26.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Sekta ya elimu kiungo mtambuka uchumi wa viwanda

Na MWANDISHI WETUSEKTA ya elimu na mafunzo kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2011/12 hadi 2024/25, imekusudia kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika ili kulifanya Taifa kufikia uchumi wa kati na shindani ifikapo mwaka 2025.

Ili kufikia malengo hayo, Serikali imekuwa ikitekeleza sera mbalimbali, hususan Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996), Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu (1999) na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Elimu Msingi (2007).

Hata hivyo, katika kipindi hicho, changamoto mbalimbali zimejitokeza zikiwemo udhaifu katika mfumo wa elimu na mafunzo, uhaba wa walimu, uhaba wa zana, nyenzo na vifaa na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ujumla wake vimechangia katika kushuka kwa ubora wa elimu na mafunzo nchini.

Katika miaka ya hivi karibuni, viwango vya ubora wa elimu vimekuwa vikishuka, ambapo hali hiyo inajidhihirisha na ufaulu katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi na elimu ya sekondari kuwa na mserereko wa kushuka kutoka asilimia 54 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 31 mwaka 2012 kwa upande wa elimu ya msingi.

Sera hizo zilibainisha masuala ambayo Serikali iliyawekea mkazo  zaidi  ili  kuweka  mazingira  mazuri  ya kufikia malengo ya mipango ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na  kuinua ubora wa mfumo wa elimu na mafunzo ili ulete tija na ufanisi, kuinua ubora wa mitaala ya elimu na mafunzo ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, pia Serikali iliweka malengo ya kuimarisha uwezo wa uongozi na utawala katika sekta ya elimu na mafunzo na kupanua wigo wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo, ambapo mafanikio yaliyopatikana yaliibuka changamoto mbalimbali ikiwemo mitaala kutokidhi mahitaji kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na teknolojia.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bejeti ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, anasema Serikali inaendelea kuboresha utoaji wa elimu katika ngazi zote za elimu ya awali, msingi hadi sekondari nchini.

Anasema katika mwaka 2017/18, Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu, wakuu wa shule na waratibu elimu kata 17,518 kuhusu mbinu za kufundisha Kusoma, Kuandika na Kuhesabu pamoja na kutoa vifaa vya Tehama (tablets) 5,450 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kukusanya takwimu na usimamizi.

Waziri Jafo anasema katika mwaka 2017/18, Serikali imefanikiwa kuajiri walimu wapya 2767 sambamba na kuwahamisha walimu wa ziada 8,834 wa masomo ya sanaa na lugha kutoka shule za sekondari kwenda katika shule za msingi na kufanya upungufu wa walimu kuwa  85,916 ikilinganishwa na upungufu wa walimu 97,517 katika mwaka 2017.

Kuhusu uandikishaji, Waziri Jafo anasema hadi kufikia Machi mwaka huu,  uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza nchini ulifikia wanafunzi 1,751,221 wakiwemo wavulana 880,391 na wasichana 870,830, ikilinganishwa na lengo la kuandikisha wanafunzi 1,732,303 sawa na asilimia 100.1 ya lengo.

“Natoa wito kwa wazazi/walezi na jamii kwamba wanao wajibu wa kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anaandikishwa na kuanza masomo,” anasema Waziri Jafo.

Akifafanua zaidi, Waziri Jafo anasema katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu na wananchi, imekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 2,278 kwa shule za msingi.

Jafo anasema ujenzi huo umeongeza idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 120,766 vilivyokuwepo mwaka 2016/17 hadi vyumba vya madarasa 123,044 kufikia Machi 2018 sawa na ongezeko la asilimia 1.8 na hivyo kufanya mahitaji ya vyumba vya madarasa kupungua hadi kufikia 264,594 ikilinganishwa na vyumba 266,872 mwaka 2017.

Kuhusu ufaulu wa wanafunzi, Waziri Jafo anasema jumla ya wanafunzi 662,035 wakiwemo wasichana 341,020 na wavulana 321,015 kati ya 909,950 sawa na asilimia 72.75 walifaulu mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2017 kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kuimarishwa kwa usimamizi wa shule.

Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu elimu na mafunzo ikiwemo  Itifaki ya SADC ya mwaka 1997 inayozitaka  nchi wanachama kuwa na elimu msingi ya lazima kwa kipindi kisichopungua miaka tisa.

Ili kufanikisha malengo hayo, ni wajibu wa sekta binafsi kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia mahitaji ya kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi katika fani mbalimbali kuelekea nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,451FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles