25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SNURA: NAPATA WAKATI MGUMU KULEA WANANGU BILA BABA

Na KYALAA  SEHEYE,

WANAWAKE wengi wako katika wakati mgumu wa kulea watoto wao wenyewe bila wanaume waliowazalisha. Hali hii inasababishwa na mambo mengi ikiwamo wanaume kutojua thamani ya mtoto au mwanamke kuzaa na mtu ambaye hakuwa na malengo naye. Pengine alimwambia mwanamke huyo atoe mimba naye akakataa hivyo ni lazima amsusie malezi. Wapo wanaume pia wanaokimbia majukumu kutokana na hali ngumu ya maisha.

Wanaume wengine wanaishi bila malengo, hivyo inapotokea amempa mwanamke ujauzito humuwia vigumu kumtunza na kumpatia mtoto haki yake ya kuwa na baba.

Wanachofikiria wao ni kutunza  mtoto, hivyo wanaona kama itakuwa mzigo kwao – jambo la haraka analolifikiria ni kutelekeza kuanzia mimba hadi mtoto.

Wanaume wa aina hii ndio wanaochangia ongezeko kubwa la watoto wa mitaani, kwani wakati mwingine inapotokea mama ametelekezwa, watoto wanakosa malezi bora hatimaye huanza kuzurura ovyo mitaani.

Snura Mushi ni msanii wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini, ambaye awali alikuwa akifanya kazi za uigizaji.

Msanii huyu ni miongozi mwa wanawake ambao wamezalishwa na kutelekezwa na wanaume waliozaa nao.

Akizungumza MTANZANIA kuhusu ugumu wa malezi ya mzazi mmoja kwa watoto, anasema ni magumu hata kama mama ana fedha za kutosha.

Snura anasema athari za malezi ya mama pekee hasa kwa mtoto ni kitu ambacho kinamuumiza mno kichwa.

Anasema kuwa mtoto hata kama unampa mahitaji yake yote muhimu ila anakosa kuita baba, ni lazima atakusumbua.

“…nimeamua kufunguka na kuweka wazi juu ya shida ninayokumbana nayo katika kulea watoto wangu, licha ya kwamba kuna wasanii wenzangu ambao ni maarufu nao wanakumbana na adha kama hii lakini hawako radhi kuweka bayana ili jamii ijifunze kitu kutoka kwetu.

“Malezi ya upande mmoja kwa kweli si jambo zuri…inaumiza mno wanawake. Wanaume wengi wanahisi kuwa tukiwa tunawahitaji basi tunataka msaada wa malezi, si kweli.

“Mtoto anayelelewa na wazazi wawili siku zote huwa na furaha kwani anakuwa hana tatizo la kisaikolojia, lakini wanaokosa malezi ya wazazi wote wawili kwa kiasi Fulani huathirika,” anasema Snura.

Anaeleza kuwa yeye anaweza kujiita kuwa ni mwenye bahati mbaya kwani mtoto wake wa kwanza hamjui baba yake na kwamba amejaribu kwa kila hali kumuweka mwanawe karibu na mzazi mwenzie lakini imeshindikana.

Mtoto wake wa pili naye pia ametelekezwa. Anasema kuwa  siku alipojifungua alimfahamisha mzazi mwenzie lakini hakufika kumuona mtoto, hadi alipolazimishwa na baadhi ya watu wakiwamo anaofanya nao kazi.

Anasema kuwa tangu alipomuona mtoto akiwa na miezi kadhaa hakwenda tena na hajui mpaka sasa anaendeleaje.

Anabainisha kuwa baada ya kumdadisi kujua tabia yake katika suala la kulea familia, akagundua kuwa ndiyo tabia yake.

“Nilipofuatilia nilifahamu kuwa kabla ya mtoto wangu alikuwa na mtoto mwingine ambaye naye kamtelekeza… nimejitahidi kuwaweka pamoja labda atawakumbuka lakini wapi, huyu mtoto wa mke mwenzangu ni mchangamfu ila siku alipokutanishwa na baba yake alikuwa mpole na ghafla alibadilika na akaonyesha dhahiri amemchukia,” anasema Snura ambaye hakutaka kuweka wazi majina ya wazazi wenzie wala watoto wake.

Kuna ugumu mkubwa sana wa kulea mtoto peke yako, tatizo si mahitaji bali ni akili ya mtoto.

Anabainisha kuwa mtoto anayelelewa na wazazi wote wawili hata kama hapati mahitaji yote, siku zote huonekana kuwa ni mwenye furaha.

“Swali ambalo huwa linaniumiza kichwa kutoka kwa mwanangu ni pale anaponiuliza baba yangu yuko wapi… mbona sisi hatukai naye?

“Swali hili huwa linamjia kila anapoona marafiki zake wakisimulia habari za wazazi wao wote wawili, wakati yeye anasimulia mzazi mmoja, huwa naumia mno,” anasema.

Snura anaendelea kusema kuwa kuna ugumu mkubwa mtoto anapolelewa na upande mmoja,  kwa sababu kuna vitu ambavyo inabidi baba achukue nafasi yake hata kama hana mchango wa kifedha. “Kuna vitu ambavyo mtoto anastahili kujifunza kutoka kwa baba, sasa kama  katelekezwa huwa inamuathiri mno na pengine atakua katika hali hiyo, hivyo baadae anaweza kumshusha thamani baba yake hata kama akiwa na uwezo atashindwa kumsaidia.

“Mapenzi ya mtoto na wazazi huanza tangu akiwa mdogo, sasa kama atakosa malezi ya upande mmoja ni lazima atapata wakati mgumu na hata kumfanya awe katili ukubwani,” anasema na kuongeza:

“Tunakutana na changamoto nyingi, ukiachilia mbali kimalezi pia kijamii kuna sehemu ambazo mtoto anahitajika kwenda na wazazi wawili, wewe inakuwa ngumu na wakianza kutambulishana  hapo mtoto huwa mnyonge hivyo inakubidi utumie nguvu ya ziada kuanza kumrudisha katika hali ya kawaida.”

Anasema kuwa hata anapokuwa katika hali ya kawaida wakati mwingine mawazo humjia na hapo ndipo anapotamani kujua baba yake alipo.

Anasema kuwa kuna kipindi watoto wanaolelewa na mama pekee huwa wanagoma kula, hasa inapotokea anaumwa… anakwambia sili hadi baba yangu aje. Anakwambia mbona fulani baba yake wanakaa naye na mimi namtaka baba yangu, hapo ndipo mzazi unaanza kuhangaika ili mradi mtoto ale na aweze kuchangamka kama watoto wengine.

Snura anawashauri wanaume kuwajali watoto wao hata kama hawana kitu.

“Usione mwanamke anakubembeleza ukajua kuwa anataka fedha ya matumizi, la hasha! Wanachohitaji na baba kupata muda kwenda kucheza na mwanae ili afarijike asijione mwenye kutengwa au kutelekezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles