24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania, Ujerumani zasaini makubaliano

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Tanzania na Ujerumani zimesaini makubaliano ya ahadi  ya msaada wa kiasi cha Euro milioni 70 sawa na Sh bilioni 193.71 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, zikiwamo sekta za maji, afya, maliasili, utawala bora na usimamizi wa sheria.

Makubaliano hayo yamefanyika   leo Machi 20,2024  Dar es Salaam kati ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya na  Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani,  Marcus Von Essen.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo,  Mwandumbya, amezipongeza timu za wataalamu wa nchi hizo mbili kwa kazi ya kuongoza majadiliano yaliyowezesha kukubaliana na kusainiwa kwa kumbukumbu za majadiliano hayo, ambazo zinaelezea ushirikiano wa nchi hizo kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania.

“Naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani kwa ahadi ya msaada huu utakaozinufaisha sekta za maendeleo nchini katika eneo la Bioanuwai, ambalo kwa kiasi kikubwa linajumuisha kusaidia Hifadhi za Taifa na Hifadhi za Wanyamapori ili kuhifadhi mazingira yake tajiri ya asili na kuongeza mapato kupitia utalii endelevu,  pia katika sekta ya afya ambayo inajumuisha maeneo ya huduma za dharura za watoto wachanga, afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa vijana na bima ya afya ya pamoja,” amesema Mwandumbya.

Amefafanua kuwa ahadi zilizotajwa zitasaidia miradi maalum kama kupunguza migogoro ya  binadamu na wanyama ambapo kiasi cha Euro milioni  9,  mradi wa Maendeleo Endelevu ya Mifumo ya Hifadhi, kiasi cha Euro milioni 15, mradi wa kuimarisha Afya ya Uzazi na kuwawezesha vijana  wa kike, kiasi cha Euro milioni 9 na  mradi wa kuimarisha mfumo wa Bima ya Afya kwa wote nchini Tanzania, kiasi cha Euro milioni  3.

Amechanganua maeneo  mengine kuwa ni mradi wa kuanzisha Bima ya Afya ya Pamoja, kiasi cha Euro milioni 15, mradi wa upatikanaji wa haki kwa wanawake na watoto, kiasi cha Euro milioni 6 , kuzuia unyanyasaji wa kijinsia ni  Euro milioni 10,  utawala bora na usimamizi wa fedha  Euro milioni 2 na fedha kwa  maandalizi ya miradi ni  Euro milioni moja.

“Ningependa kuthibitisha tena dhamira ya Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia  kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu muhimu kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu,” ameongeza.

Kwa Upande wa Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani,  Marcus Von Essen, ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wao katika maendeleo ya maeneo muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja.

“Tumekuwa na uaminifu na ushirikiano mzuri sana kati yetu, tumeangalia vipaumbele katika ushirikiano wetu na tumezungumza kuhusu namna ya kuongeza kasi katika majadiliano yetu ili mafanikio ya mazungumzo haya yaonekane kwa haraka,” amesema Essen.

Ameongeza kuwa, Ujerumani itaendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Tanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini, Thomas Terstegen, amezishauri pande zote kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu yanafikiwa kama ilivyokusudiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles