22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

SEKTA TANO ZILIZOTIKISA UTAWALA WA JPM

Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

NI wazi kwamba katika kipindi cha miezi 12 ya utawala wa Rais Dk. John Magufuli, ametikiswa na sekta takriban tano kutokana na kutokuwapo usimamizi mzuri katika maeneo husika.

Sekta hizo ni afya, bandari, elimu, hifadhi na uchumi.

 AFYA

Kwa upande wa sekta ya afya, jambo ambalo linaonyesha kutikisa utawala huu wa Rais Magufuli ni ukosefu wa dawa.

Jambo hilo lilileta mkanganyiko baada ya kuenea taarifa kwamba kuna uhaba wa dawa za binadamu, lakini Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alikanusa taarifa hizo akisema zipo dawa za kutosha.

Oktoba 11, mwaka huu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema ukosefu wa dawa unaojitokeza hivi sasa ni wa muda mfupi.

Kauli hiyo ya Samia ambayo aliitoa wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa wodi ya wazazi Hospitali ya Mwananyamala, ilikinzana na ya Waziri Ummy.

Samia alitoa kauli hiyo baada ya kuelezwa na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Daniel Nkungu, kuwa wamekuwa wakikabiliwa na upungufu wa dawa.

 UCHUMI

Septemba 12 mwaka huu, World Intellectual Property Organization (WIPO) imeiweka Tanzania katika nafasi ya 105 duniani katika ubunifu (innovation achievers) kwa mujibu wa ripoti ya Global Innovation Index (GII) 2016.

Kwa upande wa Afrika Mashariki, kwa nafasi hiyo Tanzania inashika mkia, huku Kenya ikiongoza katika ubunifu ikiwa nafasi ya 80 miongoni mwa nchi 128 duniani, ikifuatiwa na Rwanda (83), Uganda (99) na Burundi nafasi ya 123.

Kwa nafasi hiyo, ni wazi kuwa ripoti hiyo inachafua na kurudisha nyuma juhudi za Rais Magufuli za kufanya Tanzania iwe ya viwanda kwani ubunifu ni suala muhimu sana kwenye sekta hiyo.

Ripoti ya GII huchapishwa kila mwaka, lakini ya mwaka huu inaonyesha nafasi za nchi mbalimbali katika mambo ya kiuchumi katika mazingira ya kuwezesha ubunifu.

 Sekta ya fedha

Kwa mwaka huu, kumekuwa na wimbi la watu kuuza mali zao, ikiwamo mahoteli, majengo na viwanja, huku wengine wakilalamika kukosa wateja.

Si hilo tu, hatua ya Serikali kuhamisha fedha zake kutoka katika benki za kibiashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kile ilichosema kuwa mfumo huo ulikuwa ukitumika kufanya ufisadi, imeonekana kuziathiri taasisi hizo za kifedha.

Tayari benki kadhaa zimeonyesha kushindwa kujiongoza na nyingine kupata hasara kutokana na hali ngumu ya uendeshaji.

Oktoba mwaka huu, Kampuni ua udalali ya Kilindi Auction Mart, ilitangaza kwa niaba ya Benki ya Maendeleo (TIB) kupiga mnada viwanja vilivyowekwa dhamana katika maeneo ya Kunduchi Mtongani, Tegeta na Kyela.

Lakini, athari ni kubwa zaidi kwa Benki ya Twiga Bancorp ambayo Oktoba 28 iliwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu (BoT) baada ya kufikia mtaji hasi wa Sh bilioni 21, ikiwa ni chini ya kiwango cha kisheria, sababu mojawapo ikiwa ni wakopaji kutorejesha fedha.

 Sakata la Dangote

Kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara, kilisitisha uzalishaji kutokana na kuelemewa na gharama za uendeshaji, hivyo kuwaacha watumiaji wake njiapanda.

Jarida maarufu linalofuatilia nyendo za kibiashara za watu wenye ukwasi mkubwa duniani, akiwamo Dangote, Forbes, lilipata kuripoti kuwa uamuzi wa menejementi ya Dangote kusitisha uzalishaji umetokana na kuongezeka kwa gharama kubwa ya uendeshaji.

Sababu nyingine ambayo ilitajwa katika jarida hilo kupitia tovuti yake, ni kile ilichodai ‘kutozingatiwa kwa makubaliano ya mkataba’.

Forbes lilitaja sababu nyingine ya kusitishwa kwa uzalishaji wa kiwanda hicho kuwa ni hatua ya Serikali kusitisha uamuzi wa kuiondolea Kampuni ya Dangote ushuru wa forodha katika mafuta ya dizeli ambayo imekuwa ikiyaingiza nchini kuendeshea mitambo yake.

Kwa mujibu wa Forbes, kiwanda hicho kiliomba TPDC kusaidiwa upatikanaji wa gesi asilia kwa bei nafuu, lakini maombi yao yalikataliwa.

Wakati Forbes wakiripoti hayo, TPDC katika taarifa yake iliyotolewa katikati ya mzozo huo, ilisema kiwanda hicho kilikuwa kikitaka kuuziwa gesi kwa bei ya chini mno.

Kwa mujibu wa TPDC, kiwanda hicho kimeomba kupewa gesi asilia kwa bei ambayo hapa nchini ndiyo inayolipwa kununulia gesi ghafi kutoka kisimani.

TPDC ilisema haiwezi kuuza gesi asilia kwa bei ya kisimani, kwa sababu kuna gharama zinazoongezeka katika kuisafisha na kusafirisha.

Katika andiko lake, Forbes ilieleza kuwa kiwanda hicho kinatumia kiasi cha dola milioni nne, sawa na Sh bilioni 8.7 kila mwezi kwa kununua mafuta ya dizeli ili kupata nishati ya umeme kuzalishia saruji.

Mbali na hayo, jarida hilo la Forbes lilibainisha kile kinachoelezwa namna Serikali ya awamu ya nne ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na ya awamu ya tano ya Rais Magufuli zilivyochukua hatua zinazotofautiana juu ya mkataba wa kiwanda cha Dangote.

Forbes pia ilihusisha uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Juliet Kairuki, Aprili mwaka huu na sakata hilo la Dangote, jambo jipya na ambalo halijapata kutajwa tangu kuibuka kwa sakata hilo.

Hata hivyo, jarida hilo la Forbes linakiri kwamba Ofisi ya Rais haikupata kubainisha sababu za kufutwa kazi kwa mkurugenzi huyo.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alipata kueleza kwamba msingi wa mzozo huo umechochewa na vita inayopinganwa dhidi ya Kampuni ya Dangote na washindani wake kibiashara.

Katika hilo, Mwijage alipata kulieleza gazeti hili kwamba kuna watu wenye hasira zao za kibiashara wametumia mwanya huo kusambaza taarifa hasi dhidi ya mwenendo wa uwekezaji wa Dangote hapa nchini.

Watu mbalimbali wakiwamo wanasiasia, wachumi na wachambuzi walizungumzia uamuzi huo wakisema kuwa suala la Dangote halikupaswa kufikia hatua hiyo kwani linatoa picha mbaya kwa wawekezaji waliopo na wanaotarajiwa kuja nchini.

Baadaye mzozo huo ulimkutanisha mmiliki wa kampuni hiyo, Aliko Dangote na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ilieleza katika mazungumzo yao, Rais ameibua hoja mpya ambazo aghalab hazijapata kuripotiwa ama na maofisa wa Serikali au wale wa bilionea huyo tangu kuibuka kwa mzozo huo.

Rais Magufuli alisema hapakuwa na tatizo lolote kuhusu kiwanda hicho, isipokuwa mradi huo uliingiliwa na wapiga dili.

Rais Magufuli alimhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa Serikali yake itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini katika kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya viwanda.

Kwa upande wake, Dangote alidai kushangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya Tanzania, kitu ambacho alisema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.

Mfanyabiashara huyo alisema ameingiza malori mapya 600 ya kusambazia saruji yake.

 Mizigo Bandari

Mamlaka ya Bandari (TPA), ilieleza ufanisi katika upakuaji na uondoshaji mizigo na usalama wa mali katika Bandari ya Dar es Salaam.

Ilibainika idadi ya mizigo katika bandari hiyo, imepungua tofauti na matarajio.

Hatua hiyo ilitokana na kile kilichoelezwa kuwapo kwa ushindani mkali kutoka bandari za nchi jirani kama vile Mombasa (Kenya), Nacala/Beira (Msumbiji), Walvis Bay (Namibia), Durban (Afrika Kusini) na Lobito (Angola).

Bandari hizo zinaelezwa kuwa zilitikisa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ilikimbiwa na wasafirishaji wa mizigo.

ELIMU

Sekta nyingine iliyotikisa utawala wa Rais Magufuli ni elimu, hususan pale zaidi ya wanafunzi 7,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waliposimamishwa huku wakitakiwa kuondoka mara moja.

Wanafunzi hao wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada, walisimamishwa na uongozi wa chuo kutokana na agizo lililotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.

Jambo lililoshangaza wengi ni malalamiko ya wanafunzi hao kuhusu namna walivyopewa taarifa za kusimamishwa masomo yao kwa ghafla.

Wanafunzi hao waliokuwa wamekopeshwa na Serikali walisimamishwa siku mbili baada ya wenzao zaidi ya 480 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph kusimamishwa baada ya kubainika hawakuwa na sifa za kudahiliwa.

Kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wengi hawakupata.

Takwimu hiyo inaonyesha kwamba zaidi ya robo tatu ya wanafunzi wanaohitaji mikopo wamekosa.

 Sekta ya hoteli

Uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kubana matumizi kwa kuzuia wizara, taasisi na mashirika ya umma kufanya mikutano kwenye hoteli, pamoja na kodi, uligeuka mchungu kwa wamiliki wa biashara hiyo.

Kutokana na hatua hiyo, hoteli maarufu zilizopo Dar es Salaam na mikoa mingine, zimelazimika kufungwa, huku nyingine zikibadilishwa na kuwa hosteli za kuhudumia wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kati.

Mbali na hilo, pia baadhi ya wamiliki wa hoteli hizo wamelazimika kupunguza wafanyakazi kama njia ya kukabiliana na athari za ukosefu wa mapato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles