24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Shilingi Bilioni 75 kuimarisha upatikanaji umeme Simiyu

Na Mwanadishi Wetu, Simiyu

Waziri wa Nishati, January Makamba, ameeleza kuwa changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika mkoani Simiyu imefanyiwa kazi na Serikali na sasa mkoa huo umepelekewa mradi wa Sh bilioni 75 ambao unahusisha ujenzi  kituo cha kupoza umeme pamoja na miundombinu ya kusafirisha umeme wa KV 220 ambao utatekelezwa kwa miezi 18.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ikungulyabashashi iliyopo wilayani Bariadi ambayo imeunganishwa na umeme kupitia mradi wa REA III Awamu ya Pili wakifurahi na Waziri wa Nishati, January Makamba baada ya kuona manufaa ya umeme unaowawezesha kuweka makambi ya kujisomea, kutumia vifaa vya tehama na kuwasaidia kwenye majaribio ya kisayansi.

Waziri Makamba ameyasema hayo Julai 13, 2022 wakati alipokagua eneo kutakapojengwa kituo hicho cha kupoza umeme katika eneo la Imalilo wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.

“Wizara na TANESCO tumeamua kujenga miundombinu ya usafirishaji umeme kutoka Ibadakuli Shinyanga hadi Simiyu pamoja na kujenga kituo cha kupoza umeme kwa sababu kuna changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika.

“Simiyu ni Mkoa wa mkubwa wa uzalishaji, kuna viwanda vya pamba na migodi na uwekezaji mwingine unatarajiwa kufanyika lakini hakuna umeme wa uhakika hivyo mradi huu ukikamilika utatatua changamoto hii,” amesema Makamba.

Ameeleza kuwa, mkandarasi wa mradi huo atapatikana ndani ya mwezi mmoja ambapo fedha za utekelezaji wa mradi huo zitatoka katika mradi ujulikanao kama Gridi Imara wenye Sh bilioni 500 ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kuongeza uwezo na uhakika wa upatikanaji umeme katika maeneo ambayo yana mahitaji ya umeme lakini hakuna umeme wa uhakika.

Kuhusu umeme vijijini alisema kuwa, mkoa huo wenye vijiji 470, tayari vijiji 269 vimeshasambaziwa umeme na vijiji 201 vilivyosalia tayari kuna wakandarasi wawili wanaoendelea na kazi ya usambazaji umeme.

Katika kuboresha usimamizi wa miradi ya umeme vijijini, Waziri Makamba alisema kuwa, ndani ya mwezi mmoja Serikali itaajiri vijana takriban 139 watakaosambazwa katika Halmashauri zote nchini ili wawe waratibu wa miradi ya REA katika maeneo hayo.

“Vijana hawa 139 kazi yao ni kufuatilia miradi imefikia hatua gani, mfano kama vifaa vya umeme vimefika katika maeneo yao, kama nguzo zimechimbiwa mashimo, kama zimesimamishwa na kama nyaya zimevutwa, vijana hawa watakuwa pia kiungo cha mawasiliano kati ya Wizara, Tanesco, viongozi wa Serikali na kisiasa pamoja na wadau wengine wanaohusika na miradi hii,” amesema Makamba.

Kuhusu upatikanaji wa nishati bora ya kupikia vijijini,  amesema kuwa, Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 10.5 ili kutekeleza mradi huo na kufanya kampeni kubwa ya kuhamasisha matumizi ya nishati bora ya kupikia pamoja na tafiti za kubaini nishati na mfumo sahihi wa kusambaza nishati hiyo maeneo ya vijijini ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Pamoja na kukagua miradi ya umeme, akiwa mkoani Simiyu, Waziri wa Nishati alitoa elimu kwa wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia pamoja na kugawa kugawa mitungi ya gesi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na wanachi katika Kijiji cha Momela wilayani Itilima mkoani Simiyu ambapo aliwaeleza kuhusu kazi zinazoendelea za usambazaji umeme vijijini pamoja na mpango wa Serikali wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia vijijini.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles