24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TAFSIDA TATA HUSABABISHA TUNGO ZISIWACHOSHE MASHABIKI

SIWALINGANISHI Mbaraka na Nasibu, lakini nalinganisha zama na uhondo wa tungo kama ambavyo kila mmoja ameishi katika wakati wake na kuwa maarufu kwa muda wake kwenye muziki.

Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alitamba kitambo hicho (Back) hata akakwea pipa kwenda ughaibuni kutumbuiza, katika nyakati ambazo kupanda ndege kwa mfumo tuliokuwa tukiishi ni sawa na kuota kupanda Apollo ya kwenda anga za juu, lakini katika zama za sasa (Front) ni kawaida tu na wasanii wanakwea pipa kama daladala.

Mbaraka alitinga hata nchi ambazo hazikutarajiwa kama Japan, aliporudi alitunga wimbo kusifia jinsi Wabongo walioenda huko akiwemo Mzee Morris Nyunyusa walivyopagawisha.

Lakini hapa nataka nikupe mambo mengine ya upinzani wake wa kitambo hicho dhidi ya nguli mwingine, Juma Kilaza, aliyekuwa na bendi yake ya Cuban Marimba, Mbaraka akiwa na Super Volcano wenzangu wa zamani mnakumbuka tafsida tata ya ngoma: ‘Jogoo La Shamba’.

 

Vipande vikali alivyotuma Mbaraka: “Ulijidai mbabe sana leo umepigwa na kijana mdogo aibu imekupata, utamtisha nani we kwanza ushamba haujakutoka je uliona wapi jogoo la shamba likawika mjini!”

Vinavyosemekana alikuwa akimjibu mpinzani wake ingawa mwenyewe hakuwahi kusema hivyo hadharani, vilihanikiza mabitozi wa ‘Back’ hiyo kufurika dansini kila alipotumbuiza manake kama Mbaraka alimuimba hasimu wake, lakini hata mashabiki walikuwa na mahasimu wao waliowananga kwa kutumia wimbo huo.

Zama zilisonga hadi nyakati za ‘Front’ ya Sikinde na Msondo lakini nakumbuka wanamuziki waliowahi kujitenga na bendi hiyo na kwenda kuanzisha nyingine (Super Sikinde), wakawa wanaweka kionjo cha tafsida tata kwenye mashairi yao: “Kulamba asali kwa ncha ya kisu ni hatari utamu ukikolea utachanika ulimi!” wakiwananga wenzao waliobakia kundini.

Lakini unakumbuka mambo ya mtindo wa ‘Chunusi’ wa Supreme Freddy Ndala Kasheba kwa tungo ya ‘Chatu’ ya wana Ndekule Orchestra Safari Sound (OSS), vikiwa ni vijembe kwa Msondo na Sikinde?

Natamani katika ‘Front’ ya sasa, tafsida zingetawala ili kunogesha mafumbo na kuepuka kuharamishwa na kuhalalishwa kwa tungo ziwe za mtindo wowote.

Mathalan Diamond alipozua zogo kwa ngoma yake: ‘Ninyamaze Kimya’ pengine angeweka tafsida flani za fumbo mfumbie asiyeelewa ngoma isingezua hamkani na ingedumu kwa muda mrefu kwani kila mmoja angeitumia kivyake kuwananga wanaomsumbua, kama mambo ya ‘Jogoo La Shamba’ wa Mbaraka Mwinshehe katika zama hizo lakini hata ngoma ya ‘Wapo’ imesumbua na kufifia ghafla kutokana na kukosa tafsida.

Walau ile ya Darasa ‘Muziki’ licha ya kuonekana imezimwa na kiki za kisiasa kwa sasa lakini ilidumu kwa muda flani ingawa ingekuwa na tafsida nzito zaidi ingeendelea kusumbua hadi sasa.

Weledi uliosadifu zamani umeachwa kando na kuingiza biashara kupita kiasi kwenye muziki kwa kutaka kuuza sana ambacho hakidumu, kisha kesho tutengeneze kingine ndipo lilipo jibu la kwa nini licha ya maendeleo ya kiteknolojia katika muziki kwenye ‘Front’ ya sasa lakini bado tunasumbuka sana kuwapiku Waghana, Wasauzi na wengine tunaowaiga!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles