30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Simba yampa timu Mayanja, wachezaji wagawanyika

Jackson MayanjaMWALI IBRAHIM NA THERESIA GASPER, DAR

UONGOZI wa Simba umemtangaza rasmi Jackson Mayanja kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, huku ukimfungashia virago Mwingereza, Dylan Kerr na kocha wa makipa wa timu hiyo, Idd Salim.

Makocha hao jana waliwasili Dar es Salaam kutokea Zanzibar, wakiitikia wito wa uongozi wa timu uliowaita mara moja, ndipo walipokutana na dhahama hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa idara ya mawasiliano klabu ya Simba, Haji Manara, alisema maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia kikao cha kamati ya utendaji kilichokaa jana, ambapo kiliafikiana kwa pamoja na walimu hao kuvunja mikataba kwa faida ya pande zote mbili.

“Kwa masikitiko makubwa tunapenda kuutaarifu umma kupitia vyombo vya habari kuwa tumevunja mkataba na makocha hawa na kwa sasa timu itakuwa chini ya kocha Mayanja wakati mchakato wa kumpata kocha mkuu ukiendelea,” alisema.

Wachezaji walikabidhiwa kwa kocha Mayanja jana asubuhi wakiwa Zanzibar na kuanza mazoezi jioni katika Uwanja wa Mbigani chini yake wakijiandaa kuivaa Mtibwa Sugar, Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mayanja alisema anachohitaji ni ushirikiano kwa pamoja ili kuhakikisha anaifikisha timu hiyo inapotakiwa kulingana na hadhi yake.

“Simba ni timu kubwa na ina wapenzi  na mashabiki wengi, hivyo ni vizuri tukapeana ushirikiano ili kuijenga timu hii na kufika pale tunapopataka,” alisema.

Hata hivyo, habari zilizolifikia  MTANZANIA baada ya kutambulishwa Mayanja zinasema kuwa wachezaji wamepokea taarifa ya kutemwa kwa kocha huyo kwa huzuni huku wakiishia kunung’unika.

Mchezaji Abdi Banda, amepinga maamuzi ya kuondolewa kwa Kerr katika timu hiyo na jana jioni aliondoka kambini na kurudi Dar es Salaam.

“Wachezaji wamekasirika na kudai kuwa wamekuwa wanabadilishiwa makocha bila kutaarifiwa wakati wakiwa wanakabiliwa na mechi, hivyo kutokana na kutoridhika huko, Banda ameamua kubeba mizigo yake na kurudi kwao wakati wenzake wakienda mazoezini,” kilisema chanzo cha habari hizo.

Kerr alisaini mkataba wa kuitumikia Simba mwanzoni mwa msimu huu, akimrithi aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Goran Kopunovic, huku akiwekewa masharti ya kuhakikisha timu hiyo inatetea ubingwa wake wa Kombe la Mapinduzi pamoja na kumaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Tanzania bara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles