23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Serikali yasaini mkataba wa Sh bilioni 175

Mwandishi wetu -Dodoma

SERIKALI ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimetiliana saini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Euro milioni 70, sawa na takriban Sh bilioni 175.6 kugharamia mradi wa Mamlaka wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Morogoro (Moruwasa).

Mkataba wa mkopo huo umesainiwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James kwa upande wa Serikali na Mkurugenzi Mkazi wa AFD, Stephanie Essombe.

James alisema mkopo huo utawezesha wakazi wa mjini Morogoro wapatao 722,010 kupata maji safi na salama kupitia upanuzi wa mfumo wa usambazaji wa maji kutoka Bwawa la Mindu.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha upatikanaji wa maji kutoka mita za ujazo 33,000 hadi kufikia 108,000 kwa siku pamoja na kuwezesha mji wa Morogoro kupata kiwango cha mahitaji ya maji safi kinachokadiriwa kuwa mita za ujazo 126,253 kwa siku, ifikapo mwaka 2035.

“Mradi pia utaongeza upatikanaji wa huduma za majitaka kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5 hadi asilimia 15 kwa wakazi wa mjini Morogoro,” alifafanua James.

Alisema Tanzania imekuwa ikinufaika na ufadhili wa AFD hususan katika sekta za nishati, maji, usafirishaji na kilimo kupitia idadi ya miradi  mbalimbali inayoendelea na ile inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

James alisema miradi saba inayoendelea kutekelezwa katika sekta mbalimbali hapa nchini kupitia misaada na mikopo inayotolewa wa Shirika hilo inafikia takriban Euro milioni 154.5 sawa na Sh bilioni 387.6.

“Miradi sita yenye thamani ya Euro milioni 141.4 kupitia ufadhili wa AFD imekamilika na kuna miradi mingine 12 yenye thamani ya Euro milioni 1,021.7 ambayo tuko kwenye mazungumzo na AFD katika sekta ya nishati, maji, kilimo usafiri wa mwendokasi jijini Dar es Salaam, miundombinu ya viwanja vya ndege na usafi wa mazingira jijini Dar es Salaam,” alisema James.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa AFD, Essombe aliahidi shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafikia malengo yake katika kuboresha maisha ya wananchi hasa katika upatikanaji wa maji.

“Ushirikiano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ulioanza miaka 20 iliyopita umezidi kuimarika ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita shirika limewekeza kiasi cha Euro milioni 258 sawa na takriban Sh bilioni 655 za Tanzania,” alisema Essombe.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo alisema mkopo huo utatatua changamoto ya maji ambayo ilikuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Morogoro.

Alisema mkopo huu una faida nyingi nchini ikiwemo kutoa ajira pamoja na kutoa fursa kwa viwanda vya ndani kwa sababu vifaa vitakavyotumika kutekeleza mradi huo wa kihistoria vitanunuliwa ndani ya nchi.

Kitila alisema hivi sasa Serikali inatekeleza miradi ya maji 1,423, miradi 792 imekamilika na miradi 631 inaendelea na kwamba mradi huo wa maji wa Mji wa Morogoro utakuwa mkombozi mkubwa wa wananchi wa mji huo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles