29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yaongoza kwa kuwa na kiwango kidogo cha bei ya bando

Na Ramadhan Hassan,DODOMA

HADI kufikia Juni 2023, Tanzania imeendelea kuwa nchi yenye kiwango kidogo cha bei ya data kwa GB 1 ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo gharama ya GB 1 ni Dola za Marekani 0.71 sawa na Sh 1,666.

Hayo yameelezwa leo Jumanne, Julai 18,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Jabir Bakari wakati akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo na mwelekeo kwa mwaka 2023/24.

Mkurugenzi huyo amesema mwenendo wa gharama za rejareja za data bila kifurushi na kwenye kifurushi kuanzia 2015 hadi Juni 2023 (ikijumuisha kodi) zimeendelea kupungua na kuongeza utumiaji wa huduma za Intaneti nchini.

“Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, hadi kufikia Juni 2023, Tanzania imeendelea kuwa nchi yenye kiwango kidogo sana cha bei ya data kwa GB 1 ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo gharama ya GB 1 ni dola za Marekani 0.71 sawa na Sh 1,666.

“Pia kwa kiwango hicho hicho, Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa bei ndogo ya data kwa GB 1 ukilinganisha na nchi zote zilizopo SADC na hii ni kwa mujibu wa ripoti ya “Worldwide Mobile Data Pricing 2022,” amesema Dk. Bakari.

Amesema Tanzania pia inashika nafasi ya saba kwa kuwa na bei ndogo ya data kwa Afrika.

“Katika Bara la Afrika, takwimu hizo zinaonyesha kuwa wastani wa gharama ya GB 1 ni Dola za Marekani 3.51 hii ni sawa na Sh 8,157,” amesema Dk. Bakari.

Mkurugenzi huyo amesema TCRA imefanikiwa kugawa masafa yanayowezesha utoaji wa huduma ya intaneti ya kasi.

Amesema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2025 asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma ya intaneti ya kasi.

“TCRA ipo katika hatua za awali za kufungua bendi za masafa ambazo zitatumiwa na watoa huduma bure bila kuhitaji kuwa na leseni ya rasilimali masafa,hatua hii itaongeza matumizi ya Intaneti kwa kuwa na huduma za intaneti za wazi (WiFi -hotspots),” amesema.

Amesema utoaji wa huduma za mawasiliano ni wa ushindani, hivyo umesababisha kuongezeka kwa idadi ya mitandao, matumizi ya TEHAMA na aina za huduma zinazotolewa kwa wananchi, Taasisi na Serikali kwa ujumla.

“Kuenea kwa huduma hizi kunawezeshwa na uwepo wa Sera imara, sheria nzuri na mifumo wezeshi ya kiusimamizi na utoaji leseni. Aidha, TCRA imeendelea kuboresha mifumo ya huduma kwa wateja ikiwemo matumizi ya mfumo wa ‘Tanzanite Portal’,”amesema Dk. Bakari.

Amesema mfumo huo umeongeza ufanisi katika kuhudumia mteja kupitia dirisha moja la maombi ya leseni za aina zote, utoaji wa vyeti vya uhakiki wa vifaa vya kielektroniki, anuani za makazi na dawati la huduma kuwezesha mawasilisho ya malalamiko ya wateja.

Amesema TCRA imeendelea kutoa Leseni na kusimamia masharti ya leseni kwa watoa huduma za mawasiliano nchini.

Amesema hadi kufikia Juni 2023, wana watoa huduma 1481 na jumla ya leseni 2,415.

Aidha, TCRA imefanya maboresho makubwa ya mifumo ya udhibiti wa sekta ili kuhahikisha watoa huduma za mawasiliano wanatoa huduma kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo na masharti ya leseni.

Amesema TCRA imefanya upimaji wa ubora wa huduma za mawasiliano ya simu katika mikoa 24, Tanzania Bara na mikoa yote ya Zanzibar.

Dk. Bakari amesema upimaji wa hivi karibuni ulifanyika kuanzia mwezi Aprili hadi Juni, 2023 umehusisha makampuni sita ya simu katika maeneo ya miji saba nchini.

“TCRA imefanya upimaji wa kiwango cha mionzi ya masafa ya redio na simu kwa mikoa 15 Tanzania ili kuwalinda watumiaji wa huduma za mawasiliano na wananchi wanaoishi karibu na miundombinu ya minara ya Simu, Redio na Televisheni,” amesema Mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo amesema kupitia Postikodi, TCRA imefanikiwa kuhuisha kiwango cha anwani za makazi cha mwaka 2015 (Rural and Urban Addressing Standard TZS1571:2015), kuhuisha na kuchapisha orodha ya postikod.

Aidha amesema idadi ya miamala imeongezeka kutoka 349,952,830 Julai, 2023 hadi miamala 420,675,884 Juni, 2023.

Aidha, akaunti za pesa kwa simu zimeongezeka kwa asilimia 24 kuanzia Julai, 2022 hadi Juni, 2023 wakati miamala ikiongezeka kwa asilimia 20.

Mkurugenzi huyo amesema mwelekeo wa TCRA ni kuwapa watumishi mafunzo endelevu ndani na nje ya nchi ili kukuza uwezo wao kwa utekelezaji wa kazi za udhibiti.

“Itaendelea kuimarisha usimamizi wa Mfumo wa utoaji leseni na rasilimali za mawasiliano na kutoa elimu kwa watumiaji na wadau wengine wa huduma za mawasiliano ili kuongeza uelewa juu ya haki na wajibu wao,”amesema Dk. Bakari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles