30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Serikali kuanzisha kiwanda cha mafuta ya bangi

Ramadhan Hassan – Dodoma

SERIKALI imesema tayari imepata wawekezaji wawili ambao wanataka kuwekeza nchini kiwanda cha kuchakata mafuta ya bangi yanayotumika kwa matibabu.

Hayo yalielezwa jana bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki wakati wabunge wakichangia mijadala ya kamati za Kilimo, Mifugo na Maji na Ardhi, Maliasili na Utalii.

Waziri Kairuki alisema tayari wamepata wawekezaji wawili ambao wanataka kuwekeza nchini kwa kuchakata mafuta ya bangi yanayotumika kwa matibabu.

“Tunaendelea kufanyia kazi kama Serikali kwa sababu bado hakuna mwongozo kuweza kuona kama itakubalika ama la kwa sababu bado mwongozo,” alisema.

Hoja ya kuruhusu kilimo cha bangi nchini imekuwa ikiibuliwa mara kadhaa na wabunge akiwamo Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ (CCM).

Jana aliyeiibua alikuwa Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (CCM), ambaye alisema kuwa hatua ya kukosekana bangi imepanda maradufu na karibu nchi zote zinazozunguka Tanzania zimesharuhusu kilimo hicho.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye alisema ni ya msingi ambayo sasa inaweza kufanya mapinduzi katika vipato vya Watanzania.

“Mheshimiwa waziri kwa kuwa sheria hii ipo, naomba ufafanuzi watu wanaotaka kulima wamuone nani?” alihoji Kishimba.

Alisema waliopiga marufuku bangi walikuwa ni wazungu ambao ndio waliobaini kuwa ndani ya bangi kuna dawa.

 “Na sisi wenyewe tunaenda kwenye viwanda. Je, sisi tukiripoti dawa yenye ‘material’ ya bangi tutakuwa ‘tuna-import’ toka wapi? Na ‘tuta-declare’ namna gani?” alihoji.

Kishimba alisema bei ya bangi ni shindani duniani na hivyo kuitaka Serikali kufanya uamuzi huo mapema.

Wakati akichangia taarifa hiyo, ghafla alinyanyuka Mbunge wa Geita Vijijini, Msukuma (CCM) alisema kuwa kwa sheria ipo kinachofuata ni kutunga kanuni ili iweze kutekelezwa.

Msukuma alimtaka Waziri Kairuki kutoa ufafanuzi iwapo wameshatengeneza kanuni ili wakulima waanze kulima kwa sababu zao hilo litaporomoka bei.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, Kishimba alisema kuwa Tanzania ni nchi ya tatu kwa Afrika kwa kulima bangi.

“Sheria itatusaidia katika kuongeza mapato sana. Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani yuko, kama anaweza kutoa msamaha kwa bangi iliyopo hata kwa miezi sita kama anavyotoa kwa silaha, wananchi wakiwasilisha bangi polisi, watu wakauzia wakiwa polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itapata fedha yao,” alisema Kishimba.

Alisema uamuzi wa kuruhusu bangi unaweza kusaidia Watanzania kupata fedha.

 “Dunia inapobadilika lazima twende haraka sana. Uganda wamepewa na EU (Jumuiya ya Ulaya) zaidi ya dola milioni 500 kwa ajili ya kilimo cha bangi. Lakini sisi bahati nzuri wakulima wanao utalaamu wa kulima bangi muda mrefu,” alisema Kishimba.

Alisema kama Serikali itapitisha na sheria hiyo, basi anamuomba waziri kupitisha kilimo hicho kabla ya bei haijaporomoka.

Naye, Ndugai alimkatisha mbunge huyo na kusema anachozungumza sio mzaha na bangi ni biashara kubwa nchini Canada.

“Kwa hiyo anazungumza kitu cha msingi sana na wala si utani, tena inaweza kuwa zao kubwa la biashara linaloweza kuongoza mazao mengi sana na likafanya mapinduzi makubwa sana ya kipato,” alisema Spika Ndugai.

Alisema yeye anazungumzia habari ya kilimo na utaratibu kutengenezea madawa ya wanyama na binadamu.

Akimalizia kuchangia, Kishimba alisema bangi ni tiba na Tanzania inaagiza dawa kutoka nje ya nchi ambazo zina bangi.

“Na sisi huenda tukawa wazalishaji wakubwa, mradi watu wetu tayari kuna utaalamu wa bangi, inaweza kusaidia Waziri wa Afya kupunguza gharama tunazoagiza nje,” alisema Kishimba.

Alisema kumekuwa na malalamiko ya uwekezaji nchini Zambia ambao wameruhusu matajiri pekee na hivyo kuomba waruhusu na wakulima wadogo ili waweze kupata fedha.

Naye, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alisema watu wengi wamekamatwa na kupewa kesi za kusingiziwa kutokana na bangi.

“Hata ukienda polisi wilayani Tarime utakuta polisi wanafanya doria na kama sheria ipo naomba mwongozo ili watu wengi wasionewe,” alisema Heche.

Akijibu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema hakuna sheria inayoruhusu kilimo cha bangi nchini.

“Tunayo sheria ambayo imeweka mamlaka ya kudhibiti uzalishaji, uuzaji na ufanyaji biashara,” alisema Jenista.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles