25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SHUKRANI ZA MAXENCE MELO KWA WATANZANIA

photo

Na MAXENCE MELO,

KWANZA namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuiona siku ya leo nami kuwa nanyi siku hii ninapoandika waraka huu mfupi ukilenga zaidi kutoa shukrani.

Shukrani hizi nilitamani nimtumie mmoja mmoja lakini nimeshindwa kwani ni wengi wanaostahili kushukuriwa.

Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kupaza sauti zao (kwa njia yoyote ile) ili aidha nifikishwe mahakamani au niachiwe bila masharti yoyote (nilipokuwa Kituo cha Kati) na baadaye kuendelea kupaza sauti kutaka mahakama initendee haki niwe huru baada ya kupelekwa gerezani Keko.

Nawashukuru mawakili wangu na wengine walioamua kujitolea kuingia katika utetezi wangu hata bila kuombwa.

Kipekee, namshukuru na kumpa pole sana ndugu yangu, Albert Msando, ambaye tayari alishaonesha nia ya kuwa mtetezi wangu lakini yakamkuta yaliyomkuta, tumwombee kwa Mwenyezi Mungu apate uponyaji wa haraka.

Nipende kuwashukuru wana JamiiForums wote kwa mijadala iliyoendelea wakati wote ambao sikuwepo, vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vilivyoshiriki katika hatua hii ya awali (kazi ndiyo imeanza).

Watumiaji wa mtandao wa Twitter (bila kutaja mmoja mmoja) kwa jitihada zao ambazo zimenishangaza kuhakikisha ‘hashtag’ ya ‘ HYPERLINK “http://www.jamiiforums.com/tags/?t=FreeMaxenceMelo” #FreeMaxenceMelo ina-trend’ na kuwa tayari kwao kutoa maoni yao kwa vyombo vya habari pale walipohitajika kufanya hivyo.

Nawashukuru wahisani mbalimbali na wadau wa maendeleo ambao walituma wawakilishi wao Kituo cha Polisi cha Kati na Gerezani kufuatilia napitia maisha gani na hata kuwasiliana na mamlaka zinazohusika kutaka nitendewe haki.

Aidha, nawashukuru sana wafanyakazi wa Jamii Media ambao naelewa kwa kiwango gani kilichotokea kilivyowaathiri kisaikolojia na hata kiutendaji.

Nawashukuru Asasi za Kiraia zikiongozwa na THRDC, LHRC, Sikika, C-Sema, TMF na wengine wengi kwa kuwa mstari wa mbele kufuatilia na kuelewa kinachoendelea na hata kujitoa kwa ajili ya udhamini wangu pale walipoombwa na wengine hata bila kuombwa. Jukwaa la Wahariri (TEF) ahsanteni sana!

Nichukue fursa hii kuwashukuru pia Watanzania katika makundi mbalimbali ya WhatsApp, Facebook na Telegram kwa ushirikiano waliouonesha.

Watumiaji wa Instagram (nashindwa kutaja mmoja mmoja), nawashukuruni sana kwani nimeona ‘posts’ nyingi toka kwa watu hata ambao hawanifahamu lakini walioelewa ninachosimamia wakitoa ‘support’ kubwa sana.

Ndugu, marafiki na majirani zangu, ahsanteni sana kwani mlikuwa nasi bega kwa bega wakati wote.

Watanzania na wote ambao si Watanzania mliojitahidi kufika Central na Gerezani kunijulia hali, ahsanteni sana na Mungu awabariki sana!

Kuna wale ambao hata hawajaelewa kesi inahusu nini hasa na wameanza kuwashambulia waliokuwa wakinitetea, nao nawashukuru kwani naamini ni kwa kuwa hawajajua nini kimo kwenye kesi.

Ila niwahakikishie kuwa si rahisi kutetea mhaini, unapoona mtu anaamua kufanya hivi ni vyema kutafakari.

Askari wa Kituo cha Kati (Central) na wale wa Gereza la Keko, ahsanteni sana. Naelewa ni vigumu umma wa Watanzania kuelewa namaanisha nini lakini ninyi kwa andishi hili mnaelewa vema ninachomaanisha.

Wengi mliifanya kazi yenu kwa weledi mkubwa.

Viongozi wa kidini (wachungaji, masheikh, maaskofu na wengine) na wanasiasa wote (toka vyama vya upinzani na chama tawala) mlioshiriki katika hili, ahsanteni sana.

Hamkuingiza itikadi za kisiasa wala misimamo ya kidini bali mlitaka haki kutendeka. Nawashukuru!

Kuhusu kesi yangu ndiyo kwanza kesi inaanza kuunguruma Desemba 29, mwaka huu.

Si rahisi mimi kuongelea nini kilichomo kwenye kesi lakini naamini vyombo vingine vya habari kwa kuwa tunayo sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, vinajua namna ya kuhakikisha vinaueleza umma nini kilichomo ndani yake ili Watanzania waweze kuelewa mbivu na mbichi.

Kuna ambao watajikuta kuwa walikuwa ndio walengwa hata hawakuguswa na kukamatwa kwangu, hapo ndipo watajua tunapigania nini.

Nipende kuwaomba tuendelee kuwa pamoja katika safari hii tunayoianza. Mimi ni sampuli tu, nasimama kwa ajili ya wale ambao naamini wana haki ya kutoa maoni na kufichua maovu (ili mradi hawajavunja sheria) na ninaamini wengi tunataka haki hii isipotee na iendelee kulindwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri wa Muungano.

Mwandishi wa makala haya ni Mkurugenzi wa Jamii Forums.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles