30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

SWALI LA LISSU LAZUA UBISHI MAHAKAMANI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salum Hamdani, kueleza anachofahamu juu ya Katiba ya Zanzibar na kama Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar , Salum Jecha ana mamlaka ya kufuta matokeo ya uchaguzi au laa.

Lissu alihoji hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati Hamdani alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya uchochozi inayomkabili Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio.

Mshtakiwa Lissu aliomba kujiwakilisha mwenyewe mahakamani hivyo baada ya ushahidi alimuhoji maswali shahidi kulingana na ushahidi wake.

Swali hilo la Lissu lilimfanya Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, kupinga akitaka shahidi asijibu kwa sababu si mtaalamu wa sheria wala Katiba.

Kadushi alidai shahidi hawezi kutoa tafsiri ya Katiba ya Zanzibar na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza masuala ya kikatiba.

Akijibu pingamizi hilo, Lissu alidai halina msingi wowote kwa sababu suala la Serikali ya Zanzibar ni halali ama limeletwa na upande wa mashtaka wenyewe katika shtaka la pili na la tatu hivyo wakabiliane nalo.

Wakili Peter Kibatala alidai mahakamani hapo kuwa shahidi huyo anapaswa kueleza yeye mwenyewe kama hawezi kulijibu swali hilo na si vinginevyo na kwamba katika kuandika uamuzi wake mahakama ipende isipende ni lazima itajibu swali hilo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili aliahidi kutoa uamuzi leo iwapo shahidi aeleze anachokifahamu kuhusu Katiba ya Zanzibar ama la.

Kabla ya kufikia katika malumbano hayo Lissu alitaka kujua yeye na washtakiwa wenzake walikula wapi kuchapisha huo uchochezi.

Alihoji wao watu wanne waliwasiliana kwa maandishi, email ama simu na saa ngapi, maswali hayo yalijibiwa na shahidi kwamba hafahamu.

Awali akihojiwa na Wakili Kibatala kuhusu wapi alipata taarifa za kuwapo kwa mikusanyiko ya watu katika sehemu za kuuzia magazeti , Hamdani alidai alizipata kwa RCO wa Kinondoni, Temeke na Ilala na kwa upande wa Zanzibar alipata kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani.

Shahidi alidai katika Gazeti la Mawio la Januari 14 mpaka 20 kulikuwa na habari yenye kichwa cha habari Machafuko yaja Zanzibar na kwamba maneno hayo yangeweza kuleta chuki, uvunjifu wa amani, uchochezi na hofu.

Alidai baada ya kuona hivyo na kulinua gazeti hilo alifungua jalada la uchunguzi kisha aliteua wapelelezi ili kuona kama kuna kesi ya jinai na walipoona waliwafikisha washtakiwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles