24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Singida bado pagumu kwa Yanga

NA MWANDISHI WETU

-SINGIDA

TIMU ya Yanga imeshindwa kutamba tena baada ya kulazimisha suluhu na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.

Hata hivyo, sare hiyo iliifanya Yanga kufikisha pointi 55 na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza michezo 22, ikishinda 17, sare nne na kupoteza mmoja.

Matokeo hayo pia yanaifanya Yanga kuendeleza rekodi zake mbovu za kutovuna pointi tatu katika uwanja huo tangu Singida United ilipopanda Ligi Kuu msimu uliopita.

Timu hizo zilikutana mara mbili msimu uliopita, ambapo katika mchezo wa Ligi Kuu msimu wa 2017/18 zilitoka suluhu, baada ya hapo ziliumana katika robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ambapo Yanga ililala kwa penalti 4-2, baada ya dakika tisini kwa sare ya bao 1-1.

Singida United imefikisha pointi 28 baada ya kucheza michezo 24, ikishinda saba, sare saba na kupoteza 12.

Mchezo huo ulianza kwa wenyeji kuanza kwa kasi wakilenga kupata bao la mapema, huku Yanga ikianza taratibu kwa kuwasoma wapinzani wao.

 Dakika ya tisa, Deus Kaseke, alipoteza nafasi ya wazi kuiandikia timu yake bao la kuongoza baada ya kupenyezewa pasi nzuri ya Herieter Makambo na kupiga shuti lililopanguliwa na kipa wa Singida United, Said Lubawa na kuzaa kona, ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Dakika ya 16, Habib Kiyombo, nusura aiandikie bao la mapema Singida United baada ya kushindwa kutumia vema makosa ya mabeki wa Yanga walioshindwa kuondosha hatari na mpira kumkuta na kupiga shiti lililokwenda nje ya lango.

Dakika ya 18, kipa wa Singida United, Ludawa, alifanya kazi ya ziada kupangua mkwaju mkali uliopigwa na Makambo baada ya kupokea pasi nzuri ya Feisal Salumu na kuachia shuti lililopanguliwa na kuzaa kona ambayo hata hivyo walishindwa kuitumia.

Dakika ya 22, Paulo Godfrey, aliipangua ngome ya Singida United na kuingia hadi ndani ya eneo la hatari kabla ya kuachia mkwaju uliokwenda nje ya lango.

Dakika ya 24, Boniface Maganga, alilimwa kadi ya njano baada ya kumzonga kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili.

Dakika ya 45, Kabwili alifanya kazi ya ziada kupangua mpira wa kichwa uliopigwa na Boniface Maganga na kuzaa kona ambayo Singida United walishindwa kuitumia.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana, huku walinda milango wa pande zote mbili wakifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo hatari iliyoelekezwa kwenye lango lao

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuja juu wakihitaji kupata bao la kuibuka na ushindi, huku wenyeji wao, Singida United nao wakiongeza kasi ya kusukuma mashambulizi makali kuelekea lango la Yanga.

Dakika ya 47, Salum, alipoteza nafasi ya wazi ya kuiandikia Yanga bao baada ya kukutana na mpira uliopanguliwa na kipa wa Singida United kufuatia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Thaban Kamusoko na kuachia shuti lililopaa juu ya lango.

Dakika ya 55, Salum, alilimwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Kenny Ally.

Dakika ya 58, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kuwatoa Kelvin Yondani na Matheo Anthony na kuwaingiza Andrew Vicent na Pius Buswita.

Dakika ya 65, Kocha wa Singida United, Dragan Popadic, alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kumtoa Athanas Adam na kumwingiza Geofrey Mwashiuya.

Dakika ya 66, beki wa Singida United, Kennedy Juma, alilimwa kadi ya njano  baada ya kumchezea rafu, Pius Buswita.

Dakika ya 67, Yanga ilimfanya mabadiliko mengine ya kumtoa Salum na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Ajib.

Dakika ya 77, Makambo alipoteza nafasi ya wazi baada ya kupokea pasi safi ya Ajib akiwa katika nafasi nzuri, lakini mkwaju wake ulishindwa kulenga lango na kwenda nje.

Dakika ya 83, Singida United ilifanya mabadiliko baada ya kumtoa Kiyombo na kumwingiza Frank Mkumbo.

Dakika ya 90, Makambo alilimwa kadi ya njano baada ya kubishana na mwamuzi.

Mbali na mchezo, ligi hiyo iliendelea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali, ambapo JKT Tanzania ikiwa nyumbani ilivuna ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Biashara United katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Meja Jenerali  Michael Isamuhyo, Dar es Salaam.

Stand United iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Tanzania Prisons iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mbeya City ikiwa ugenini iliwachapa wenyeji wao, Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, nayo Lipuli FC ilizinduka na kuilaza KMC bao 1-0 mchezo uliochezwa Uwanja wa Samora, Iringa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles