23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI IELEZEALIYEMTISHIA NAPE BASTOLA YUKO WAPI

HIVI sasa watu wanauliza kwamba askari kanzu aliyemnyooshea bastola Waziri wa zamani wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, kwa nini hajakamatwa!

Nape alitishiwa kuuawa kwa bastola na askari huyo Machi 23, mwaka huu, wakati akishuka katika gari lake na kutaka kuzungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Hoteli ya Protea, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Rais Dk. John Magufuli kumvua uwaziri.

Askari huyo ambaye picha zake zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, inaelezwa kuwa ni miongoni mwa askari waliopewa maagizo ya kumzuia Nape asizungumze na waandishi wa habari siku hiyo, hivyo akatumia nguvu kumsukuna na kisha kumnyooshea bastola kutaka arudi kwenye gari na kuondoka eneo hilo, ili mkutano wake na wanahabari usifanyike.

Askari hajakamatwa tangu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alipotoa agizo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, kumsaka hadi kumtia mikononi mtuhumiwa huyo.

Mwigulu alitoa agizo la kumsaka hadi kumkamata mtuhumiwa huyo Machi 24, mwaka huu na leo ni zaidi ya wiki mbili bado hajakamatwa!

Watu wanauliza hivi kweli inawezekana polisi wameshindwa kumkamata askari kanzu huyo?

Watu wanataka kumfahamu mtuhumiwa husika lakini Jeshi la Polisi limesema bado linachunguza undani wa tukio hilo na kwamba linaendelea kumsaka mhusika.

Kuna taarifa kuwaMsemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, tayari amekaririwa kuwa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kumnasa aliyemtishia Nape kwa bastola.

Hata hivyo, kauli hiyo inakinzana na ile iliyotolewa na Mwigulu hivi karibuni wakati akifungua mkutano wa kazi wa mwaka wa maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa Vikosi wa Jeshi la Polisi mjini Dodoma kuwa mhusika wa tukio hilo amekwisha kupatikana na atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi vinasema kuwa kuna ugumu katika kumkamata mtuhumiwa huyo.

Nape, mmoja wa makada wa CCM waliofanikisha uteuzi wa Rais Dk. Magufuli na hata ushindi wake, alivuliwa uwaziri siku moja baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tuhuma za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia Kituo cha Televisheni cha Clouds saa nne usiku akiwa na askari wenye silaha za moto.

Uvamizi huo ulikuwa na lengo la kuwashinikiza watangazaji wa Kipindi cha Shilawadu kurusha video inayomwonyesha mwanamke mmoja akidai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa lengo la kumchafua kiongozi huyo wa kiroho.

Ripoti ya kamati hiyo ilimtia hatiani mkuu wa mkoa huyo, kwa sababu ilibaini namna alivyofika na kuwatisha wafanyakazi wa Clouds Media.

Tunaamini Wizara ya Mambo ya Ndani italieleza hili la askari kanzuili kuondoa taharuki ya watu na kuweka rekodi sahihi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles