26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi

*Kiswahili kutumika mahakamani kuwasaidia wananchi

*Serikali kuja na huduma jumhishi

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imesema itaanza kutoa elimu ya Katiba na Sheria nchi nzima kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia ili kuongeza uelewa wa wanachi kuhusu haki na wajibu wao pia kuonyesha mambo mazuri na mabaya yanayopatikana ndani ya katiba hiyo.

Utekelezaji huo unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha 2022/23 ikiwa ni kati ya vipaumbele vinavyotarajiwa kutekelezwa na Serikali.

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam Jumatano Julai 20, 2022 na Waziri wa Katika na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha.

Amesema katiba iliyopo hivi sasa iliandikwa tangu mwaka 1977 nakwamba kwa sasa kuna mazingira tofauti yanayokinzana na katiba hiyo jambo ambalo amesema ni muhimu wananchi waelimishe kwanza ilikujua mambo hayo ni yapi.

“Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwapo na mitazamo mingi juu ya katiba yetu inayotumika hivi sasa, hivyo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2022/23 watalaam watafanya tathmini kwa kuwa katika mjadala wa katiba mpya unaoendelea kwa sasa wengi wanaoongea ni wanasiasa na kusahau kwamba wananchi nao wana nafasi yao ya kutoa maoni yao baada ya kuelewa mazuri na mabaya yaliyomo kwenye Katiba.

“Hivyo, kutokana na kuwepo na mapungufu kwenye katiba iliyopo ndio sababu serikali imetoa wigo mpana kwa Asasi za kiraia kujadili ili kuweza kuirekebisha na kupata katiba nzuri, tutatoa fursa kwa wananchi kwanza kuwaelimisha mazuri yaliyoko ndani ya katiba yetu ya sasa lakini pia changtamoto zilizoko ndani ya katiba hiyo kwani sote tunafahamu kwamba katiba imeandikwa muda mrefu na ndiyo sababu tunaifanyia marekebisho.

“Lakini pamoja na yote haya lazima tujue kwamba katiba hii ni nzuri, inafaa ila ina mapungufu kama zilivyo katiba nyingine duniani, hata katiba ya Marekani inayo mapungufu lakini huwa inafanyiwa marekebisho,” amesema Dk. Ndumbaro.

Katika hatua nyingine Dk. Ndumbaro amesema kuwa milango iko wazi kwa wenye maoni juu ya katiba huku akisihi kwamba wanapokosoa ni vizuri pia wakaeleza na mbadala wa nini kinapaswa kufanyika.

“Hatumzuii mtu kusema kwamba katiba yetu ina mapungufu, ila tuambie kifungu, tuambie mapungufu na tueleze mapendekezo yako.

“Katiba yetu ni tunu ambayo imebeba mambo muhimu ya Muungano ambao tunapaswa kuulinda kwa nguvu zote,” amesema Dk. Ndumbaro.

Aidha, kuhusu Rasimu ya Jaji Warioba, Dk, Ndumbaro amesema kuwa kwa sasa ni muda mrefu umepita tangu rasimu hiyo ilipopatikana nakwamba kuna mabadiliko ya watu hivyo ni kuendelea mchakato huo bila kuwashirikisha ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kutoa maoni.

Aidha, katika hatua nyingine Dk. Ndumbaro ameeleza kuwa serikali inakwenda kujenga taasisi jumuishi za Sheria tofauti na ilivyo kwa sasa na kwa kuanzia inakwenda kujenga kwenye majiji na kwenye manispaa

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuondoa usumbufu kwa wananchi wanapotaka kupata huduma katika taasisi hizo za kisheria kufanya kazi maeneo tofauti na pale mwananchi anapohitaji huduma kulazimika kutumia gharama kubwa kuzifikia huduma hizo.

“Tunataka kufungamanisha mifumo ya utoaji haki nchini ndiyo sababu tunakwenda kujenga vituo hivi jumhishi, kama ni mahakama basi kuanzia mahakama ya mwanzo hadi ile ya juu zitapatikana kwenye jengo moja na siyo kusumbua wananchi kwenda huku mara kule,” amesema Dk. Ndumbaro.

Ameongeza kuwa kipaumbele kingine ni pamoja na kutumia lugha ya Kiswahili katika katika utoaji haki nchini ili nkujenga uelewa zaidi kwa jamii juu ya mambo yanayowahusu huku akisisitiza kuendelea kusajili matukio muhimu.

“Pia Serikali itaendelea kuimarisha usajili wamatukio muhimu ya binadamu na takwimu pamoja na shughuli za ufilisi na udhamini, usajili huu utafanikisha utambuzi wa mtu mmoja mmoja pale mwananchi anapopatiwa cheti cha kuzaliwa pia nchi inapata takwimu sahihi za mtiririko wa hali za ndoa na talaka,” amesema Dk. Ndumbaro ambapo kazi hiyo ya usajili inafanywa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini(RITA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles