26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI YA KUTIBU, KUEPUKA VIPELE VINAVYOSABABISHWA NA NEPI

VIPELE vinavyotokea kwa watoto wanaotumia nepi (diaper dermatitis) husababishwa na unyevu-nyevu, michubuko, kugusana na kinyeshi na mkojo kwa muda mrefu.

Mara nyingi vipele hivi hutokea katika maeneo ya mtoto yaliyofunikwa na nepi. Tatizo hili huwakumba watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja na hutokea kwa kiasi kikubwa kwa watoto wenye umri wa miezi 9-12.

Hali ya unyevu inayochangiwa na mtoto kukaa na nepi muda mrefu husababisha madhara ya ngozi, na ngozi iliyolowanishwa kwa muda mrefu huruhusu sumu zilizo katika mkojo na kinyesi ziingie ndani ya ngozi.

Katika ngozi kuna vimeng’enyo (enzymes) vinavyoitwa urease ambayo hutengeneza ammonia kutoka kwa bakteria walio kwenye ngozi.

Pia kwenye kinyesi kuna vimeng’enyo vinavyoitwa lipase na protease, ambavyo huibadilisha ngozi kwa kupunguza hali ya tindikali na hivyo kusababisha michubuko zaidi.

Watoto wanaonyonya maziwa ya mama wana tindikali zaidi katika kinyesi chao, hali inayowakinga na vipele hivi. 

Pamoja na madhara ya mkojo na kinyesi pia maambukizi ya fangasi yanachangia utokeji wa vipele hivi. Tafiti zimeonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya watoto wenye vipele vinavyosababishwa na nepi walikuwa na maambukizi ya fangasi.  

Hali hii ya kutokea vipele huchangiwa na vitu vifuatavyo:

Hali ya unyevu, michubuko, kukaa na nepi yenye mkojo na kinyesi kwa muda mrefu, kuharisha kwa mtoto (kupata choo cha maji maji mara tatu au zaidi kwa siku.

Sababu nyingine ni madhara ya dawa za kuua bakteria (antibiotic adverse effects) na ukosefu wa madini ya biotin na zinc.  

 

Dalili za ugonjwa wa vipele vya nepi

Watoto wenye tatizo la vipele vya nepi huwa wanakuwa na michubuko na wekundu katika sehemu zinazofunikwa na nepi.

Wanaweza kuwa na vipele katika baadhi ya sehemu (patchy) au sehemu yote inayofunikwa na nepi (confluent).

Wakati mwingine vinaweza kutokea sehemu ya tumboni mpaka kwenye kitovu.

Watoto wanaweza kuwa na muwasho na wakati mwingine kujisikia vibaya.  

Vipele hivi vinaweza kusababisha watoto kupata maambukizi ya fangasi na hata bakteria na wakati mwingine huwa na maumivu makali (serious bacterial infection) 

 

Jinsi ya kumkinga mtoto na tatizo la vipele vya nepi 

Wazazi na walezi wanaweza kuwakinga watoto wao na tatizo hili kwa kuzingatia yafuatayo:

Kuweka ngozi ya mtoto safi na kavu, kubadilisha nepi mara kwa mara, nepi zinazotumika mara moja na kutupwa (disposable diapers) ni bora zaidi katika kuzuia tatizo la vipele vya nepi ukilinganisha na nepi za nguo.

Pia inashauriwa kuosha sehemu zinazofunikwa na nepi za mtoto kwa maji ya uvuguvugu na sabuni kidogo, kutumia mafuta yanayomkinga mtoto na vipele baada ya kumwogesha na kila unapombadilisha nepi.

Nini cha kufanya endapo mtoto wako ana vipele vya nepi

Iwapo mtoto wako ana vipele vya nepi kwa kiasi kidogo, unaweza kufuata maelekezo tajwa hapo juu ili kudhibiti hali hiyo.

Iwapo vipele ni vingi na mtoto ana michubuko na wekundu kwenye sehemu zake za siri, ni vyema ukampeleka kwa daktari kwa kuwa anaweza kuwa na maambukizi ya fangasi au bakteria.

Makala hii imeandaliwa na Dk. Francis Fredrick, MD.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles