21 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Serikali yatangaza kiama kwa madalali

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na  Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Na HERIETY FAUSTINE, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na  Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametishia kuwafutia usajili baadhi ya madalali wa ardhi na nyumba, kutokana na utendaji wao unaokiuka sheria wakati wa uuzwaji wa nyumba.

Kwa mujibu wa Lukuvi, nyumba nyingi zimekuwa zikiuzwa bila kufanyiwa tathmini ya gharama zake halisi na hata zilizofanyiwa wahusika wamekuwa hawashirikishwi.

Lukuvi alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokutana na madalali wa kampuni mbalimbali, ambapo aliwaeleza malalamiko anayoyapata kutoka kwa wananchi ambao nyumba zao ziliuzwa kwa utaratibu usioeleweka.

“Madalali mmekuwa mkiuza nyumba bila kujali thamani ya mali husika na wengine mnauza kwa bei ya chini, wengine mnauza kwa bei ya deni lile lile, huo ni uonevu wa hali ya juu huku mkitambua mnaowafanyia ni maskini,”alisema.

Alisema asilimia kubwa wanaokumbwa na uonevu huo ni wanawake wajane kutokana na kutojua kama mali walizoachiwa na waume zao kama ziliandikishwa katika mkopo wa benki.

Waziri Lukuvi aliongeza kuwa madalali wengi wamekuwa wakikiuka sheria za uuzaji wa nyumba pamoja na mali za masikini kwa bei ya chini, huku wengine wakifanya mnada katika siku za mwisho wa wiki.

“Madalali wengi wamekuwa wakiuza mali za watu kwa kisingizio cha amri ya mahakama tena kwa bei ya asilimia 25 badala ya 75 kama sheria inavyotaka huku mkijua kufanya hivyo ni uonevu na wizi.

“Ninazo taarifa zenu na hata majina yenu nayajua, nitawafutia usajili na majina yenu kutangazwa katika gazeti la Serikali,”alisema.

Waziri Lukuvi alisema madalali wengi wamekuwa wakifanya mnada wa kuuza mali wakati tayari wakiwa wameshapata wanunuzi na wengine wakiwa wameshatoa fedha za awali.

Alisema amepata malalamiko ya watu 84 kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao wameonewa kwa namna moja au nyingine na madalali wanaoshirikiana na baadhi ya maofisa wa benki kwa kuwauzia au kuwabomolea nyumba zao kinyume cha utaratibu.

Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi aliwataka madalali hao kupeleka taarifa zote za mali husika kabla ya kupigwa mnada kwa msajili wa ardhi na nyumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,504FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles