BINGWA wa mchezo wa tenisi kwa upande wa wanawake, Serena Williums, ameanza vizuri juzi katika michuano ya wazi ya Australia, baada ya kumchapa mpinzani wake, Camila Giorgi, kwa seti 6-4, 7-5.
Serena alikuwa nje ya uwanja tangu Septemba mwaka jana, lakini amedai kwamba msimu huu amekuja kwa kasi kwa ajili ya kunyakua mataji mbalimbali.
“Mchezo dhidi ya mpinzani wangu Camila ulikuwa wa kawaida wala haukunipa wakati mgumu na ninaamini nimeshinda kwa urahisi, lakini alionesha mchezo mzuri na mimi nilikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
“Kwa upande wangu nina furaha kubwa kurudi uwanjani baada ya kukaa nje kwa kipindi kirefu, ila kwa sasa lengo langu ni kuhakikisha ninachukua mataji mbalimbali hivyo lazima nifanye mazoezi ya hali ya juu ili kuweza kushindana na wapinzani wangu,” alisema Serena.
Hata hivyo, Serena anaamini kwamba ushindani msimu huu utakuwa mkubwa sana kutokana na wapinzani wake walivyotumia muda kufanya maandalizi.