25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Sh bil. 33 kuimarisha bandari Kigoma

Na ESTHER MBUSSI

-KIGOMA

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imeanza mradi wa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika bandari ndogo mbili zilizopo mkoani Kigoma.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa gati katika Bandari ya Kibirizi na Ujiji, na Ofisi ya Mkuu wa Bandari. Tayari mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi na ameshaanza kazi.

Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema mradi huo unafanywa na Kampuni ya China Railway 15 Group Corporation.

Msese alisema kazi ilianza Februari 28, mwaka huu na imetekelezwa kwa asilimia tano.

Alisema pamoja na mambo mengine, wanatarajia kujenga gati ya vyombo vidogo yenye urefu wa mita 120 na maghala makubwa matatu.

“Mradi wa Kibirizi ni sehemu mojawapo ya mradi ambao una sehemu tatu, mradi wa Bandari ya Kibirizi, Ujiji na mradi wa Ofisi ya Meneja wa Bandari.

“Gati hili litakuwa na urefu wa mita 250. Mradi huu kwa ujumla katika sehemu zote tatu unagharimu Sh bilioni 33,” alisema.

Alisema Ofisi ya Meneja wa Bandari itakuwa jengo la ghorofa moja, lakini sehemu kubwa ya mradi iko katika eneo hili la Kibirizi.

Msese alisema kuna changamoto ya watu kuingia bandarini hapo kiholela, hivyo katika mradi huo kutakuwa na uzio wa kuzunguka eneo lote la bandari na kuruhusu kuingia watu wanaokwenda kwa shughuli za bandari, wafanyabiashara na abiria.

“Zamani watu walikuwa wakipanda na kushuka huku wanakanyaga maji, lakini kwa sasa hivi tumeweka haya maboya ambayo yanaruhusu watu kwenda katika maeneo yao,” alisema.

mwisho

Mhasibu Wizara ya Afya ashikiliwa Takukuru kwa kudanganya mwajiri

Na UPENDO MOSHA

-MOSHI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, inamshikilia Mhasibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Yahya Mbegu, kwa tuhuma za kumdanganya mwajiri wake na kufanya ubadhirifu wa fedha za umma zaidi ya Sh milioni 34.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari mjini hapa juzi, Kamanda wa Takukuru mkoani Kilimanjaro, Holle Makungu, alisema wanamshikilia mhasibu huyo kutokana na kufanya makosa hayo kinyume na kifungu cha 22 na 28 vya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

“Tunamshikilia mhasibu huyo kwa kosa la kutumia nyaraka za kumdanganya mwajiri wake na kufanya ubadhirifu wa fedha za umma kiasi cha Sh 34,230,000,” alidai.

Makungu alisema uchunguzi wa Takukuru unaonesha kuwa mwaka 2014 wizara iliendesha chanjo ya rubella katika halmashauri mbalimbali, ikiwemo Moshi Vijijini na  wahasibu kutoka wizara hiyo walipewa jukumu la kusimamia fedha hizo.

Alidai kuwa Mbegu alipewa jukumu na wizara hiyo kusimamia matumizi ya Sh milioni 491.8 kwa Mkoa wa Kilimanjaro, fedha ambazo ziliwekwa katika akaunti ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

“Fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti na zilikuwa na maelekezo na kukabidhiwa Yahya ili asimamie matumizi katika halmashauri za Manispaa ya Moshi, Moshi vijijini, Siha, Hai, Rombo, Mwanga na Same,” alidai.

Alidai kuwa katika mgawanyo, halmashauri ya Moshi Vijijini ilikuwa ni Sh milioni 99 na kwamba uchunguzi umebaini kuwa Mbegu aliandaa na kuwasilisha nyaraka za udanganyifu kwa mwajiri wake  ambazo zilisababisha ubadhirifu wa fedha hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles