27.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatangaza ajira mpya sekta ya afya

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

Serikali imetangaza ajira mpya 171 za kada mbalimbali katika sekta ya afya ili kujaza nafasi za waliochaguliwa awali ambao wameshindwa kuripoti kwa wakati katika zahanati na vituo vya afya walivyopangiwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jijini hapa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, jumla ya waombaji 513 kati ya 6,180 waliopangiwa awali walishindwa kuripoti kwa wakati katika vituo vyao vya kazi. Ni 5,667 tu ndio walioripoti.

Jafo alisema tayari Serikali imewaajiri watumishi wapya 342 kati ya 513 wa kada mbalimbali za afya kujaza nafasi hizo.

Jafo alisema watumishi hao wamekidhi vigezo vya kuajiriwa katika vituo vya afya na zahanati zilizopo katika mamlaka za Serikali za mitaa.

“Idadi hii ya watumishi wapya imepatikana kutokana na kushindwa kuripoti kazini kwa wakati kwa waombaji 513 kati ya waombaji 6,180 waliopangiwa awali na badala yake ni watumishi 5,667 tu ndio waliripoti, sasa tumechambua katika maombi ya awali tumewapata 342 kujaza nafasi hizo na tumetangaza ajira mpya 171 ili kufikia idadi ya ambao hawakuripoti,” alisema Jafo.

Alisema nafasi hizo mpya zinapaswa kuombwa kuanzia Oktoba 5, mwaka huu hadi Oktoba 12.

Alizitaja kada ambazo hazijapata watu wenye sifa kuwa ni daktari daraja la II, tabibu daraja II, tabibu msaidizi, ofisa muuguzi msaidizi daraja II na ofisa muuguzi daraja II.

Alizitaja kada nyingine kuwa ni pamoja na nafasi ya mteknolojia mionzi daraja la II, fundi sanifu vifaa tiba daraja la II, mfamasia daraja II na mtoa tiba kwa vitendo II.

“Hao waombaji wawe tayari kufanya kazi katika halmashauri yoyote watakayopangiwa, maombi yote yatumwe kwa njia ya mtandao (online) kupitia mfumo wa elektroniki unaopatikana kwenye tovuti ya Tamisemi na mwisho itakuwa ni saa 9:30 alasiri Oktoba 12, mwaka huu. Maombi yatakayotumwa nje ya mfumo hayatashughulikiwa,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles