27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Simanzi yatawala Moshi

Upendo Mosha – Moshi

NI simanzi. Ndivyo unaweza kusema baada ya mji wa Moshi kuzizima kutokana na maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro kuhudhuria ibada ya kuwaaga watu 20 waliofariki dunia kutokana na kugombea kukanyaga mafuta ya upako.

Waumini hao waliofariki dunia Februari Mosi, saa 1:30 usiku katika viwanja ya Majengo Manispa ya Moshi wakati wa mkutano wa injili wa Mtume Boniface Mwamposa (Bulldozer).

Miili hiyo iliagwa jana katika Viwanja vya Mashujaa mjini hapa na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.

Baadhi ya waombolezaji wakiwamo ndugu wa marehemu hao, walionekana kushindwa kuvumilia na wengine kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu huku wahudumu wa Chama cha Msalama Mwekundu Tanzania, wakilazimika kutoa msaada.

SERIKALI KUTOFUNGIA DINI

Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mghwira, alisema kuwa licha ya madhara yaliyotokea yaliyohusisha vifo vya watu 20 na majeruhi 16, Serikali haitafungia taasisi za dini kufanya shughuli zake bali itashughulika na mapungufu yaliyojitokeza.

“Asubuhi ya leo (jana) nilipozungumza na Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli, aliniambia shughulikieni mapungufu yaliyojitokeza, msizifungie shughuli za kidini, hivyo Serikali haitafungia shughuli hizo, tuendelee kumtafuta Mungu,” alisema Mghwira.

Alisema mapungufu yote ya kibinadamu yaliyojitokeza na kuleta madhara yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na kwamba shughuli za dini zitaendelea kama kawaida.

“Kwa niaba ya Serikali na taifa letu, nazileta pole hizi kwa ujumbe huu ya kwamba tushughulikie mapungufu na tusifungie shughuli za kiimani,” alisema Mghwira.

APATA HOFU

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa tukio hilo lililoondoa uhai wa watu 20, lilimwogopesha sambamba na wananchi wengi nao kupatwa na hofu huku akiwataka ndugu waliopoteza wapendwa wao kutokata tamaa bali wasimame imara kumtegemea Mungu.

“Sote tumeumizwa, tumeghafilishwa, tumechanganywa sana na tukio hili, lakini bado tupo na tunampenda na kumwamini Mungu, hivyo jambo hili liwe ni darasa kwetu.

“Wananchi wote na viongozi wote tushikamane na tukio hilo lisitufanye kutengana bali liwe mwanzo wa kujifunza na kutuimarisha katika mambo ya imani,” alisema Mghwira.

AANGUKIA MAKANISA

Pamoja na hayo, Mghwira alizitaka jumuiya zote za makanisa kutoka madhehebu mbalimbali nchini kukutana na viongozi wa Serikali kwa lengo la kuweka misingi madhubuti.

“Nawaombeni viongozi wa dini sisi tuwe chachu ya maarifa ya amani na upendo wa kweli na hali ya kujali watu, mfuate utaratibu mzuri katika mafundisho yenu,” alisema Mghwira.

Alisema mafundisho ya dini lazima yalenge kuimarisha imani kwa Mungu na kwa wanadamu kwani mwendo uliochukua uhai wa marehemu hao ulikuwa ni upungufu.

“Siwezi kuhukumu kwamba mafuta yale yalikuwa hayafai maana kitu chochote kikitumika kwa imani kinazaa matunda,” alisema Mghwira.

VIBAKA WAVAMIA

Alisema katika taarifa za awali imebainika kwamba katika eneo la tukio kulikuwa na vifaa vingi vya kukanyaga mafuta hayo, lakini alishangazwa na waumini kuvamia eneo moja.

Mghwira alisema milango yote vilikuwemo vifaa hivyo na kwamba utaratibu ungetumika wa watu kujipanga na sio kuvamia eneo moja pekee.

Aidha alisema taarifa za awali za uchunguzi zinaonyesha kuwepo kwa uvamizi wa vibaka ambabo walikuwa wakipora mali za waumini hao.

“Vibaka waliingia ndani na kuanza kupora watu, watu wakaanza kukanyagana na sasa tunaachia vyombo vyetu vya ulinzi ili vifanye uchunguzi ili watuambie ni waumini walikanyagana au tatizo ni vibaka.

“Leo hii kama kweli vibaka waliingia tunaweza tusiwakamate kama viongozi wa dini, lakini damu zilizo mwagika ambazo hazina hatia ni dhambi kwao,” alisema Mghwira.

Alisema jana alipata fursa ya kwenda kuwaangalia majeruhi wa tukio hilo, ambapo alikutana na mama mmoja na baada ya kuhoji kwa nini alikwenda, alisema kuwa ni kwa sababu watoto wake hawaelewani.

KAULI ZA VIONGOZI WA DINI

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa dini walioshiriki katika ibada hiyo, walionyesha kutokufurahishwa na tukio hilo na kuonya wananchi kufuata mafundisho ya dini yasiyofuata misingi ya kibiblia.

Padri Colman Siriwa wa Jimbo Katoliki Moshi, alisema tatizo limesababishwa na baadhi ya viongozi wa dini kutafuta majibu rahisi kwa mambo magumu.

“Siku hizi tunatafuta majibu rahisi kwa maswali magumu ya maisha. Viongozi wa dini baadhi wamekuwa wakitumia njia ovu ili kuleta majibu rahisi ambayo yanagharimu uhai wa watu,” alisema Padri Siriwa.

Naye Askofu wa Umoja wa Makanisa ya KKKT, Dk. Stanley Hotay alisema viongozi wa dini wanapaswa kutubu kutokana na baadhi yao kutumia matatizo ya watu kama mitaji.

“Tunapaswa kutubu kwa familia hizi, tusitumie vitabu vya dini vibaya, lakini pia kwa Serikali zamani kulikuwa na utaratibu wa kusajili dini zinapoanza au dhehebu, tunaomba utaratibu ule urudi,” alisema Askofu Dk. Hotay.

Alisema utaratibu huo utasaidia kupunguza madhara na jambo hilo liwe fundisho kwa wananchi wote.

“Wananchi msome majira na nyakati tunazoishi msishiriki tu mafundisho ili mradi, leo tumepoteza watu 20 kwa uzembe,” alisema Askofu Dk. Hotay.

RPC AZUNGUMZA

Akizungumza wakati akitoa taarifa fupi ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni, alisema kuwa mhubiri huyo alipewa kibali na Jeshi la Polisi kufanya mkutano huo kwa siku tatu mfululizo na kwamba siku ya mwisho ndiyo vifo hivyo vilitokea kwa watu kukanyagana kwenye mafuta.

Alisema hadi sasa watu nane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi akiwamo Mtume Mwamposa huku majeruhi wa tukio hilo wakiendelea na matibabu Hosptali ya Rufaa Mawenzi mjini Moshi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,530FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles