29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

TATIZO LA UZAZI KWA WANAWAKE, WANAUME NI 50/50


Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

FURAHA ya binadamu aliyekamilika hapa duniani ni kupata mtoto, hasa kwa wale ambao wamekubaliana kuishi pamoja (wanandoa). Hata hivyo, siku hizi watu wengi wanakabiliwa na matatizo ya uzazi.

Tunashuhudia baadhi ya ndoa zikivunjika kutokana na wanandoa kushindwa kupata watoto, ni jambo linalohuzunisha.

Mara nyingi wanawake ndio hutupiwa lawama inapotokea changamoto hiyo, lakini wataalamu wa afya wanaeleza kwamba hata wanawaume wanaweza kushindwa kuzalisha.

Zipo pia simulizi za ndugu, jamaa na marafiki ambao hulazimika kwenda nje ya nchi kufuata matibabu ya kibingwa ili kupandikiza ujauzito.

Uongozi wa Hospitali ya Kairuki (KH), Shule ya Uuguzi Kairuki (KSN), Hospitali ya Kairuki (KH) na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki  (KHMU) unakusudia kuanzisha huduma ya kupandikiza ujauzito nchini, ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya Hubert Kairuki aliyefariki mwaka 1999.

Mwasisi huyo alifariki dunia wakati miradi yake hiyo ikiwa michanga na sasa imekuwa kimbilio la wananchi wengi.

Daktari Bingwa wa Wanawake hospitalini hapo, Clementina Kairuki anasema kwa kawaida iwapo mke na mume wanahitaji kupata mtoto wanapaswa kushiriki tendo la ndoa mara mbili hadi tatu kwa wiki.

“Ikiwa watashiriki kwa kipindi cha mwaka mmoja huku wakiwa hawatumii kinga yoyote lakini wakashindwa kupata mtoto hapo tunaanza kufanya uchunguzi wa awali kwanini hali hiyo ipo.

“Hapo tunaanza kuhesabu kwamba kuna tatizo hivyo tunamfanyia uchunguzi, kwa sababu katika kipindi cha mwaka mmoja wanakuwa na uwezekano wa kupata mimba kwa kiwango cha asilimia 86.

“Kipindi cha mwaka wa kwanza huwa ni cha kusubiri, lakini ikiwa watakaa zaidi hadi mwaka wa pili hapo inabidi tuwafanyie uchunguzi wa kina, lakini kabla ya yote tunaangalia ushiriki wao katika tendo,” anasema. 

Ukubwa wa tatizo

Anasema Shirika la Afya Duniani (WHO) linabainisha kuwa watu milioni 48 duniani wanakabiliwa na tatizo la kutopata ujauzito.

“Lakini matokeo hayo yalikuwa ni ya uchunguzi wa watu ambao walikaa kwa kipindi cha miaka mitano bila kupata ujauzito, tafsiri ni kwamba inabidi wawe wamekaa miaka miwili bila kupata ujauzito hivyo, WHO mwaka 2014 likasema kwa waliokaa miaka miwili hadi miwili na nusu maana yake watu milioni 12 ndiyo wenye tatizo la kutopata ujauzito,” anasema.

Anasema kutokana na matokeo ya utafiti huo, WHO ilitangaza tatizo hilo kuwa ni janga.

“Hapa nyumbani (Tanzania) tuna matokeo ya utafiti ambao ulifanyika zamani kidogo, unaonesha asilimia 20 ya mtu mke na mume walio katika umri wa kupata ujauzito wanakabiliwa na changamoto hiyo,” anasema.

Anasema katika kliniki yao, asilimia 30 ya wanawake na wanaume wanaowahudumia wanakabiliwa na tatizo hilo na kwamba kati yao asilimia mbili hadi 10 wanashindwa kabisa kutatuliwa matatizo yao na hivyo kuhitaji njia mbadala (kupandikiza).

Anasema changamoto wanayoiona ni kwamba mara nyingi wanawake ndiyo ambao hujitokeza na kugundulika mapema huku wanaume wakija baadae kuhudhuria kliniki. 

Visababishi

“Wote wanapaswa kuchunguzwa, mwanamume anaweza kuchangia tatizo hili kwa asilimia 40 hadi 50 na wanawake hivyo hivyo. Ni kwa asilimia tano tu wanaweza kuchangia wote wawili kushindwa kusababisha ujauzito,” anasema.

Dk. Kairuki anasema tafiti zinaonesha wanawake wengi nchini hushindwa kupata ujauzito kutokana na kuziba kwa mirija ya uzazi kuliko wakina baba.

Anataja sababu za kuziba kwa mirija kuwa ni pamoja na kutoa mimba ovyo, kujifungua katika mazingira ambayo si salama ambako kunaweza kusababisha maambukizi na hatimaye kuziba mirija ya uzazi.

Anasema iwapo mwanamke atatoa mimba na asisafishwe vizuri, matokeo yake ni kupata maambukizi yanayoweza kusababisha mirija ya uzazi kuziba.

Pia mjamzito anapochelewa kujifungua na kufanyiwa upasuaji wa haraka ili kutoa mtoto kunaweza kusababisha maambukizi.

Dk. Clementina anasema wapo wengine ambao wamezaliwa na matatizo ya homoni, kwamba zinakuwa hazijawiana inavyotakiwa na hivyo kushindwa kupata ujauzito.

“Mtu anaweza pia kuwa amezaliwa huku viungo vyake vya uzazi vikiwa havijakamilika, kupata maradhi mbalimbali ikiwamo saratani au uvimbe kwenye kizazi kunaweza kumfanya mwanamke asibebe ujauzito.

“Kuna asilimia 15 ya wanandoa ambao hawapati ujauzito na sababu hazijulikani, yaani ukiwachunguza unakuta hawana tatizo lolote na wanashiriki vema kabisa tendo,” anasema. 

Wanaume nao wana matatizo

Dk. Kairuki anasema kwa upande wa wanaume huwa wanaangalia vitu vinne ikiwamo ubora wa mbegu zake.

“Ule wingi wa mbegu anaotakiwa kutoa mara moja kiwango cha chini kinapaswa kuwa milioni 39 kwa mkupuo wa kwanza, ile kasi yake inapaswa kuwa angalau asilimia 32 na ‘concentration’ katika ujazo huo iwe mililita moja,” anabainisha.

Anasema huwa wanaangalia pia umbo la mbegu zake jinsi zilivyokaa, ambapo wakichunguza huwa wanajua iwapo zipo sawa sawa kama zinavyopaswa au la. Anasema kuna akina baba hawana mbegu kabisa au zipo chache na hazikidhi kiwango kinachotakiwa.

“Hii inatokana na mambo mengi, inawezekana ikawa ‘chromosome’ zake hazipo sawa sawa au anakuwa anatengeneza mbegu chache mno. Kuna vitu vingi vinasababisha matatizo ya genetics, homoni hazitoshi au viungo vyake havijakamilika,” anabainisha.

Anasema kama mtu anakabiliwa na ugonjwa wa kisukari huweza kumsababishia kushindwa kufanya vema tendo la ndoa au kupungukiwa nguvu hivyo kushindwa kutoa mbegu au akatoa kwa kiwango cha chini.

“Wengine wanashindwa kabisa kutoa yale majimaji kwa sababu mbegu hutoka zikiwa na majimaji yake, hali ya hewa nayo inaweza kusababisha tatizo hasa katika joto jingi, au kutokunywa maji ya kutosha pia ni kisababishi,” anasema. 

Matibabu

Anasema pale wanapogundua tatizo kuna njia nyingi huzitumika kuwatibu wahusika ikiwamo za vidonge na upasuaji.

“Tunaweza kuwatibu kwa kuwapatia dawa maalumu za vidonge wote wawili au tunafanya upasuaji wa kuzibua mirija kama imeziba. Kama mayai ya mama hayakomai vizuri tunaweza kufanya upasuaji katika vifuko vya mayai yake na yakatoka yakiwa yamekomaa vizuri,” anasema.

Anasema wanaweza kufanya upasuaji huo kwa njia ya kisasa ya ‘laparascopic’ na mama akaeendelea na shughuli zake kama kawaida baada ya muda mfupi.

“Ikiwa njia hizo zitashindikana, basi hutulazimu kupandikiza. Tunaweza kuchukua mbegu za baba na kuzitayarisha maabara huku tukisubiri mayai ya mama yakomae, tunachukua zile mbegu za baba na kuweka kwa mama kupitia njia ya uke.

“Njia hii imeanza kutumika tangu miaka ya 1970 lakini ili kuitumia inapaswa mirija ya mama iwe wazi (haijaziba), kama imeziba inabidi kutumia njia nyingine ikiwamo ile ya IVF.

“Mwaka 1978 alipatikana mtoto wa kwanza kwa kutumia njia hii ya IVF, baada ya hapo zikagundulika pia njia zingine ambazo zinaweza kutumika kwa wanandoa wenye shida ya uzazi,” anasema.

Dk. Clementina anasema ipo njia nyingine ambapo mbegu za baba huhifadhiwa na mayai ya mama hutayarishwa kwa kuchomwa sindano maalumu.

“Kwa kawaida mayai mawili hukomaa kwa pamoja, lakini kwa njia ya kitaalamu tunaweza kuvuna hata mayai 20 kwa mkupuo na kuyapeleka maabara,” anasema.

Anaongeza: “Mwanamume anaweza kutoa mbegu kwa njia ya kawaida ya kujamiiana au kwa kupiga punyeto, huwa tunamshauri jinsi ya kufanya na muda gani akae ndio azitoe.

“Ikishindikana tunampatia dawa maalumu ya kumchangamsha ili zitoke zenyewe na ikiwa hazitoki kabisa tunaweza kuzichukua kitaalamu kwa upasuaji kutoka kwenye korodani zake na kuzipeleka maabara.”

Anasema wakizifikisha maabara huziweka pamoja na kwamba baada ya siku mbili hadi tano huwa tayari zimetengeneza kijusi ambacho huchukuliwa na kuingizwa katika tumbo la uzazi la mama kwa njia ya uke.

“Baada ya hatua hiyo, mama anapewa muda wa kupumzika kwa dakika 15 kisha anakwenda zake nyumbani akiwa tayari ana ujauzito.

“Mimba hiyo huwa haina tofauti na zile zilizotungwa kwa njia ya kujamiiana, licha ya kwamba hii huwa imetayarishwa maabara, kiumbe kinakua kikiwa maabara na tunakitumbukiza kwa njia ya uke kwenda kwenye tumbo la uzazi ambalo nalo linakuwa limeandaliwa kukipokea.

“Kwa njia ya IVF tunakuwa tumechukua mayai ya mama na kuyamwagia mbegu za baba ambazo hufuata yale mayai, kasi yake huwa kubwa zaidi kuliko njia ya kawaida kwa sababu yanakuwa yameandaliwa.

“Kwa njia ya IX tunachofanya ni kuchukua yai la mama na mbegu ya baba kisha tunachomeka moja kwa moja wakati njia ya IVF tunaingiza zile mbegu nyingi kwa pamoja,” anabainisha. 

Njia mbadala

Daktari huyo anasema wapo wanawake ambao hawana mayai au wanayo lakini hayakidhi viwango hasa wale walio na umri mkubwa kwa kuwa yanakuwa yamepoteza ubora, hivyo njia hii huwasaidia.

“Nchi za wenzetu, wana benki ya kuhifadhia mayai na mbegu za uzazi, zinahifadhiwa katika chumba chenye nyuzi joto 196 ambayo ni baridi kali sana na kuna kemikali ambazo hutumika kuhifadhia, zinaweza kukaa hata miaka 50 ndani ya chumba hicho,” anasema.

Wizara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya anasema mpango huo ni mzuri na wa kupongeza kwa kuwa utasaidia wengi.

“Nawaomba muendelee na mshikamano huo wa kubuni mambo yanayohusu tiba kwa maslahi ya wananchi, wazo hili litakapoanza litasaidia wananchi wengi.

“Hivi sasa serikali ina mambo mengi ya kufanya, si vibaya watu binafsi wakiwa na miradi itakayokwenda sambamba na msaada kwa wananchi,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles