26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

Spika Ndugai azuia wabunge 15 Chadema

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amewazuia wabunge 15 wa Chadema kuhudhuria bungeni, iwapo hawatakamilisha masharti mawili muhimu.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Spika jana, ilieleza kuwa wabunge hao watatakiwa kutimiza masharti hayo kwa kuwa hawajulikani waliko na wamekuwa wakihesabiwa kama watoro tangu walipoacha kuingia bungeni Mei 1, mwaka huu.

 “Ofisi ya Bunge inatoa taarifa kwamba katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekuwa watoro kwa kutohudhuria vikao vya Bunge bila ruhusa ya Spika kwa muda wa wiki mbili, kinyume na masharti ya Kanuni ya 146 inayosisitiza wajibu wa kila mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge.

“Aidha, tunapenda ifahamike kwamba wabunge hao walisusia vikao vya Bunge huku wakiwa wamelipwa posho ya kujikimu ya kuanzia Mei 1-17, 2020. 

“Kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 5 ya Kanuni za Bunge, Spika alitoa masharti mawili kwa wabunge hao,” ilieleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa sharti la kwanza ni kuwataka wabunge hao kurejea bungeni au kurudisha fedha walizolipwa mara moja na sharti la pili ni kwa kuwa haijulikani wabunge hao walipo, watalazimika kuwasilisha ushahidi kwamba wamepimwa na hawana maambukizi ya virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kuingia bungeni.

Taarifa hiyo iliwataja wabunge hao kuwa ni Freeman Mbowe, Ester Bulaya, Halima Mdee, John Heche, Joseph Mbilinyi, Peter Msigwa, Rhoda Kunchela, Pascal Haonga, Catherine Rage, Devotha Minja, Joyce Mukya, Aida Khenan, Upendo Peneza, Grace Kiwelu na Joseph Haule.

“Hivyo basi, kwa taarifa hii, na kwa mujibu we Kanuni ya 144 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayohusu usalama katika maeneo ya Bunge, Spika ameagiza Kitengo cha Usalama cha Bunge kutowaruhusu wabunge waliotajwa hapo juu kuingia katika maeneo ya Bunge kuanzia leo (jana) Jumatano Mei 13, 2020 mpaka watakapotimiza masharti tajwa hapo juu,” ilieleza taarifa hiyo.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Spika Ndugai aliyoyatoa Mei 6, mwaka huu akisema wabunge hao waliojipa karantini ya siku 14 ni watoro na wanatakiwa kurudi bungeni haraka ili waendelee na kazi.

Pia aliwataka wabunge hao ambao wamelipwa fedha za kujikimu za kuanzia Mei Mosi hadi 17, mwaka huu kama hawatarudi bungeni mara moja, wakati watakaporudi baada ya siku 14 hawatapokewa hadi wawe na vyeti vya kuonyesha wamepimwa corona na pia wawe wamerudisha kwenye akaunti ya Bunge fedha hizo.

Spika Ndugai alisema endapo hawatafanya hivyo hawataruhusiwa kuingia bungeni na majina yao yatapelekwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zaidi kwa sababu watakuwa wamefanya wizi wa fedha hizo.

Agizo hilo lilitokana na hatua ya uongozi wa Chadema kuwaagiza wabunge wake kuacha kuhudhuria vikao vya Bunge na kukaa mbali na majengo ya Bunge ya Dodoma na Dar es Salaam ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Hivi karibuni akisoma maamuzi ya Kamati Kuu ya Chadema iliyofanywa kwa njia ya mtandao, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, aliwataka wabunge hao kutorudisha fedha hizo na waendelee kuwa karantini kama chama kilivyoelekeza.

Mnyika aliwasisitiza wabunge wao wote walioko Dodoma wasiende majimboni au mikoani bali wabaki Dodoma kwenye karantini hadi itakapothibitika kuwa ni salama na au kupata maelekezo mengine yoyote yaliyo rasmi.

Siku 14 za wabunge hao kujiweka karantini zilikamilika jana.

KUHUSU POSHO

Hata hivyo pamoja na maagizo ya awali kuhusu wabunge wa Chadema kurejesha posho za siku 14 ambazo walishalipwa, chama hicho kimekaidi maelekezo hayo na kueleza kuwa hakuna mbunge aliyefanya kosa kwa kupokea posho hizo. 

Mnyika alisema kuwa Kamati Kuu ilijadili kwa kina kuhusu madai ya Spika Ndugai kwamba wabunge wa Chadema waliopewa posho za kujikimu Dodoma ni wezi na ilifikia uamuzi kwamba madai hayo ni ya uongo na chama kutoa rai kwa wabunge kuwa kwa sababu siyo wezi, wasitekeleze yale yaliyoelekezwa na Spika ambayo yanakwenda kinyume cha sheria, Katiba ya nchi na utaratibu wa Bunge.

“Kwa hiyo kimsingi Kamati Kuu imepitia madai hayo na kuona kwamba wabunge wa Chadema siyo wezi kama alivyojaribu kudai Spika,” alisema Mnyika.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho cha Kamati Kuu kiliazimia kuwafuta uanachama wabunge wake wanne, wakiwamo Joseph Selasini (Rombo), Antony Komu (Moshi Vijijini) ambao wote kwa nyakati tofauti walitangaza kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi mara baada ya Bunge kumaliza muda wake.

Mbali na hao pia kikao hicho kiliwavua unachama wabunge Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) na Davidi Silinde (Momba) huku Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu akivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya chama na kutakiwa kujieleza kwanini asichukuliwa hatua.

Aidha, wabunge wengine ambao wanaendelea kuhudhuria vikao vya Bunge wametakiwa kujieleza ni kwa vipi wasichukuliwe hatua zaidi kwa kukiuka hayo maagizo na makubaliano ya chama.

Waliotakiwa kujieleza kwa kukiuka makubaliano hayo ni Suzan Masele, Joyce Sokombi, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Sware Semesi, Jafari Michael, Peter Lijualikali, Willy Kambalo, Rose Kamili, Sabrina Sungura na Anne Gideria.

Hata hivyo, akizungumza bungeni mwanzoni mwa wiki, Spika Ndugai alisema yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuwaapisha wabunge, hivyo wabunge wa Chadema wanaoingia bungeni wasitishwe na mtu yeyote na kwamba vikao vinavyoendelea ni vya majungu tu.

“Lakini niseme wabunge mnaapishwa na Spika, wakati nawaapisha hapa na wabunge wangu niliowaapisha wala msiwe na wasiwasi, vikao ni vya majungu wala msiwe na wasiwasi.

“Eti mtu mmoja anajifanya ana mamlaka ya kuburuza wabunge anavyotaka, haiwezekani. Biashara itaishia huko huko, sio kwa hii Tanzania, unafanya unavyotaka, mara kushoto geuka, kulia sawa, kushoto sawa, nyuma geuka sawa, ukipata mshahara haya lete huku.

“Kweli mmekuwa watumwa wa mtu, hili jambo halipo duniani wala Tanzania, muendelee kutulia msiwe na shaka,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles