25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaongeza ‘Combination’ kidato cha tano

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imezindua mfumo wa kufanya mabadiliko ya tahasusi(Combination) za kidato cha tano na kozi za vyuo kwa njia ya mtandao kwenye mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha tano na vyuo mwaka 2024 baada ya kuongeza mpya 49 kutoka 16 za awali na kufikia 65.

Akizungumaza na waandishi wa habari leo Machi 20,2024 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, amesema mfumo huo unawapa fursa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2023 kuchagua tahasusi za kidato cha tano na kozi za vyuo vya elimu, vyuo vya kati na elimu ya ufundi kwa mfumo wa kielektroniki.

Mchengerwa amesema Serikali imekua ikitoa fursa kwa wahitimu wa kidato cha nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya tahasusi na kozi mbalimbali walizochagua kupitia fomu ya uchaguzi.

“Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye fomu za uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa wakiwa shule, hivyo basi mfumo huu umeanza kazi leo na utafungwa rasmi April 30, mwaka huu,”amesema Mchengerwa.

Amesema kwa mujibu wa mabadiliko ya sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 na Mitaala ya Elimu kwa Kidato cha Tano, yameanza kutekelezwa, ambapo utekelezaji huo umehusisha uanzishaji wa tahasusi mpya 49, kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia tahasusi 65.

“Tahasusi hizo mpya zitakazoanza kutekelezwa Julai, 2024 zipo katika makundi saba ambayo ni tahasusi Sayansi ya Jamii, Lugha, tahasusi za Masomo ya Biashara, tahasusi za Sayansi, tahasusi za Michezo, tahasusi za Sanaa pamoja na tahasusi za Elimu ya Dini,”amesema.

Amefafanua kuwa baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za kidato cha tano na kozi mbalimbali katika vyuo vya kati na vya elimu ya ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao.

Amesema ili kuhakikisha masomo hayo yanatolewa na kuwaandaa vijana, serikali imeajiri walimu 10,300 ili kukidhi ufundishaji wa masomo hayo huku akihimiza Halmashauri kuharakisha madarasa mtandao.

Ameeleza kuwa TAMISEMI imetoa fursa kwa wahitimu wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Nne mwaka 2023 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yao ya baadaye hivyo amewasihi wazazi na waleze kuwasaidia watoto wao katika uchaguzi wa tahasusi hizo.

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba wakati wa ujazaji wa fomu za machaguo ya awali, tahasusi mpya 49 hazikuwepo kwenye orodha ya machaguo na pia matokeo ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne hayakuwa yametoka kumuwezesha mwanafunzi kuweza kuwa na machaguo mazuri zaidi kulingana na ufaulu wake.

“Ili kuingia kwenye mfumo itabidi mhitimu atumie Namba ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2023, jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa na alama ya ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa,”amesema.

Ameongeza kuwa baada ya matokeo ya kujiunga na kidato cha tano na vyuo kutangazwa, Ofisi haitashughulikia changamoto hizo kwa kuwa fursa ya kufanya mabadiliko hayo imeshatolewa.

“Huduma hii ya kubadilisha tahasusi ni bure na endapo wanafunzi watapata changamoto, wawasiliane na Dawati la Huduma la Mteja,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles