21.1 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Shahidi aeleza Mbowe alivyotimua mbio risasi zikirindima

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

  • Ni katika tukio ambalo mwanafunzi Akwilina aliuawa kwa risasi

MRAKIBU Mwandamizi wa Polisi, Gerald Ruichi amedai aliruhusu mabomu ya moshi na risasi za moto zitumike kutawanya maandamano ya viongozi wa Chadema na wafuasi wao waliokuwa wakielekea kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, huku Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akikimbia hadi kudondosha miwani.

Alidai baada ya kuamuru kutumika silaha za moto watu walikimbia, na hakuamini Mbowe anakimbia kiasi hicho kwani alitimua mbio hadi akaangusha miwani.

Ruichi alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbowe na wenzake wanane.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, shahidi huyo alidai Februari 16 mwaka jana, Chadema walikuwa wanafunga kampeni ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni uliofanyika Februari 17 mwaka jana.

Ruichi alidai kuwa mikutano ya Chadema, CCM na CUF ilisimamiwa na maofisa wa polisi wenye dhamana kuanzia Mrakibu wa Polisi.

Alidai kuwa mkutano wa Chadema ulisimamiwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Dotto.

“Chadema wakiwa katika kampeni walihamasishana kuandamana kuelekea kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na walipozuiliwa kufanya hivyo walikaidi.

“Waandamanaji walijaa katika barabara zote, nilitoa ilani watawanyike kwamba mkusanyiko huo sio halali, waandamanaji wakiongozwa na viongozi hawakutawanyika, nikaamuru mabomu ya machozi yatumike.

“Askari walirusha mabomu ya machozi lakini utekelezaji haukufanikiwa kwa sababu badala ya moshi kuelekea kwa waandamanaji ulirudi kwa askari, waandamanaji walikuwa wanarusha chupa za maji huku wakizomea askari.

“Ilani ya pili ya kurusha mabomu ya moshi iliposhindikana na askari wawili walikuwa wameshajeruhiwa, nikaruhusu matumizi ya silaha za moto kuwatawanya.

“Niliamuru kikosi cha mabomu kirudi nyuma, kikosi cha silaha za moto kisonge mbele, risasi zilipigwa watu walikimbia, sikuamini kama Mbowe anaweza kukimbia kiasi kile, alikimbia mpaka akaangusha miwani, waandamanaji walitawanyika,” alidai shahidi.

Aliwataja waliojeruhiwa katika maandamano hayo ni PC Fikiri, Koplo Rahim huku Akwilina Akwiline aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji Dar es Salaam (NIT) akifariki dunia.

Shahidi alitakiwa kwenda katika kizimba kuwataja mshtakiwa mmoja mmoja kwa kuwagusa katika mabega, na alifanikiwa kumtaja na kumgusa Mbowe, Msigwa, Salum Mwalimu na Halima Mdee.

Wengine alishindwa kuwataja majina yao na kuwagusa, lakini alidai wote walikuwepo kwenye maandamano.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi, kula njama, kufanya maandamano isivyo halali, kuhamasisha chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali tukio lililofanyika Februari 16 mwaka jana katika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni.

Pia washtakiwa wanadaiwa katika tarehe hiyo, barabara ya Kawawa, eneo la Mkwajuni wakiwa na wengine 12 ambao hawapo mahakamani, walikaidi agizo la SSP Gerald Thomas lililowakataza kufanya maandamano.

Washtakiwa wanadaiwa kwa kuandamana walisababisha kifo cha Akwiline na askari wengine wawili kujeruhiwa. Washtakiwa walikana mashtaka.

Mbali Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Katibu Mkuu, Dk. Vicent Mashinji na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles