33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mawasiliano ya Trump kuchunguzwa kwa kina

WASHINGTON, MAREKANI

MAWASILIANO ya simu yanayotajwa kuwa na nia ya kumwangamiza Joe Biden ambaye ni mpinzani wa kisiasa wa Rais Donald Trump, wa Marekani, sasa yatachunguzwa kwa kina baada ya Ikulu kutoa muhtasari wake.

Malalamiko hayo yanahusu mawasiliano tata ya simu baina ya Rais Trump na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Tayari wabunge wa baraza la Congress nchini Marekani wameona kwa mara ya kwanza malalamiko ya mtu aliyefichua malalamishi dhidi ya Trump yaliyosababisha wito wa kutaka achunguzwe.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Marekani Joseph Maguire jana alifika mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya masuala ya ujasusi kutoa ushahidi juu ya suala hilo.

Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC limeandika kuwa malalamishi  hayo dhidi ya Trump yatachunguzwa kwa kina ingawa kwa sasa bado ni siri.

Lakini afisa wa ngazi ya juu kabisa wa Democrat katika bunge la seneti la Marekani Chuck Schumer, ametoa wito maelezo hayo yafichuliwe.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano jioni kwa mara nyingine tena Rais Trump alipuuzia mbali uchunguzi dhidi yake akiutaja kuwa “feki ” na “wenye hila”.

Katika ujumbe wake wa twitter Jumatano, Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden  alimshutumu Trump “kutumia vibaya madaraka yake.

Wabunge wa Democrat wanamshutumu Trump kwa kutaka usaidizi kutoka Ukraine ili kumuangamiza hasimu wake wa kisiasa, Biden.

Mazungumzo hayo ya simu yamewafanya wabunge kutoka chama cha upinzani cha Democrats kuanzisha uchunguzi rasmi wenye lengo la kumng’oa madarakani Trump.

Ikulu ya White House imetoa taarifa ya kina juu ya mazungumzo ya simu baina ya Trump na mwenzake wa Ukraine.

Taarifa ya White House imethibitisha kuwa, Julai 25, Trump alimuomba Rais Volodymyr Zelenski kumchunguza Biden anayesaka tiketi ya urais kupitia chama cha Democrats, ambaye mtoto wake alikuwa akifanya kazi na shirika la gesi la Ukraine.

Trump anakanusha kuwa alizuia msaada wa kijeshi kwa Ukraine kama njia ya kuishinikiza nchi hiyo kumsaidia kumchafua adui yake wa kisiasa, Biden.

Taarifa juu ya mazungumzo hayo ya simu yametolewa na mtoa taarifa wa siri.

Spika wa Bunge la congress kutoka chama cha Democrat Nancy Pelosi amesisitiza  kuwa Rais Trump “lazima awajibike’.

Jumanne Trump aliahidi kutoa ushirikiano wa kikamilifu juu ya suala hilo kwa kuchapisha mazungumzo yote bila kuondosha hata kipande.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House haikuwa nakala ya mazungumzo, bali muhtasari wa mazungumzo hayo ambao uliandaliwa na maafisa wa Ikulu hiyo waliokuwepo wakati wa mazungumzo hayo yakifanyika.

Mazungumzo hayo ya simu baina ya maraisi hao wawili yalifanyika siku chache baada ya Trump kuiagiza serikali yake kuzuia msaada wa kijeshi wa dola milioni 391 kwenda Ukraine.

Katika mukhtasari wa White House suala hilo la msaada wa kijeshi halijagusiwa.

MAZUNGUMZO YENYEWE

Kwa mujibu wa mukhtasari, Trump alimwambia Zelensky juu ya namna ambavyo Joe Biden akiwa makamu wa rais alishawishi Ukraine kumtimua kazi mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin mwaka 2016.

Ofisi ya Shokin ilifungua jalada la uchunguzi dhidi ya Burisma, kampuni ya gesi asili ambayo mtoto wa, Hunter alikuwa ni mjumbe wa bodi yake.

Nchi kadhaa za magharibi pia zilikuwa zikishinikiza Shokin atimuliwe kazi kwa madai alikuwa akivumilia vitendo vya rushwa.

“Nimesikia mlikuwa na mwendesha mashtaka ambaye alikuwa ni mzuri kweli na alifutwa kazi kwa njia ya uonevu. Watu wengi wanalizungumzia jambo hilo,” Trump ananukuliwa akisema kwenye mazungumzo hayo na kuongeza:

“Kitu kingine, kuna mjadala mkubwa kumhusu mtoto wa Biden, kuwa baba yake alizuia waendesha mashtaka na watu wengi wanataka kujua undani wa hilo, so chochote unachoweza kufanya na Mwanasheria Mkuu (wa Marekani) litakuwa jambo jema.

“Biden alikuwa akijitamba kuwa amezuia uchunguzi angalia utakachokifanya hapo…ni jambo baya sana kwangu.” Anadaiwa kusikika Trump katika mazugumzo hayo

Zelensky naye anaripotiwa kujibu”Tutalishughulikia hilo na tutafanyia kazi uchunguzi wa kesi hiyo.

“Juu ya hilo, pia ningeomba kama una taarifa zozote za ziada pia tupatie, zitatusaidia sana.”

Akimshukuru Trump, Zelensky alisema kuwa alikaa kwenye jumba lake la jijini New York, Trump Tower, mara ya mwisho alipozuru nchini humo.

Huku kukiwa na uungaji mkono mkubwa kutoka kwa wafuasi wa Democrat juu ya uchunguzi huo unaoweza kumuondoa madarakani, ikiwa utaendelea huenda usipitishwe na baraza la seneti – linalodhibitiwa na wabunge wa chama cha Trump cha Republican.

Akitangaza uamuzi huo, Pelosi alisema kamati nyingine sita zinazofanya uchunguzi wa masuala mengine dhidi ya Trump zitaendelea na uchunguzi wao chini ya uchunguzi wa sasa.

Ikiwa uchunguzi huu utaendelea, Bunge la wawakilishi litapigia kura mashtaka yoyote yatakayobainika na kwasababu Democrat ndio wengi katika bunge la congress wanaweza kupitisha umuzi wa kumshtaki.

Hata hivyo maamuzi hayo yanaweza kupelekwa katika bunge la Seneti ambako theluthi tatu ya wabunge inahitajika kupitisha maamuzi – na huko Republicans wataweza kuzuwia mashtaka.

Spika Pelosi alisema kuwa Trump amefanya kosa la “ukiukaji wa sheria “, na kuyataja matendo yake kama “uvunjaji wa wajibu wake wa kikatiba”.

Kwa upande wake Biden amekanusha kufanya kosa lolote na pia anaunga mkono juhudi za kumfanyia upelelezi Rais Trump iwapo hataonyesha ushirikiano katika sakata hilo dhidi yake.

Kura ya maoni iliyoendeshwa na shirika la A YouGov imeonyesha kuwa  asilimia 55 ya Wamarekani wangeunga mkono kushtakiwa kwa Trump ikiwa itathibitishwa kwamba alisitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine ili kuwashinikiza maafisa wa nchi hiyo kumchunguza Biden.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles