22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wastaafu 10,000 wa PSSSF hawajulikani walipo

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM 

WASTAAFU 10,500 kati ya 124,500 wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), hawajulikani walipo baada ya kutojitokeza kuhakikiwa tangu uhakiki wa wastaafu wa mfuko huo uanze Desemba mwaka jana.

Kabla kulikuwa na mifuko ya LAPF, GEPF, PPF na PSPF ambayo iliunganishwa na kuundwa mfuko wa PSSSF unaoshughulikia watumishi wa umma na NSSF unaoshughulikia sekta binafsi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Uhusiano wa PSSSF, Eunice Chiume, alisema wanafanya uhakiki wa wastaafu na wategemezi wao Tanzania Bara na Visiwani ili kutambua uhalali wao.

Eunice alikuwa akizungumza baada ya kutembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd kwa lengo la kutambulisha mfuko huo na shughuli zilizofanyika tangu ulipoanza hadi sasa.

“Tunahakiki wastaafu na wategemezi wao kwa sababu katikati ya mwaka mstaafu anaweza kufariki hivyo inawezekana ukaendelea kulipa mtu kumbe ameshafariki.

“Kuna changamoto ya watu kupuuzia ama kusahau, sasa pensheni ikisimamishwa ndio wanalalamika kwamba hawalipwi na tumewaambia kama mstaafu ni mgonjwa watueleze tutamfuata,” alisema Eunice.

Alisema awali uhakiki huo ulipangwa kumalizika Machi mwaka huu lakini wameongeza muda na kuwataka wastaafu wote ambao bado hawajahakikiwa wajitokeze katika ofisi za mfuko huo ili kuepuka kusimamishiwa pensheni zao.

MALIPO YA WASTAAFU

Alisema tangu mfuko huo ulipoanza shughuli zake Agosti Mosi mwaka jana, hadi sasa umelipa Sh trilioni 1.1 kwa wastaafu. 

Kwa mujibu wa Eunice, kati ya fedha hizo Sh bilioni 880 zililipwa Septemba mwaka jana kwa wastaafu waliorithiwa kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF na Sh bilioni 300 zililipwa Machi, mwaka huu.

Alisema pia wastaafu waliokuwa wamelipwa kwa kutumia kikokotoo kipya cha asilimia 25 wamelipwa mapunjo yao baada ya Serikali kurudisha kikokotoo cha zamani cha asilimia 50.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya Rais Dk. John Magufuli kukutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, wakuu wa mifuko ya PSSSF, NSSF, SSRA na waziri wa kazi na baada ya majadiliano alitangaza kufuta kikokotoo kipya na kuagiza kila mfuko kutumia kikokotoo cha zamani.

“Waliokuwa wameshalipwa kwa kikokotoo cha asilimia 25 tulibaini kulikuwa na mapungufu ya Sh bilioni 119 hivyo, baada ya kurejea kikokotoo cha zamani walilipwa mapunjo yao,” alisema.

Alisema pia wamefungua ofisi katika mikoa 29 na kwamba wana ofisi Zanzibar ambako kuna wastaafu 7,924.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles