Simba yavunja mwiko Kagera

0
754
Kiungo wa Simba, Sharaf Shiboub (kulia), kichuana na beki wa Kagera Sugar, Isihaka Hassan katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba. Simba ilishinda mabao 3-0. Picha na Maregesi Nyamaka.

NYEMO MALECELA-BUKOBA

TIMU ya Simba imevunja mwiko katika Dimba la Kaitaba, mjini Bukoba, baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 3-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana.

Mabao ya Simba katika mchezo huo, yaliwekwa kimiani na Meddie Kagere dakika ya nne na 77, huku lingine likifungwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dakika ya 35.

Wekundu wa Msimbazi hao wamefuta rekodi mbovu ya kufungwa na Wakata Miwa hao wa Kagera katika michezo mitatu mfululizo misimu miwili iliyopita.

Vijana wa Kagera Sugar wanaonolewa na Mecky Mexime, waliandika rekodi ya kuwa timu pekee iliyovuna pointi sita mbele ya Simba msimu uliopita, baada ya kushinda mechi zote mbili, yaani nyumbani na ugenini.

Ushindi wa jana unaifanya Simba kufikisha pointi tisa na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikiiengua Kagera Sugar iliyokuwa ikishilia usukani huo.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Kagera ikionekana kujiamini zaidi na kutengeneza mashambulizi kuelekea lango la Simba.

Lakini Simba ilizima cheche zao hizo pale Kagere alipozitikisa nyavu za wenyeji wao dakika ya nne, akifanya hivyo kwa kichwa kutokana na krosi ya Deo Kanda.

Kabla ya Kanda kupiga krosi, alitengewa mpira kwa pasi maridadi kutoka kwa Ibrahim Ajib ambaye jana alikuwa katika kiwango bora.

Hata hivyo, fundi huyo alijikuta matatani dakika ya 10 baada ya kulimwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi kiungo wa Kagera Sugar, Awesu Awesu.

Beki wa Kagera Sugar, Erick Kyaruzi alifanya kazi ya kumdhibiti ya Kagere aliyekuwa akielekea kumsabahi mlinda mlango wa timu hiyo, Said Kipao, hiyo ikiwa ni dakika ya 29.

Tshabalala aliindikia Simba bao la pili dakika ya 35 baada ya kugongeana pasi fupi fupi na Kagere hadi ndani ya eneo la hatari la Kagera kabla ya kuachia shuti lililomshinda Kipao na kujaa wavuni.

Kiungo wa Kagera, Zawadi Mauya alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Ajib, hiyo ikiwa ni dakika ya 40.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Simba kutoka kifua mbele kwa mabao 2-0, kabla ngwe ya pili kuanza kwa Mexime kufanya mabadiliko, akimtoa Kyaruzi na kumwingiza Juma Nyoso.

Naye kocha wa Simba, Patrick Aussems, alimtoa Kanda na nafasi yake kuchukuliwa na Miraji Athumani, hiyo ikiwa ni dakika ya 61.

Dakika ya 71, Ajib alitoka baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa Hassan Dilunga.

Kagere aliindikia Simba bao la tatu dakika ya 77 kwa mkwaju wa penalti uliotokana na Miraji kuangushwa ndani ya eneo la hatari wakati akiwa katika harakati za kufunga.

Dakika ya 87, Wilker da Silva aliingia kuchukua nafasi ya Kagere.

Hadi dakika 90 za mtanange huo zinakamilika, Simba iliondoka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Kagera: Said Kipao, Mwaita Gereza David Luhende, Hassan Isihaka, Erick Kyaruzi ‘Moppa’/ Juma Nyoso, Zawadi Mauya,  Awesu Awesu, Ally Ramadhani, Avarigestus Mujwahuki, Abdallah Seseme, Yusuf Mhilu/Peter Mwalyanzi.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’,  Tairone Santos, Pascal Wawa, Gerson Fraga,  Deo Kanda/Miraji Athuman, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere/Wilker da Silva, Sharaf Shiboub na Ibrahim Ajib/Hassan Dilunga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here