23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI KUWEKA SERA KULINDA VIWANDA VYA CHUMA

JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM

ONGEZEKO kubwa la uzalishaji wa bidhaa za chuma katika soko la dunia, limetajwa kuwa moja ya changamoto zinazovikabili viwanda vya chuma vinavyochipukia hapa nchini kutofanya vizuri.

Hayo yanabainishwa na Mshauri wa Maendeleo ya Viwanda  kutoka Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani (JICA), Hiroshi Kumagai, katika mkutano wa wadau wa uzalishaji wa chuma na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

“Uzalishaji wa chuma duniani umekuwa wa hali ya juu sana kuliko matumizi, hivyo nchi nyingi kukimbilia kuuza bidhaa zake nchini ambazo kwa kiasi kikubwa hazina ubora wa kutosha.

“Serikali inatakiwa kudhibiti uingizwaji holela wa bidhaa za chuma nchini ili kulinda soko la ndani kwani bidhaa zinazoingia nyingi hazina ubora wa kutosha, hivyo kuuzwa kwa bei ya chini na kuathiri ustawi wa viwanda vya ndani,” alisema Kumagai.

Alisema uwezo wa dunia katika uzalishaji wa chuma kwa mwaka jana ulikuwa unakadiriwa kuwa ni tani milioni 2,400 ambapo mahitaji yalikuwa ni tani milioni 1,500, hivyo ziada iliyobaki ni zaidi ya tani milioni 900.

Kumagai alisema China pekee ina uwezo wa kutengeneza chuma tani milioni 1,150 katika 2015 na kuongoza uzalishaji duniani kwani ni karibu nusu ya uwezo wa jumla wa dunia wakati mahitaji ya kimataifa yakipungua na ukuaji wa uchumi ni wa polepole.

Alisema Serikali za nchi zenye uzalishaji mkubwa zimekuwa zikiwawezesha wawekezaji kuwatafutia masoko nje ya nchi ambapo imefikia hatua ya kuifanya Tanzania kuwa jalala la bidhaa za chuma zisizokuwa na ubora.

“Uzalishaji wa chuma ni mkubwa kuliko matumizi ambapo nchi nyingi zinaingiza bidhaa zake nchini tena kwa bei ya chini, baada ya kupata usaidizi kutoka Serikali zao, jambo ambalo limekuwa linaathiri viwanda vya ndani,” alisema Kumagai.

Kumagai aliongeza kuwa kunatakiwa kuwapo kwa sera thabiti ya uingizaji wa bidhaa za chuma ili kuwalinda wazalishaji wa ndani katika ushindani wa soko la dunia, bila kuathiri ubora wa chuma yenyewe na masilahi ya watumiaji.

Alisema Tanzania ina amana kubwa ya chuma katika Mkoa wa Njombe ambako  hakuna kiwanda chochote cha kutumia makaa ya mawe.

“Kwa bahati mbaya, hadi sasa hiki ni chanzo kikubwa lakini hakihusishwi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kwa sasa kuna kampuni mbili tu zinapatikana na  matumizi yake ni tani 400,000 ya chuma kwa mwaka,” alisema Kumagai.

Alisema kampuni za Steel Africa Kenya iliyoko Koru eneo la Kisumu, inazalisha tani 300,000 kwa mwaka na Steel Rolling ya Jinja nchini  Uganda cha tani 100,000 ambapo kutokana na upatikanaji mdogo wa makaa ya mawe, hulazimika kutumia kati ya asilimia 30 hadi 40 ya uwezo wake.

“Steel Rolling ya Jinja hulazimika kuingiza makaa ya mawe kutoka Msumbiji hivyo kufanya bidhaa inayozalishwa kiwandani hapo kuwa ya bei ya juu sana wakati Prime Steel Africa Kenya huingiza makaa ya mawe kati ya tani 120,000 na 300,000.

“Kuhusu miradi ya makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma inayoendeshwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na China International Mineral Resource Limited (TCIMRL) haujanza kazi,” anaongeza.

Alisema lengo la mradi wa Liganga  ni kuwa na uwezo wa kuzalisha makaa ya mawe tani milioni moja na Mchuchuma ilikuwa ni kuzalisha umeme megawati 600.

“Nguvu ya umeme kuzalisha ingekuwa kubwa, hivyo kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji kwa ajili ya uzalishaji chuma tani milioni moja kwa mwaka na ziada ya umeme mradi wa Liganga ungeunganishwa katika gridi ya Taifa kwa mkataba na Tanesco,” alisema Kumagai.

Alisema mgawanyo wa viwanda si mzuri ambapo vingi kuwa Dar es Salaam takribani 18, Arusha 3, Mwanza 3, Morogoro 2 na Tanga 1 lakini Njombe ambako kuna rasirimali ya chuma na makaa hakuna hata kiwanda kimoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Maganga Matitu Resource, Lawrence Manyama, anabainisha changamoto zinazokabili uzalishaji wa chuma nchini kuwa ni pamoja na upungufu wa wataalamu wazawa katika viwanda vya ndani.

Alisema kutokana na upatikanaji duni wa wataalamu (wahandisi na mafundi) wenye uzoefu kwa ajili ya matengenezo na uendeshaji wa viwanda vya kisasa vya chuma, imekuwa ikisababisha utegemezi kwa nchi za India na China.

“Ukosefu wa wataalamu umekuwa changamoto kubwa kwa Serikali, hivyo inapaswa kuangalia upya mifumo ya vyuo vya ufundi ambavyo vimegeukia kuzalisha wahandisi badala ya kuhakikisha vinazalisha mafundi mitambo na mchundo wa kutosha.

“Kama kweli Serikali inalenga kufikia uchumi wa viwanda, utaratibu wa zamani wa vyuo vya ufundi kuzalisha mafundi mitambo na mchundo urudiwe tofauti na ilivyo sasa mbapo vimegeukia kuwa vyuo vikuu kutoa wahandisi. Hali hii ni sawa na kuzalisha madaktari bila kuwa na wauguzi,” alisema Manyama.

Alisema vipo vyuo kama vile VETA Dar es Salaam, DIT, Mbeya University of Technology (MUST) n.k  vilipaswa kuzalisha mafundi badala ya wahandisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles