24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ni Simba, Rekodi Yanga

yanga-vs-simba-leo

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

DAKIKA 90 zitaamua nani mbabe katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayowakutanisha watani wa jadi, Yanga na Simba katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo.

Mechi hiyo yenye hamasa kubwa kwa mashabiki wa timu hizo itachezeshwa na mwamuzi, Martin Saanya kutoka mkoani Morogoro, atakayesaidiwa na Samwel Mpenzu (Arusha) na Ferdnand Chacha (Mwanza).

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani wa aina yake kutoka katika vikosi vyote viwili, ni mchezo wa kwanza timu hizo kukutana tangu ilipoanza Ligi Kuu Tanzania Bara ya msimu wa 2016/17 na inaonekana kila upande ukitaka kushinda mechi hiyo.

Yanga inajivunia kasi ya wachezaji wake ambao wamekaa pamoja kwa muda mrefu wakati Simba wao wakiwa na uhakika wa kupata ushindi kulingana na usajili walioufanya msimu huu.

Watani hao wa jadi wanakutana kwa mara ya 83 huku Yanga ikiongoza kwa kuifunga Simba mara nyingi licha ya ukweli kuwa Simba nao wanajivunia kuwafunga watani zao kwa idadi kubwa ya mabao ambayo hadi sasa inaonekana kama deni lisiloweza kulipwa.

Simba iliyo chini ya kocha Mcameron, Joseph Omog, inaonekana kuwa na hasira zaidi na Yanga, kwani licha ya msimu uliopita kushindwa kupata ubingwa, lakini pia walijikuta wakipata machungu ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu wao hao.

Inakumbukwa kuwa msimu uliopita Simba ilijikuta ikipokea kipigo hicho katika mechi zake zote mbili, lakini hali hiyo ikidaiwa imejitokeza kutokana na ubovu wa kikosi chao.

Hivyo Simba wanaamini kuwa mabadiliko makubwa waliyoyafanya msimu huu kwenye kikosi chao ndiyo chachu ya kumaliza machungu ya vipigo vya msimu uliopita.

Kwa upande wa Yanga wamekuwa na kocha wao,  Hans van de Pluijm, msimu huu hawajafanya mabadiliko makubwa lakini pia wakijipa matumaini ya kuwa pamoja kwa muda mrefu ndiyo silaha yao kubwa.

MAANDALIZI

Wakati timu zote zikitokea mafichoni, Simba wanatokea Morogoro, Yanga wao walipiga kambi Pemba.

Simba wanaingia katika mechi hiyo wakiwa hawajapoteza mechi katika ligi tangu ianze huku pia  wakiwa kileleni kwa pointi 16 kwenye msimamo katika michezo sita na hivyo kuonekana wamewazidi watani wao ambao wana mechi moja mkononi.

Yanga hadi sasa wamecheza mechi tano na wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 10 baada ya kupoteza mechi moja dhidi ya Stand United.

Mabao

Katika kufunga na kufungwa, Simba inaonekana kuipoteza Yanga kwani imevuna mabao 12, wakati watani zao wakifunga manane huku kwa upande wa kufungwa Yanga inaonekana kuwa makini zaidi kwani imeruhusu bao moja tu ambalo walifungwa na Stand Jumapili iliyopita wakati Simba nyavu zao zikiguswa mara mbili kwenye ushindi wao wa mabao 2-1 (Ruvu Shooting) na mabao 3-1 (Ndanda).

Hii inamaanisha kuwa ili walingane kwenye mabao Yanga wanatakiwa kuifunga Simba mabao 4-0.

Vikosi

Tangu kuanza kwa ligi msimu huu, Yanga imewakosa wachezaji wake, Geofrey Mwashiuya, Said Makapu na Malimi Busungu ambao wapo kwenye kuuguza majeraha tofauti, pia iliwakosa Ally Mustapher ‘Barthez’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani, waliokuwa wakisumbuliwa na majeraha lakini kwa sasa wapo fiti.

Kwa Simba haijawakosa wachezaji wake muhimu licha ya kipa Dennis Richard na Awadhi Juma ambao hawana tatizo lakini wamekosa namba katika kikosi cha kocha Omog, wakati Mwinyi Kazimoto na Hamad Juma wakikosa mechi kadhaa kutokana na kupata maradhi huku Mussa Ndishi akishindwa kuitumikia timu hiyo kutokana na kukosa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC).

Kasi

Simba wanaonekana wapo vizuri zaidi tofauti na watani zao ambao inawezekana suala la uchovu baada ya kucheza mechi nyingi pasipo kupumzika huku Pluijm akiwatumia wachezaji walewale linaonekana kuwaathiri.

Makocha

Kocha wa Yanga ambaye amekinoa kikosi hicho kwa zaidi ya misimu miwili sasa, ameweka wazi kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na kila timu kuhitaji kushinda.

“Hatutaingia uwanjani tukitaka ushindi kwa sababu ni mechi ya watani pekee, ila tunahitaji kufuta kovu la mechi moja tuliyopoteza lakini pia kuendeleza rekodi yangu nzuri niliyoiweka msimu uliopita.

“Kwa sasa nimekiandaa kikosi changu kulingana na mahitaji ya mechi hiyo, lakini sitaki kuwapa presha wachezaji wangu juu ya Simba, kikubwa kila mechi tunahitaji matokeo ya pointi tatu hivyo tutaingia kama inavyokuwa katika mechi nyingine, tofauti iliyopo ni mashabiki wanavyoipa kipaumbele mechi hiyo kutokana na historia ya timu hizi mbili,” alisema Pluijm.

Kwa upande wa Omog ambaye aliwahi kutoka sare na Yanga mara mbili kipindi akiinoa Azam kabla ya kutimuliwa, mechi ya leo itakuwa ya kwanza kwake itakayotoa tathmini ya ubora wake, lakini akitupiwa jicho la tatu kwa kuwa kila Mwanamsimbazi anahitaji ushindi.

Omog anasema itakuwa mechi ngumu kwani analifahamu soka la Tanzania, hususani zinapocheza timu zenye upinzani mkubwa, lakini akiwataka mashabiki kuwaachia kazi wachezaji wake ili watekeleze majukumu aliyopata kwani anaamini hawatafanya makosa.

“Mechi ni ngumu, lakini naomba tu mashabiki waje kutushangilia na kutupa nafasi ya kufanya kazi yetu uwanjani, nina hakika wachezaji wangu hawataniangusha,” alisema Omog.

Manahodha

Nahodha msaidizi wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema: “Ninajua mashabiki wanahitaji ushindi nami ninawaahidi tutazitumia vizuri dakika 90 za mechi kuhakikisha tunawapa kile wanachokihitaji.”

Naye Jonas Mkude aliyebeba mikoba ya Mussa Hassan ‘Mgosi’ ndani ya Simba, anasema: “Kuvaa kitambaa hicho katika mechi ya watani ni mara ya kwanza, lakini ana imani itakuwa ni mechi ya kihistoria kwa upande wake pale atakapoliongoza jahazi kuwaangamiza wapinzani wao.

“Sijaona kitu cha kutupa wasiwasi kutoka kwa wapinzani kwani kikosi chetu kinanifanya nijiamini,  tunaweza kuwafunga lakini pia kwangu inaweza ikawa ni mechi ya historia kuona naongoza mashambulizi ya kuwahukumu watani zetu,” alisema Mkude.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles