28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: Changamoto za kuwa mwanamke nchini India

JOSEPH HIZA NA MITANDAO

BINTI mwenye umri wa mwezi mmoja Khushi, neno linalomaanisha ‘furaha’ kwa Kihindi, angeweza kuishi kama mama yake, Sumanjeet angesalimu amri dhidi ya shinikizo kali alilopata kutoka kwa baadhi ya ndugu na majirani zake.

“Wangelia, wangenipigia kelele na kunipayukia kwa mengi kama vile; “Unafaidika nini kwa kuzaa msichana? Msukume huyo kutokea paa la jengo, afie mbali! Kwanini unamlea?’’ mama huyo mwenye umri wa miaka 25 anakumbushia.

Sumanjeet pia anasema watu humtaka aende kunyofoa viumbe wanne wa kike waliopo tumboni.

Humwambia kwamba angeweza kuwa na fedha kwa ajili ya kuwapatia mahari ya kutosha watakapozaliwa na kuwa tayari kuolewa.

Ijapokuwa Sumanjeet hakuwa na uhakika wa namna atakavyowalea ‘malaika’ wake watarajia, alijua ni kosa la jinai kuwaua, mbali ya kuwa dhambi na ukatili.

“Kwanini wanaua wasichana, wakati wakiwa bado tumboni? Hii ni dhambi kubwa, ambayo watapaswa kuijibu kwa Mungu. Wasichana wadogo wasiojua chochote kama mdoli, wanawaua tumboni? Ni dhambi,” anapofikia hapo, Sumanjeet anashindwa kujizuia anaangua kilio.

Mbali ya hayo, vitendo vya wanaume kuwabaka wasichana kwa zamu ni vya miaka mingi na havikuwa vikipigiwa kelele hadi hivi karibuni.

Kubakwa kwa msichana mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23 akiwa kwenye basi mjini New Delhi kulizua hasira na maandamano nchini humo miaka kadhaa iliyopita, hali iliyoitetemesha serikali na kulazimisha kutungwa sheria kali dhidi ya wabakaji.

Kama unadhani tukio hilo na kutungwa kwa sheria ya adhabu ya kifo kungepunguza vitendo hivyo, unajidanganya, kwani ni kama vile zilivichochea kutokana na kwamba tayari vimekuwa sugu na vinaendelea hadi leo.

Hivi karibuni mwanamke mmoja alibakwa hadi kufa na kundi la wanaume 45 huku wasichana watatu wa ukoo mmoja wakiuawa kwa kitanzi baada ya kubakwa na genge lingine.

Wimbi la hasira za wanaharakati wanawake kote nchini humo, ambalo pia lilichangia anguko la kilichokuwa chama tawala cha Congress kipindi kile kwa kile kilichoelezwa kushindwa kuzuia, linaashiria udhalili na taabiko wanazokumbana nazo wanawake wa India katika maisha yao ya kila siku.

Maelfu ya watu walimimiika mitaani kupinga si tu kuhusu ubakaji bali pia kwa ujumla wake ukandamizaji wa wanawake nchini India, ambao mara nyingi unadumu katika sehemu nzima ya maisha yao.

Kura ya maoni iliyoendeshwa na Mfuko wa Thomson Reuters mwaka miaka mine iliyopita uliiorodhesha India kama nchi ya nne hatari kabisa duniani kwa wanawake kuishi ikiwa mbele ya Afghanistan, Congo na Pakistan tu.

Pamoja na kwamba utoaji mimba umeharamishwa,  mimba kati ya 300,000 hadi 600,000 zinazoashiria kuzaliwa kwa mtoto wa kike hunyofolewa kila mwaka nchini India kwa sababu jamii  hupendelea kuzaa wavulana, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2011 wa Jarida la Sayansi la The Lancet.

Na ukandamizaji, ambao huanzia kwao tangu wawapo tumboni mwa mama na huendelea katika kipindi chote cha maisha ya usichana wao hadi utu uzima.

Mwanaharakati wa haki za wanawake na Mwanasheria wa Mahakama ya Juu, Kirti Singh anasema kuna tofauti ya dhahiri ya namna wazazi wengi wanavyowachukulia watoto wao wa kike na kiume.

Anasema wasichana hawapewi chakula kile kile, hawasomeshwi sawa na wenzao na hulelewa ili waje kuwa wake wa fulani.

“Kuanzia kipindi wanachozaliwa au kutozaliwa hadi wanapokuwa wake au kina mama, mzunguko katili wa maisha wa kikandamizaji na kinyanyasaji huendelea.”

Sumanjeet anasema kuwa ameyaona yote hayo. “Huwapeleka wavulana katika shule nzuri, huwapatia chakula kizuri, nguo nzuri za kuvaa. Wanawalea vyema. Utawasikia kitu kama, ‘Oh, huyu ni mwanangu.’ Kwa binti husikika wakisema, “Wee! Hebu ondoa kinyesi cha ng’ombe, fagia sakafu. Shule itakusaidia nini?'”

Karibu nusu ya wasichana wa India huozwa kabla hawajafikisha umri wa miaka 18. Sumanjeet mwenyewe alilazimishwa kuolewa na mwanaume mwenye umri mkubwa wa miaka 15 kuliko yeye wakati akiwa na umri wa miaka 12 tu.

Anasema kuwa hakukataa ndoa hiyo kwa sababu hakuwa akijua kinachoendelea.

Wasichana pia huhesabiwa kama hasara kwa familia kifedha. Mara wanapoolewa, huondoka nyumbani na mara nyingi hutakiwa kuchukua kiwango kikubwa cha mahari pamoja nao, ambacho wakati mwingine huigharimu familia akiba yao nzima.

Utamaduni huu mkongwe nchini humo umepigwa marufuku na serikali, lakini bado umeenea nchini humo.

Mara wanapoolewa, wanawake wengi hukumbana na unyanyasaji wa majumbani.

Utafiti wa mwaka 2012 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) ulibaini kuwa zaidi ya nusu ya wanaume watu wazima wanadhani ni haki kumpiga mke katika hali fulani.

je ya kaya, uhalifu dhidi ya wanawake nchini India pia unazidi kuongezeka na ushahidi unatisha.

Julai 2012, msichana mdogo wa shule alidhalilishwa kijinsia na kutomaswa tomaswa na kundi la wanaume 18 kwa dakika 45 katika jimbo la kaskazini mashariki la Assam.

Watu walioshuhudia walirekodi tukio hilo kwa simu zao na wengine video camera, lakini hakuna aliyejitokeza kumsaidia msichana huyo.

Septemba 2012, msichana mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16 alibakwa na wanaume nane kwa zamu na baba yake alijinyonga kukwepa aibu hiyo.

Dakika tu  20 kutoka jiji la Jhajjar, mama wa watoto wanne aliburuzwa kutoka nyumbani kwake na kubakwa na wanaume watano.

Alisema aliburuzwa kutoka kitandani kwake kwenda kwenye zizi la ngombe, ambako walimbaka kwa zamu. Wanaume hao walikimbia wakati watoto wa mama huyo walipoamka.

Kesi hizo chache miongoni mwa maelfu hazikuripotiwa zaidi ya kuishia huko huko katika jamii husika kabla ya hivi karibuni genge la wanaume la Delhi kumbaka msichana hadi kufa na kuibua picha ya kiwango cha manyanyaso kinachowakabili wanawake nchini humo.

“Tofauti ni kwamba sisi tu masikini, hatusikiki na wakati tunapoenda vituo vya polisi kuripoti, hatusikilizwi. Tunataka haki,” alisema.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali kesi 24,000 za ubakaji ziliripotiwa mwaka 2011.

Sehemu kubwa ya kesi hazikuripotiwa kwa sababu ya unyanyapaa unaozingira wanaobakwa, ambao wakati mwingine mbali ya kujiua, huuawa na familia zao ili kuficha aibu.

Lakini pia wanawake wa India kwa namna fulani wanapiga hatua. Kiwango cha kuelimika kimeongezeka miongoni mwa wanawake na idadi ya vifo vya uzazi imepungua huku mamilioni ya wanawake wakiunganisha nguvu.

Viongozi kama vile Rais wa Baraza la Ushauri la Taifa (NAC) na mjane wa Waziri Mkuu wa zamani marehemu zamani  Rajiv Gandhi, Sonia Gandhi ni kioo kuwa wanawake wanaweza kuinuka. Lakini bahati mbaya kuna changamoto.

Mamlaka zinakiri hatua za makusudi zinatakiwa ili kujaribu kuwalinda wanawake. Miongoni mwa hatua zilizopangwa kuchukuliwa ni kuajiri zaidi maofisa wa polisi wanawake.

Kwa sasa ni asilimia saba tu ya jeshi la polisi ni wanawake.

Hatua nyingine ni kuwekwa makali zaidi kwa sheria zinazohusu vitendo vya udhalilishaji wanawake na kuangalia nini kifanyike kuufanya mji wa Delhi kuwa salama.

Lakini wanaharakati wa haki za wanawake wanasema wakati ukandamizaji wanawake unapoendelea kabla ya uzazi, mabadiliko kamwe hayatakuja kirahisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles