25.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Prof. Kabudi aeleza nafasi ya Tanzania kimataifa

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imewasilisha bajeti yake huku ikijivunia mafanikio nane, ikiwemo kufungua balozi mpya nane za Tanzania katika nchi za Qatar, Uturuki, Sudan, Cuba, Israel, Algeria, Jamhuri ya Korea, na Namibia.

Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 199.75 ambapo kati ya fedha hizo zaidi ya Sh bilioni  179.75 ni kwa matumizi ya kawaida na Sh bilioni 20 kwa bajeti ya maendeleo.

Akiwasilisha bajeti jana bungeni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi, alisema mafanikio makubwa ambayo wizara inajivunia kuyaratibu kwa ufanisi mkubwa na kufanikisha utekelezaji wake kwa kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kufungua balozi mpya nane.

 “Kufunguliwa kwa balozi hizo kunaifanya Tanzania kuwa na jumla ya balozi 43 na konseli kuu tatu katika miji ya Mombasa, Dubai na Jeddah,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema kadhalika balozi za Ethiopia na Poland zilifunguliwa hapa nchini katika kipindi hicho na kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa balozi 62 na mashirika ya kimataifa.

Profesa Kabudi alisema pia wamefanikiwa kuifanya lugha ya Kiswahili kutumika katika jumuiya za kimataifa na katika nchi mbalimbali.

 “Juhudi hizo za Tanzania zimefanya Kiswahili kitumike katika eneo la Maziwa Makuu, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema kuwa pia wamefanikisha kufanyika kwa viwango vya juu mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Dar es Salaam Agosti mwaka jana, ambapo Tanzania ilikabidhiwa rasmi uenyekiti wa jumuiya hiyo utakaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Agosti.

Profesa Kabudi pia alisema wizara yake imefanikiwa kuhamasisha watalii kuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

“Kwa mfano, kuanzia mwaka 2015 hadi 2018, watalii 5,234,448 wametembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema watalii hao walitoka nchi mbalimbali zilizopo Bara la Afrika, Ulaya, Amerika ya Kaskazini, Asia, Mashariki ya Kati, Australia na nchi za Karibeani.

Profesa Kabudi pia alisema kuwa wizara yake iliratibu ujio wa madaktari bingwa wa fani tofauti kutoka nchi mbalimbali kama vile Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Misri, Israel, Italia, China, India, Pakistan, Marekani, Ujerumani na Cuba.

“Madaktari hao walitoa huduma za kitabibu katika baadhi ya hospitali zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar na kufanikisha msaada wa ujenzi wa jengo la kitengo cha magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma,” alisema Profesa Kabudi.

Akieleza mafanikio mengine, alisema kuwa waliratibu ushiriki wa Tanzania katika kurejesha na kuimarisha amani na utulivu kwa kushiriki katika utatuzi wa migogoro na operesheni za kulinda amani kikanda na kimataifa.

Alisema kuwa Tanzania iliratibu mkutano wa 18 wa mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika na Nordic (Africa – Nordic Summit) uliofanyika Dar es Salaam Novemba mwaka jana.

Profesa Kabudi alisema pia uliratibiwa mchakato wa upatikanaji wa kampuni za Arab Contractors na El Sewedy Electric za Misri kwa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 katika Bonde la Mto Rufiji (Mwalimu Julius Nyerere Hydropower Project – MJNHP).

CHANGAMOTO

Akielezea changamoto, Profesa Kabudi alisema kuwa  wamekuwa wakikutana nazo, ikiwamo kasi ndogo ya sekta binafsi kutumia fursa za biashara na uwekezaji zitokanazo na mtangamano wa Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa.

Alisema pia uelewa mdogo wa Watanzania kuhusu masuala na fursa zitokanazo na mtangamano wa kikanda.

Profesa Kabudi alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili kupatiwa vibali vya ajira mpya na kujaza nafasi zilizo wazi.

Alisema pia wameendelea kutoa kipaumbele cha upatikanaji wa magari katika bajeti ya wizara na kuendelea kuhamasisha umma kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza katika nchi mbalimbali, jumuiya za kikanda na kimataifa.

TANZANIA KIKANDA

Profesa Kabudi alisema kuwa Tanzania inaendelea kushirikiana na mataifa mengine katika kushughulikia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanahatarisha maisha, ustawi na maendeleo ya nchi.

Aidha alisema nchi mbalimbali zimeendelea kukabiliana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

“Mathalani katika kipindi hiki, baadhi ya nchi za SADC, zikiwemo Comoro, Malawi, Msumbiji, Madagascar na Zimbabwe zilikabiliwa na majanga ya asili ikiwemo mafuriko na ukame uliosababisha kuwepo kwa upungufu wa chakula katika nchi hizo,” alisema Profesa Kabudi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,567FollowersFollow
517,000SubscribersSubscribe

Latest Articles