LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
SIMU ya mkononi ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT–Wazalendo), Zitto Kabwe, iliyokuwa ikishikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za baadhi ya viongozi wa Serikali kukwamisha Mradi wa Mchuchuma na Liganga imerejeshwa.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT, Ado Shaibu, simu hiyo ilirejeshwa juzi baada ya kushikiliwa kwa siku nne na Takukuru.
Ado aliishukuru Takukuru kuirejesha simu hiyo lakini akidai kuwa muda wa siku nne walioishikilia ni mrefu na si kitendo cha uungwana.
“Wasidhani kwamba sisi ni wajinga kwamba simu hiyo ikirudishwa tutaendelea kuitumia hivyo hivyo au tutaendelea kuitumia bila kuichuguza, tunajua wanaweza kuwa wameifanya wanavyojua.
“Labda niseme hii si mara ya kwanza kushikiliwa kwa simu ya kiongozi wetu na kama kuna mwanasiasa simu yake imeshikiliwa mara nyingi basi ni Zitto, mara ya kwanza aliposema Serikali inatoa takwimu za uongo ili kupindisha ukweli simu yake ilishikiliwa na hadi sasa haijarudishwa.
“Mara ya pili ni wakati ule alipotoa taarifa za mauaji ya wananchi yaliyofanyika Kigoma na hii ya sasa alipotahadharisha kuhusu njama za makusudi za kukwamisha Mradi wa Mchuchuma na Liganga ambayo tunashukuru wameirudisha,” alisema Ado.
Simu hiyo ilishikiliwa kutokana na taarifa ambazo Zitto alizichapisha Novemba 29, mwaka jana katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akidai kuwa mradi huo unahujumiwa na baadhi ya kampuni za chuma kutoka China, Urusi na Uturuki kwa kuwahonga baadhi ya watendaji wa Serikali ili waukwamishe.
“Nimepata taarifa za kushtusha, kampuni za chuma za China, Urusi na Uturuki zimehonga baadhi ya watendaji wa Serikali kukwamisha mradi wa Mchuchuma na Liganga hadi mradi wa SGR uishe. Lengo ni kuhakikisha nchi hizo zinapata soko la vyuma vyao,” aliandika Zitto.
Baada ya Zitto kuandika ujumbe huo, aliitwa na Takukuru kupeleka ushahidi kuhusu taarifa hizo na ndipo simu hiyo iliposhikiliwa.