24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI KUTOA MATREKTA KUINUA KILIMO BIASHARA

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


SERIKALI imeahidi kutoa pembejeo za kilimo cha kisasa yakiwemo matrekta kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kupitia Taasisi inayojihusisha na kuendeleza wanawake katika kilimo Tanzania (CAWAT) ili waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo cha kisasa hususani cha kibiashara.

Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha, kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati  akizungumza kwenye harambee ya kukusanya fedha  kwa ajili ya kuwezesha mradi wa kuwajengea uwezo wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara iliyoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Land O’  Lakes kwa kushirikiana na CAWAT na kufanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Serikali ipo tayari kutoa pembejeo hizo za kilimo cha kisasa yakiwemo matrekta bora kabisa ambayo yatatolewa kwa vikundi vya kinamama wanachama wa CAWAT ambao wataonyesha nia na uwezo wa kutekeleza kilimo cha kisasa hususani cha kibiashara.

“Zaidi wanufaika hao watahakikishiwa soko la uhakika kwa kile watakakichozalisha,” alisema Ole Nasha ambaye pia alitoa mchango wa Sh milioni mbili kwenye harambee hiyo.

Alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na taasisi yoyote nchini yenye nia ya dhati katika kuleta mabadiliko yenye tija yatakayoliwezesha Taifa kuongeza kasi yake katika kuelekea uchumi wa viwanda na mapinduzi ya kilimo.

Hatua hiyo ya Serikali inakwenda sambamba na ahadi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) kwa CAWAT ambapo kupitia Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wake, Francis Assenga, ilitangaza kwenye warsha hiyo kwamba ipo tayari kushirikiana na CAWAT ili kutoa ushauri utakaoambatana na fursa ya kutenga Sh milioni 600 kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake katika kuendesha kilimo hicho cha kibiashara kupitia taasisi hiyo.

“Kupitia ushirikiano wetu huo na CAWAT, ni wazi kwamba TADB tunakwenda kufanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya kilimo hasa cha kisasa kupitia wanawake nchini. Baada ya kupitia malengo ya CAWAT, tumeridhika moja kwa moja kuwa tuna kila sababu ya kushirikiana nao ili kuifikisha hii nchi kwenye uchumi wa viwanda kupitia kilimo,” alisema.

Katika harambee hiyo kiasi cha fedha cha zaidi ya Sh milioni 27 kilipatikana, huku  pia ikielezwa kuwa balozi za Japan na Switzerland hapa nchini zimeonyesha nia ya kusaidia miradi mbalimbali itakayoendeshwa na Taasisi hiyo ya CAWAT.

Awali wakizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya CAWAT, Dk. Victoria Kisyombe pamoja na Mkurugenzi Mradi kutoka Taasisi ya Land O’ Lake, Dk.  Rose Kingamkono, walisema kwa sasa Taasisi ya CAWAT ipo kwenye mchakato wa awali wa kuanza kujitegemea yenyewe kiuendashaji bila kutegemea msaada iliyokuwa ikiupata kutoka Shirika la Msaada la Marekani (USAID).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles