24.8 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa rai kwa wakulima nchini kuweka akiba ya chakula

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli ametoa rai kwa wakulima nchini kuendelea kuweka akiba ya mazao ya chakula kwa ajili ya kukidhi familia zao pamoja na Serikali kufungua wigo kwa wakulima kufanya kilimo biashara kwa kuuza mazao yao nje ya nchi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Riziki Shemdoe.

Mweli ametoa rai hiyo leo Agosti 30, jijini Dar es Salaam katika Mdahalo wa kujadili fursa na changamoto zitokanazo na mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) ulioshirikisha Wahariri na Waandishi wa Habari na Taasisi za Fedha kwa kushirikiana na Kampuni ya Habari Media Brains (MB).

Amesema wizara imeamua kufanya kilimo kuwa biashara ili kumsaidia mkulima kuweza kuwa huru katika biashara zake na kujikwamua kiuchumi.

“Tumefanya kilimo kuwa biashara kwa kufungua mipaka ili kila mfanyabiashara awe huru kuuza mazao yake lakini kabla hujauza ahakikishe ameweka chakula cha kutosha kwa ajili ya familia,” amesema Mweli.

Akielezea mpango wa Jenga kesho iliyobora (BBT) amesema uwepo wa BBT ni kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana ambapo Serikali imeanza kutumia vijana na wanawake kwenye mpango huo.

Amesema katika mpango wa BBT vijana na wanawake wanapatiwa ardhi kwa ajili ya kulima mbegu bora na kuwatafutia masoko.

“Tumefanya tathimini ya kutosha ili kupunguza changamoto ya ajira na vijana na wengi kutojihusisha na kilimo ndipo tulipojua changamoto na serikali kuanza kulifanyia kazi ndipo ilipokuja swala la BBT kilimo,” ameeleza Mweli.

Amesema changamoto walizokuwa nazo vijana ndio imekuwa fursa kwenye mpango wa BBT-KILIMO kwa kutoa mitaji kwa vijana, masoko na kuboresha Teknolojia.

Ameongeza kuwa wakulima wadogo ndio kichocheo cha uwepo wa chakula cha kutosha nchini.

Amesema katika mpango wa BBT haujaacha wakulima wadogo ambao tayari walishaingia kwenye kilimo wanaendelea kuwajengea uwezo na kuboresha miundombinu ili kuweza kulima kitaalam na kuweza kulima kibiashara.

Akizungumzia Mweli kuhusu fursa zitakazopatikana kutokana na mkutano wa AGRF kwa wakulima wadogo amesema mkutano huo utakutanisha wadau mbalimbali wa kilimo hivyo wataweza kuongeza thamani ya mazao yao lakini pia kujitangaza kimataifa na kupata masoko ya nje

Amesema utayari wa nchi kulisha Dunia unachochewa zaidi na wakulima wadogo ambapo Serikali inaendelea kuwaboreshea miundombinu ikiwemo kuendelea kuwajengea mabwawa makubwa ya maji kwa ajili ya kufanya kilimo cha umwagiliaji lakini pia kutoa mbolea za ruzuku kwa kila zao.

Aidha, amesema uwepo wa mkutano wa AGRF nchini umechagizwa na sababu mbalimbali ikiwemo utayari wa nchi kulisha dunia lakini pia kupanda kwa bajeti ya izara ya kilimo kutoka Bilioni 298 hadi bilion 979 kwani imepelekea ufanisi mkubwa katika sekta ya kilimo.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Riziki Shemdoe amesema mkutano huo ni mara ya kwanza kufanyika nchini mwaka jana ulifanyika nchini Rwanda, fursa za uwekezaji zilizopo ni vema kuwekeza nguvu kwenye mkutano huo.

Kwa upande wao wadau wa taasisi za fedha mbalimbali ikiwemo Benki ya CRDB, NMB, NBC na EQUITY BANK wamesema kuwa wataendelea kusapoti wakulima ili kuboresha sekta ya kilimo ili nchi kuendelea kuwa na chakula cha kutosha na kufikia lengo la kulisha dunia.

Mkutano mkubwa wa mifumo ya chakula Afrika AGRF unatarajiwa kufanyika Septemba 5, hadi 8, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam huku washiriki zaidi ya 3,300 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kushiriki kwenye mkutano huo ambao utatoa fursa nyingi kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo lakini pia kwa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles