27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Bil 82/- zatengwa uchaguzi Serikali za Mitaa

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

SHILINGI bilioni 82.9 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Oktoba.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana jijini hapa na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara wakati akijibu maswali mawili yaliyoulizwa na Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF), aliyetaka kujua kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo na kauli ya Serikali

kuelekea uchaguzi huo kutokana na yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita ambako wagombea wa upinzani walizuiwa kugombea kwa madai ya kutokuwa na sifa.

Akijibu maswali hayo, Waitara ambaye pia alivitoa hofu vyama vya upinzani kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na haki, alisema tayari Serikali imekamilisha maandalizi ya kanuni zitakazotumika kuendesha uchaguzi huo na kutangaza katika gazeti la Serikali, Aprili 26, 2019.

“Lipo tangazo namba 371 linalohusu kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo, tangazo namba 374 linalohusu kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji,” alisema.

Aidha Waitara aliyataja maandalizi mengine yaliyokwishafanywa na Serikali kuwa ni pamoja na kuhakiki maeneo ya utawala na kufanya mafunzo na mikutano kwa wadau wa uchaguzi huo. 

Alisema kwa sasa Serikali inaendelea na maandalizi ya ununuzi wa vifaa vya uchaguzi.

Awali akiuliza swali lake, mbunge huyo alitolea mfano mkoani Morogoro ambako alisema CCM wameanza kampeni ya Kijani na kufananisha jambo hilo na kuanza kampeni mapema.

Akijibu swali hilo, Waitara aliyepata kuwa mbunge kupitia chama cha upinzani cha Chadema kabla ya kuhamia CCM kwa hoja ya kuunga mkono juhudi za Serikali alisema; “nadhani wapinzani mna hofu kwa kuwa mnajua CCM ipo katika nafasi nzuri ya kushinda kutokana na mambo mazuri yanayofanywa na Rais John Magufuli… uchaguzi utakuwa huru na haki na majina ya wapigakura yatabandikwa vituoni.”

Akizungumzia kampeni ya Kijani ya Morogoro, Waitara alisema huo ni mkakati wa CCM kupata taarifa za wanachama wake kama ambavyo Chadema wanafanya mikutano yao ya Chadema ni Msingi kwa ajili ya kukutana na wanachama wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles