31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mexime aahidi kuwafuta machozi Yanga

Mecky MeximeNA MICHAEL MAURUS, ZANZIBAR

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime, amesema kuwa kikosi chake kimejipanga vema kuelekea mchezo wa leo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi utakaopigwa Uwanja wa Amaan, huku akiahidi kuwafunga URA ambao waliwatoa Yanga katika hatua ya nusu fainali Jumapili iliyopita.

Mchezo huo wa kuhitimisha michuano hiyo utaanza saa 2:00 usiku, ukitarajiwa kuwa mkali kutokana na ubora wa timu zote mbili.

Wakati URA wakiitoa Yanga kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90, Mtibwa waliwafungasha virago Simba kwa ushindi wa bao 1-0, shujaa wao akiwa ni kiungo, Ibrahim Jeba.

Na kutokana na ubora wa Mtibwa na URA, wadadisi wa mambo ya soka visiwani hapa wamekuwa wakishindwa kutabiri ni timu gani kati ya hizo inayoweza kutwaa ubingwa.

Japo URA inaonekana kuwa timu hatari zaidi, lakini Mtibwa nao si wa kubeza, wakiwa wanacheza kwa mipango, huku wachezaji wake wakiwa si ‘mabishoo’ ambao wanawajibika vilivyo kwa kufuata maelekezo ya makocha wao, huku pia wakivitumia vema vipaji vyao katika mchezo huo.

Akiuzungumzia mchezo huo wa leo, Mexime alisema wapinzani wao hao hawamtishi akiamini ni wa kawaida tu kama ilivyokuwa kwa timu nyingine walizocheza nazo ikiwamo Simba waliyoifunga.

Alisema wamejiandaa kucheza kwa umakini wa hali ya juu, wakifahamu kuwa kosa lolote linaweza kuwagharimu, hivyo wapenzi wa Yanga wafike kwa wingi uwanjani kushuhudia watakavyowalipizia kisasi kwa Waganda hao.

“Kikosi chetu kipo vizuri na tumejiandaa kwa mchezo huo wa fainali, hivyo tuna imani kubwa tutawafunga URA na kutwaa ubingwa wa mashindano haya,” alitamba Mexime.

Kwa upande wake, mfungaji wa bao la kusawazisha la URA dhidi ya Yanga, Peter Lwassa, alisema: “Mtibwa si timu ya kubeza, tutakabiliana nao kwa umakini mkubwa na matarajio yetu ni kushinda.”

Mchezo huo utachezwa ikiwa ni baada ya sherehe rasmi za maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanyika jana visiwani hapa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles