23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

UHUSIANO WA KIMAPENZI, UGOMVI HUVURUGA AKILI ZA WANAWAKE

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

KUNA baadhi ya familia suala la ugomvi, vipigo na matusi kwao ni jambo la kawaida, hawafahamu kuwa hali hii inaweza kusababisha matatizo ya afya ya akili.

Matatizo haya yanazidi kuongezeka kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo maradhi, pombe na visa vya mara kwa mara katika jamii.

Uhusiano mbovu kwenye familia, ndoa au mapenzi ni miongoni mwa vitu vinavyochangia msongo wa mawazo, ambao huenda kuathiri afya ya akili moja kwa moja.

Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Said Bakari anasema suala hilo wengi bado hawajalibaini.

“Ni jambo ambalo tumeligundua hapa Muhimbili katika Idara ya Afya ya Akili, kwamba wakina mama wengi tunaowapokea sababu kubwa ya kuchanganyikiwa ni changamoto za uhusiano,” anasema.

Anasema ni vema familia zikaishi kwa umoja, upendo na mshikamano ili kuepuka changamoto hii.

“Kwa wanaume, tumegundua kuwa chanzo cha magonjwa ya akili kwao ni unywaji pombe kupita kiasi, ingawa wapo pia waliopata tatizo kutokana na sababu nyinginezo,” anasema.

Afya ya akili ni nini

Dk. Bakari anasema afya ya akili ni ule ustawi au kutengamaa kwa akili katika nyanja tofauti tofauti, kutambua mambo, kufikiria, kuhisi na kutenda.

“Jamii husika ndiyo ambayo huwa inafafanua kipi kimekuwa timamu na kipi si timamu, kwa hiyo kuna akili ambayo tunasema ni timamu na ambayo si timamu.

“Kama si timamu je, mhusika ni mgonjwa au si mgonjwa? Kwa mfano mtoto hatuwezi kusema ni mgonjwa bali huwa tunasema akili yake si timamu muacheni akikua ataacha.

“Ila jambo lile lile lililofanywa na mtoto likifanywa na mtu mzima hapo tunajua wazi si sawa na tunaweza kusema akili yake si timamu,” anasema.

Anasema kuwa hivyo wakisema magonjwa ya akili, wanamaanisha kwamba mtu huyo ameathirika kiakili hivyo kuna athari katika uwezo wake wa kuhisi, kutambua mambo na hatimaye kufanya matendo yake ya kila siku.

Daktari huyo anasema kwa kawaida huwa wanatambua hilo kutokana na jamii inayomzunguka mgonjwa husika.

“Kwa kawaida kila jamii ina namna ilivyokubaliana jinsi ya kuishi inapotokea mtu mwingine akaishi kinyume na makubaliano husika huanza kumchunguza mtu na wanao uwezo wa kubaini mwenzao kama yupo timamu au ana tatizo la akili.

 “Kwa mfano katika jamii yetu haiwezekani mtu mzima akasimama juani kuanzia asubuhi hadi jioni hatingishiki, au akatembea na vitu vya ajabu ajabu mtaani na uchafu wa hata mwezi mzima.

“Watu tunamuona jinsi alivyochafuka lakini yeye wala hajali, huyo moja kwa moja tunasema ana shida ya akili, kwa sababu anafanya jambo ambalo jamii haikubaliani nalo,” anasema.

Anafafanua kuwa akili ikihama katika ule uhalisia, au ukweli wa jamii husika itafahamika kwamba imeathirika. Lakini tatizo hili hadi liwe ugonjwa ni lazima kujiuliza vitu mbalimbali, kwa mfano je, limeathiri vipi utendaji kazi wa mhusika wa kila siku?

Anatoa mfano mathalani mtu hakupata usingizi mwezi mzima, anaenda ofisini anarudi halali, inafika kipindi hata kazi za ofisi haziendi kwa sababu umakini haupo, kila akienda anakaa tu haongei na mtu mara ameondoka nyumbani, au anakuja ofisini lakini mkali hakuna kitu anachokifanya kwa siku hiyo anaenda nyumbani, hapo wanaweza kusema mtu huyo ana tatizo la akili.

Yanatambulikaje

Anasema magonjwa ya akili yapo mengi lakini yamegawanyika katika maeneo makubwa mawili, yapo yale ambayo huambatana na kuchanganyikiwa akili yaani uwezo wa kutambua mambo kiuhalisia unakuwa umepotea. Anasema hapo ndipo utakuta mtu anaongea mambo ambayo hayaeleweki au anayaelewa mwenyewe katika ulimwengu wao, lakini wale wanaowatazama hawaelewi.

Anatoa mfano; “unaweza kusikia mtu anawasiliana na jua, au anaongea habari za jua utafikiri ni rafiki yake, au anawasiliana na Mungu katika hali ambayo sisi wengine hatujaipata, wala hatujaisikia kwenye kitabu chochote na tupo na imani sawa na huyo mtu, hii maana yake ni kwamba mwenzetu hayupo katika ile hali ya uhalisia.

“Kwa hiyo tunasema huyu mtu yupo katika hali ya kuchanganyikiwa, zipo namna nyingi za kuchanganyikiwa, maneno, mawazo na hisia zake zinaweza kuonesha hali ya kuchanganyikiwa kwa muhusika,” anasema.

Unaweza kuwa na akili timamu lakini mgonjwa

Anasema lipo kundi lingine ambalo linajumuisha watu wengi, hili ni lile ambalo halihusishi kuchanganyikiwa.

“Yaani mtu unakuwa na akili yako timamu lakini mgonjwa,  wengi hawajui kwamba huzuni ikizidi kiwango chake cha kawaida ni ugonjwa lakini muhusika anakuwa hajachanganyikiwa,” anasema.

Anasema hasira ambayo ni hali ya kawaida inayojitokeza katika kipindi fulani mtu anapoudhika lakini nayo ikipitiliza ni ugonjwa.

“Wapo ambao wanapata shida ya kudhibiti hasira hivyo kuwasababishia athari nyingi kwao wenyewe na jamii inayowazunguka, wakati mwingine akili ikichoka mtu huweza kuonesha dalili kwenye mwili wake, mfano kichwa kuuma hata miaka miwili kumbe wamehifadhi huzuni moyoni,” anasema.

Anaongeza; “wengine hufikia hatua hadi wanashindwa kutembea kutoka eneo moja hadi lingine kutokana na maumivu ya miguu na kwamba wanapowachunguza hugundua hali hiyo imetokana na msongo wa mawazo walionao.

“Wapo pia ambao hushindwa kuona vema. Nakumbuka wakati ule wa mlipuko wa mabomu Gongo la mboto na Mbagala (2009 na 2011) tulipokea watu kadhaa ambao walipata shida hii, macho yao yalikuwa hayaoni kabisa, wamepima vipimo vya macho lakini hawajagundua tatizo.”

Anasema walipopelekwa kwenye kitengo cha magonjwa ya akili waligundua kuwa hali hiyo ilisababishwa na tatizo la akili, wakawaeleza jinsi akili inavyoweza kusababisha mtu asione kabisa. Hivyo walipowapa ushauri na dawa wakarudi katika hali yao ya kawaida.

Anabainisha kuwa mtu anapopatwa na mshtuko wa akili anaweza pia kupata kiharusi (kupooza mwili), tatizo ambalo linatibika.

Visababishi vikuu

Anasema magonjwa ya akili hutokana na sababu nyingi ambazo zimegawanywa katika makundi makuu matatu.

“Kuna sababu za kibaiolojia, yaani kuna wakati mwili wenyewe unapopata shida fulani fulani husababisha akili yake ilipuke,” anasema.

Anasema zipo sababu za kijamii hasa pale inapotokea hali ya kutokuelewana na umasikini.

 “Kuna suala la kimazingira pia, iwapo mtu ataishi katika maeneo ambayo hakuna amani inaweza kumsababishia kupata mlipuko wa akili, wengine hupata kutokana na ulevi,” anasema.

Anasema zipo pia sababu za kisaikolojia, yaani uwezo wa mtu binafsi kukabiliana na changamoto za kimaisha.

“Kwa mfano; mtu akikukera au ukiwa na huzuni unachofanya ni kulia ili kuondoa dukuduku au unapigana, unakubali wakati mwingine unaamua kusamehe. Hali ya uwezo wa mtu kukabiliana na maeneo haya inatakiwa iwe imara hapo ndipo ataimarika kiakili, lakini yakiwa yana utata kidogo lazima atapata shida kwenye afya ya akili,” anasema.

Yanarithiwa

Daktari huyo ambaye pia ni mjumbe wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA), anasema zipo tafiti zinazobainisha kuwa magonjwa hayo pia hurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

“Tafiti zinaeleza kuna kemikali zipo kwenye ubongo zinaitwa kitaalamu ‘neural transimiters’ yaani vipashio taarifa, habari au ufahamu. Hivi mtu huzaliwa navyo vikiwa vipo katika uwiano sawa. Vinatakiwa viwe hivyo ili mtu afanye kazi zake katika hali ya kawaida.

“Sasa ule uwiano ukiwa na hitilafu huyo mtu anakuwa katika hatari ya kupata matatizo ya akili… si lazima apate lakini anakuwa katika hatari,” anasema.

Anasema uwiano huo unaweza kuharibiwa kwa vilevi, ugomvi wa mara kwa mara, hali ya kukosa amani na sababu nyinginezo.

“Kwa mfano; mtu akikasirika muda mrefu hizo kemikali zinabadilisha utaratibu wake, unaweza kukuta katika familia wamezaliwa watoto watano na wakifika umri wa kuanzia miaka 18 hadi 25 wanaanza kukabiliana na zile changamoto za kimaisha kwa mfano wanahitaji kumaliza shule, kwenda chuo, kufanya kazi nzuri sasa kama mtu ana hitilafu na anaishi katika mazingira yanayomsababishia msongo wa mawazo ile hitilafu yake inaanza kujionesha mapema.

“Kuna wagonjwa tunawatibu wamepata matatizo kwa kurithi, unakuta kizazi cha kwanza, pili na tatu kinaugua.

Vipimo vya kubaini hitilafu

Dk. Bakari anasema kwa sasa vipimo hivyo havipo hapa nchini lakini katika nchi zilizoendelea wataalamu wake wanao uwezo wa kupima iwapo mtu anakabiliwa na hitilafu.

“Wenzetu katika nchi zilizoendelea wanafanya upimaji, wanapima na wakiona kuna hitilafu muhusika hushauriwa kwamba vizazi vyake vinaweza kupata tatizo kwa hiyo awe makini katika kutengeneza vizazi vingine.

“Kwa hiyo, anaweza kuamua mwenyewe iwapo asizae ili kuepusha hali hiyo au azae lakini anakuwa tayari ameshajua kwamba kuna tatizo, maana hitilafu hiyo haiwezi kuondoshwa kwa namna yoyote ile,” anasema.

Anasema kwa kuwa kipimo hicho hakipo nchini hulazimika kuwatibu wagonjwa wao kwa dawa mbalimbali na kuwapa ushauri wa kisaikolojia.

“Mgonjwa anapoacha kutumia dawa anakuwa anajiongezea ukubwa wa tatizo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles