26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

WENYE HOSTELI WALALAMIKIA VUNJA BEI YA MAGUFULI

Na Mwandishi Wetu,

SERIKALI inatakiwa ijichunguze katika utekelezaji wa mipango yake ambayo inaonekana  kuminya au kuvuruga masilahi ya uwekezaji kutoka sekta binafsi kabla mambo hayajaenda kombo kwao.

 Kinacholalamikiwa na wengi ni kuwa kumeongezeka kuwapo kwa vitendo  vya kushtukiza kwenye uchumi ambavyo huathiri mwenendo wa ustawi wa wafanyabiashara  katika sekta mbalimbali na hivyo kuzua  lawama, malalamiko na kufilisika kibiashara.

Nia ya  Serikali kwa maendeleo ni nzuri lakini utekelezaji wa miradi umekuwa katika mtindo wa unyang’anyi na kutokujali athari zake kwa wafanyabiashara kama vile wao si kitu katika uchumi.

“Ni makosa kufikiri  hivyo kwani wafanyabiashara ni injini ya kukua uchumi na wao ndio wenye uwezo wa kufanya mambo mengi na kwa wingi wao huleta tija katika uchumi husika,” anasema  Godfrey Simbeye, Mkurugenzi  Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Anasema hali imekuwa mbaya zaidi pale amabapo Serikali inatoa ushindani wa dhati kwa sekta hiyo kama vile haipo na hivyo kuashiria kukatika kwa mawasiliano kwa pande hizo mbili za uchumi yaani binafsi na sekta ya umma.

Mifano ni mingi lakini inatosha kusema ujenzi wa hosteli za UDSM, kazi za majengo ya Magomeni  na ujenzi wa Chuo cha Muhimbili Mloganzila kuchukuliwa na Tanzania Buildings Agency (TBA), kuzuia zabuni kupewa  watu binafsi kuendesha miradi TPA na ujenzi wa nyumba mbalimbali za wilaya nchini ni  mifano halisi.

Wafanyabiashara  wa  majengo  ya kukodisha  eneo la Savei karibu na UDSM wanalamika kwa kusema wanasema kuwa  hatua ya  Serikali ya kujenga mabweni mapya ya  Chuo Kikuu  Cha  Dares Salaam (UDSM)  na nafuu ya pango iliyotoa kwa  wanafunzi wa chuo kwa kupunguza  kiwango cha pango kimevuruga uwekezaji na mwenendo wake katika sekta hiyo.

Vunja bei aliyoitoa Rais Magufuli kwa wanafunzi wa UDSM imegeuka kuwa  mchunga kwa wamiliki wa nyumba za kupanga zilizo katika maeneo na taasisi hiyo kubwa ya elimu ya juu nchini.

Rais  John Magufuli  amezindua  matumizi ya mabweni yenye uwezo wa kuwalaza wanafunzi 3,840 kutekelezwa na  alienda mbali zaidi kwa kuamuru kupunguza kiwango cha pango kwa mwezi kwa kila mwanafunzi kutoka Sh 24,000 hadi Sh 15,000 na  kuvunja ushindani kutoka  mabweni ya watu binafsi  katika eneo linalozunguka chuo hicho.

Rais alizindua hosteli hizo wiki mbili zilizopita na ujenzi wake umechukua chini ya mwaka mmoja na kugharimu Sh  bilioni  10 na zilijengwa na TBA badala ya Sh bilioni 28 walizodai wajenzi binafsi.

“Choyo kwa kupata faida iliyopitiliza kutoka serikalini ndio ninachopinga na si kuwa adui wa wafanyabiashara ingawa inaonekana hivyo kwa watu wasio waaminifu,” alisema Rais Magufuli.

 “Tunajenga nchi na watu lazima waweke  uzalendo katika masuala haya ili nchi ipige hatua,” alisema.

Rais alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwekeza katika elimu hivyo itahakikisha wanafunzi nchini wananufaika kwa kupata elimu bora  kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu. Elimu ni pamoja na makazi bora kwa wanafunzi husika.

Kwa miaka mingi wamiliki wa nyumba za kupanga walikuwa  wakinufaika na  ukosefu wa makazi ya kutosha chuoni hapo na hivyo wanafunzi kuwa wateja wao wakubwa na kuwapangisha kwa kiwango kikubwa cha kodi  na masharti mengine yenye kero kwa  walipakodi kukiwa  na manyanyaso tele na kukosa utu wa kusubiri pale kodi ya pango inapochelewa kutolewa kwa wakati.

Kwa viwango vipya vinavyotakiwa kutozwa, kila mwanachuo atatakiwa kulipa sh 15,000 kwa mwezi na hivyo Sh 120,000 kwa miezi minane badala ya shilingi 200,000 zinazodaiwa na wapangishaji binafsi.

Kiwango  hicho ni kidogo ikilinganishwa na fedha ya kwenda na kurudi kutoka chuoni, ukijumlisha na nauli ya kila siku  na muda mwanafunzi anapoteza akisubiri mabasi kituoni  kwenda na kutoka chuoni.

Mambo si  kuntu kwa Mariam  Yohana anayesimamia hosteli zilizopo maeneo ya ‘Survey’ ambaye anaona mdororo wa ujaji wa wapangaji wake wanafunzi na kutishika kwa uhai wa biashara yake ya miaka mingi na kufichua kuwa kila mpangaji wake alikuwa anamlipa Sh  300,000 kwa miezi nane, ikiwa ni mara mbili ya kile watakacholipa kwa uongozi wa chuo kwa  mabadiliko haya ya kodi. 

John Massawe  ni mmiliki, naye anasema hosteli yao kila mwanafunzi analipa Sh 300,000 kwa muhula mmoja na katika chumba kimoja wanakaa wanafunzi wanne. Anasema hosteli yake ina vyumba kumi na tano na hivyo kipato chake kiko hatarini na anaogopa anaweza kushindwa kulipa mkopo wake wa ujenzi na kuweka samani.

 Lakini mmiliki mwingine mwenye hosteli iliyoko Sinza E, anayeitwa Godfrey Ulomi, anasema katika pango lake kila mwanafunzi analipa Sh 200,000 kwa miezi minane, hivyo  ana wasiwasi  wa kupata wateja  wa kutosha baada ya mabweni ya Chuo Kikuu kufunguliwa. Yeye ana wanafunzi 20 kati yao wanawake ni wanne.

Ni furaha tele kwa Said  Salum  ambaye amepata nafasi katika ‘mabweni ya Magufuli’ na kuondokana na adha ya kuishi maeneo ya Sinza ambapo mwenye nyumba alikuwa na manyanyaso.

 “Mimi hapa hulipa Sh 350,000 kwa mwaka yaani kila muhula nalipa Sh 175,000 ila sasa huyu baba mwenye nyumba ana mke mdogo ambaye ulimi wake ni mkali kama kisu kwa kutochagua  neno la kusema kama  atacheleweshewa kodi kwa madai kuwa maisha yake yanategemea kodi hiyo tu. Huwa hasikilizi mtu,” anasema Said. Anasema kunaokoa matumizi mengi kwa kuishi chuoni.

Manonga Josephat anadai  kuwa si  siri wanafunzi wengi walikuwa wanashinda na njaa kwa sababu fedha zote wanalazimika kumpa mwenye nyumba na hivyo kuwa kero kwa masomo yao.

Suala la Usafiri nalo linawaumiza zaidi kwani ulipaji wa nauli na chakula  ulikuwa unafanya  mikopo wanayoipata kutokidhi  haja  na ilibidi waishi kwa mbinu na mbinde, mwenendo usiolingana na hali ya kubobea kusoma.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles