23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANITE BADO INA NAFASI MASHINDANO YA KIMATAIFA

TIMU ya Taifa ya vijana ya wanawake walio chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’,

juzi imeanza vibaya safari ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Ufaransa.

Tanzanite ilipoteza mchezo huo baada ya kufungwa mabao 3-0 na wenyeji wao Nigeria, katika mchezo wa awali uliopigwa nchini humo, hivyo kusubiri mchezo wa marudiano utakaochezwa baadaye nchini.

Timu hiyo inahitaji kupambana mno katika mchezo wa marudiano unaotarajiwa kuchezwa baada ya wiki mbili, hivyo ushindi wa mabao 4-0 ndio pekee utakaoiwezesha timu hiyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa fainali hizo.

Sisi MTANZANIA tuna imani na timu hiyo kutokana na uwezo wa wachezaji lakini pia ujasiri walionao wa kupambana pamoja na kufanya maandalizi ya kutosha katika kukabiliana na mashindano ya kimataifa.

Tunaamini kuwa kikosi hicho kinachonolewa na kocha mkuu Sebastian Mkoma, kitajipanga vyema kukabiliana na Nigeria katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini na kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao.

Ni wakati wa Watanzania kuiunga mkono zaidi timu hiyo kuelekea katika mchezo huo wa marudiano, ili kuhakikisha inapata ushindi wa zaidi ya mabao 4-0 ili iweze kusonga mbele na hatimaye kufuzu kwa fainali hizo.

Bado kuna nafasi ya kufanya vizuri katika kufuzu kwa fainali hizo za Kombe la Dunia, si wakati wa kukata tamaa, timu hiyo ijiandae vya kutosha kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano na kwa hakika lolote linaweza kubadili matokeo ya awali.

Sisi MTANZANIA tunaiunga mkono timu hiyo ya Tanzanite katika harakati za kusaka tiketi ya kufuzu kwa fainali hizo, lakini ipo haja kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya uongozi wa Rais Wallace Karia, kuweka nguvu katika kuiandaa timu hiyo ili iweze kufanikisha ifuzu kwa fainali hizo.

Timu hiyo iandaliwe mechi ngumu za kimataifa za kujipima nguvu kabla ya mchezo wa marudiano na Nigeria, lakini pia wachezaji waandaliwe kisaikolojia ili waone kuwa matokeo ya awali ya kufungwa mabao 3-0 wanaweza kuyabadilisha wakiwa katika uwanja wa nyumbani.

Lakini pia kwa umoja wa Watanzania wakijitokeza uwanjani kwa wingi kuishangilia Tanzanite, kunaweza kubadili matokeo na hivyo kuiondoa Nigeria katika nafasi ya kufuzu fainali hizo.

Watanzania wanapaswa kuiunga mkono timu hiyo ambayo inaweza kuleta faraja kutokana na timu nyingine za soka za Taifa kukosa nafasi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia.

Iwapo Tanzanite itafanya vizuri na kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana wa umri huo, itakuwa imeweka rekodi bora kabisa katika medani ya kimataifa kwa kucheza fainali hizo, ambazo hata timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ haijawahi kuifikia rekodi hiyo tangu fainali za kwanza ilipochezwa mwaka 1930 nchini Uruguay.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles