TCRA na watoa huduma tukaamua kuunda ‘group’ letu la kuwashughulikia watu wa namna hiyo.

“Katika ‘group’ hilo, mmojawapo akipokea ujumbe wa utapeli ukiwamo kutuma pesa katika namba fulani, sisi watu wa mawasiliano na watoa huduma tunashirikiana kuharibu ile namba na simu husika, nadhani SMS zimepungua kwenu, tunaomba wale wanaotumiwa ujumbe huo watumie namba hiyo katika kampuni husika.

“Naombeni wananchi kuweni makini, ukitumiwa ujumbe wowote kaa kimya, inakuwaje unatuma fedha kwa mtu ambaye humjui. 

“Pia kwa upande wa watoa huduma naomba msitume SMS  za ofa zenu usiku wakati watu wamelala, maana zinaleta migogoro,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema baadhi ya watu maarufu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuandika mambo yasiyo ya kweli, huku jamii ikiwaamini kuliko vyombo vya habari vyenye leseni.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka watu hao wakiwamo wanasiasa na wasanii kuwa makini kuanzia sasa, kwani wanafuatilia kwa ukaribu na endapo watawabaini watawachukulia hatua.

Pia alisema kuanzia Januari Mosi mwakani, kila mtu atakuwa akimiliki laini moja kwa mtandao mmoja na atakayetaka kuwa na zaidi ya namba moja kwenye mtandao mmoja, atapaswa kuandika maelezo ya uhitaji wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles