26.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 26, 2022

TATIZO SIYO KIKI ILA MATOKEO YAKE

WASANII wa kileo kila siku wanasababisha habari. Wameshajua kuwa staa ni kutafuta kiki, basi watafanya chochote ili jamii iachane na mambo yote imuulike jambo lao.

Wengi wamefanikiwa kutokana na hizi kiki. Ukiingia kwenye mitandao ya kijamii na hasa ule maarufu wa Instagram utakutana na visa vya kutosha kutoka kwa mastaa mbalimbali.

Kiki siyo jambo jipya. Hata mastaa wa mtoni hutumia kiki kujiweka masikioni mwa mashabiki. Tatizo la wasanii wetu wa Bongo ni kutokuchagua aina ya kiki zinazofaa.

Wengi hudhani kwamba kiki ni kutafuta skendo, tena skendo yenyewe ya mapenzi. Wanaamini kiki ni kufanya kitu kibaya au cha ajabu kwenye jamii.

Siyo kweli. Tunaweza kujifunza zaidi kupitia marehemu Steven Kanumba na rafiki yake Vincent Kigosi. Hawa walikuwa maswahiba wakubwa katika tasnia ya filamu.

Wakikutana chemba pamoja, waligongeana glasi za vinywaji na kufurahi lakini kwenye jamii wana bifu. Somo kubwa tunalopata kwao, ni kwamba bifu lao halikuhusisha kugombania wanawake.

Lilihusisha kazi tu. Kanumba akitoa filamu hii, kesho Ray anamjibu kwa filamu nyingine. Ray akimuwahi, Kanumba anamjibu.

Ndiyo maisha ya kibiashara yanavyokuwa. Lakini baada ya kipindi fulani, ambacho si chini ya mwaka mmoja, marafiki hawa walikuwa wakikutana kwenye filamu ya pamoja.

Wengi mtakumbuka sinema kama O’prah na Off-side ambazo ziliwakutanisha mahasimu hawa waliotokea kuwa marafiki wakubwa.

Kilichokuwa kinafurahisha zaidi kwa hawa jamaa ni kwamba wanapokuwa mbele za watu wengine hata kama ni watu wao wa karibu kabisa, huendelea kujifanya wana bifu, lakini mkiondoka tu ni marafiki wakubwa.

Nitafurahi kuona siku moja Ali Kiba na Diamond wakikutana kwenye singo moja. Profesa Jay aliwahi kuingia kwenye mzozo na Jose Chameleone wa Uganda baada ya Chameleone kutumia melody ya wimbo wake wa Zali la Mentali lakini wiki kadhaa mbele wakakutana kwenye singo ya Ndivyo Sivyo.

Na pengine kwa kizazi cha sasa, wasanii wanaweza kujifunza kwa namna fulani hata kwa Harmorapa ambaye anaendelea kupaa bila kutumia skendo za kuudhi. Yeye anajifanyia yake tu, magazeti yanaandika. Mitandao yote inamzungumzia yeye.

Kabla ya kutengeneza kiki kwa skendo za kipuuzi, jiulize jamii itakuchukuliaje? Utajipandisha kisanii au utajivunja heshima? Ukipata majibu ya maswali hayo, chukua hatua.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,803FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles