Tarura wamkera RC Lindi

0
1183

Hadija Omary, Lindi

Serikali mkoani Lindi imechukizwa na kitendo cha Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) mkoani humo kutuhumiwa kutoa kazi kwa wakandarasi  kwa njia za rushwa hali inayopelekea baadhi ya miradi kushindwa kusimamiwa kikamilifu.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa huo Godfrey Zambi leo alipokuwa anafunga kikao cha kwanza cha Bodi ya  Barabara mkoani humo.

Amesema  amechukizwa  kutokana na  kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakandarasi mkoani humo  kuwa ili wapate kazi lazima watoe kiasi fulani cha fedha na ataendelea kulifanyia uchunguzi na atakapobaini ukweli wa jambo hilo hatosita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

“ Kitendo hiki si cha kiungwana nawataka waratibu wa Tarura katika halmashauri kuacha tabia hiyo kwani kufanya hiyo kutawafanya mshindwe kuwawajibisha wakandarasi hao endapo watafanya vibaya katika miradi wanayoitekeleza, “ amesema RC Zambi.

Kwa upande wake Mratibu wa Tarura mkoa wa Lindi Mhandisi Agatha Mtwangambate amesema  malaamiko hayo yanachafua taasisi yao na kwamba madai hayo wanayachukuwa kama changamoto na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuwabaini watendaji wanaofanya  vitendo hivyo.

Amesema kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 wamejipanga kufanya kazi kwa ufanisi na kuondoa malalamiko yaliyojitokeza katika kipindi cha mwaka uliopita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here