23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Sekondari Mlowa yakumbukwa, utoro sasa wapungua

CHRISTINA GAULUHANGA

KUANZISHWA kwa shule za sekondari za kata nchini kumechangia kwa kiasi kikubwa familia nyingi kupata fursa ya  kujiendeleza kielimu na kupata mafanikio makubwa.

Miaka iliyopita, watoto wengi walijikuta wakiishia shule za msingi kwa sababu ya gharama kubwa za shule za sekondari binafsi na vyuo.

Lakini hivi sasa, Serikali imefungua fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye vigezo ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu.

Katika kuunga mkono sekta ya elimu nchini, wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wamejitokeza kuhakikisha wanaiwezesha sekta hiyo ili kuendeleza kizazi cha sasa na kijacho, hatimaye kufikia maendeleo ili kuendana na kasi ya teknolojia ambayo imelishika soko la Afrika Mashariki.

Umoja wa nchi zinazozalisha na Kusambaza Mafuta Duniani (OPEC), ni miongoni mwa wadau ambao waliona haja ya kuwezesha sekta ya elimu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao waliamua kujenga miundombinu ya elimu ikiwamo nyumba za walimu, jengo la utawala na mabweni ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mlowa, iliyopo Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Raymond  Kyando, anasema kujengwa kwa shule hiyo kumesaidia usalama wa wanafunzi na walimu kwani hapo awali, mazingira ya shule hiyo yalikuwa hatarishi kwa sababu ya kuzungukwa kwa pori na umbali mrefu wa wanafunzi kutoka maeneo wanayoishi.

Anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2014 ikiwa na madarasa matatu ambapo kwa sasa ina madarasa tisa na wanafunzi wa kutwa wengi wao wamekuwa wakitembea umbali wa kilometa 12.

“Umbali wa kuja shule ni kilometa 12 hivyo, kwenda na kurudi ni sawa na kilometa 24. Wanafunzi hawa wamekuwa wakiamka alfajiri ili waweze kuwahi lakini kadri siku zinavyokwenda maendeleo yao yalikuwa mabaya,” anasema Kyando.

Anasema ili kubadili matokeo ya shule hiyo, mwaka 2015 walilazimika kuanzisha kambi ya wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani, mpango ambao uliwajenga vema wanafunzi na kufaulu vizuri.

Anasema mwaka 2016 waliamua kushirikiana na wazazi pamoja na walimu kuanzisha kampeni ya ujenzi wa hosteli ili wanafunzi hao wapate makazi salama, lakini kwa sababu ya uwezo mdogo wa jamii inayowazunguka walishindwa kufikia malengo.

“Wakati huu tayari tulikwishaanza kupata athari baada ya wanafunzi wetu wanne kukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito na hii ilitokana na mazingira kutokuwa rafiki kimasomo,” anasema Kyando.

Anaongeza kuwa mwaka 2017, iliibuliwa miradi ya TASAF na mwaka 2018 walianza ujenzi wa hosteli ndani ya shule hiyo kupitia Mradi wa OPEC ambao kwa kiasi fulani ulitokomeza mimba za utotoni ndani ya shule hiyo.

Anasema tangu kuanzishwa kwa hosteli hizo, mahudhurio na taaluma inazidi kupanda japokuwa wapo baadhi ya wanafunzi wa kiume ambao wanaendelea kuteseka kwa sababu bado wanatokea nyumbani.

“Baada ya hosteli hizi kukamilika, ambazo zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 48 tuliamua kuwapa kipaumbele zaidi wasichana kwa sababu wao ndio waathirika zaidi wa mazingira na baadhi yao wamekuwa wakidanganyika na kukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito, huku wengine wakikimbilia kufanyakazi za ndani,” anasema Kyando.

Anasema kwa upande wa walimu, usalama wao mitaani haukuwa mzuri na siri nyingi za ofisi zilikuwa zinavuja kwa sababu ya ukosefu wa majengo ya utawala na nyumba za kuishi.

“Kwa sasa tunashukuru tumepata uhakika wa wanafunzi kuhudhuria masomo yao kwa wakati na hata muda wa jioni kujisomea kwa kushirikiana na walimu kwani tuna umeme wa uhakika,” anasema Kyando. 

Mwalimu Nzangwa Silinu, anasema uwapo wa nyumba za walimu umeileta faraja na furaha ya kufundisha kwa moyo wa dhati.

“Mazingira rafiki tuliyonayo sasa ni deni kubwa kwetu kwa Serikali, nasi tunaahidi kuwa tutalilipa kupitia ufaulu wa juu wa wanafunzi,” anasema Silinu.

Anasema watahakikisha wanafundisha kwa kiwango cha juu ili kuleta mabadiliko makubwa ndani ya jamii hiyo.

Naye mkazi wa Kijiji cha Mlowa, Elia Ally, anaishukuru Serikali kwa ujenzi wa hosteli hiyo kwani imesaidia kuzuia mimba shuleni kwa sababu wanafunzi wengi walikuwa wanabakwa na kupata mimba mtaani kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

“Kama Mungu akipenda tunaiomba Serikali isituache isonge mbele zaidi kutusaidia sisi kwa sababu familia zetu zilikuwa nyuma na wengi hawakuwa na uwezo wa kusoma kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha,” anasema Ally.

Anasema awali eneo hilo lilikuwa ni pori na wanyama walikuwa wametapakaa kwa wingi jambo ambalo lilikuwa likitishia usalama wa wanafunzi, walimu na hata wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Ally anasema uwapo wa shule za kisasa na majengo yenye hadhi yameipa hadhi ya kipekee halmashauri hiyo hivyo, wanaishukuru OPEC, TASAF na Serikali pia.

Msimamizi wa Miradi ya TASAF, Halmashauri ya Mji wa Njombe, Edwin Mlowe, anasema gharama za mradi wa ujenzi wa hosteli hizo ni zaidi ya Sh milioni 287.

Anasema fedha hizo zilitumika kujenga majengo manne likiwamo bweni la wasichana, ofisi ya utawala na nyumba za walimu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi Ngazi ya Jamii (CMC), Agnes Kawogo, anaiomba Serikali iwaondolee changamoto ya miundombinu ya kielimu kwa kuwajengea hosteli ya wanawake na wanaume pamoja na bwalo la chakula.

Anasema ujenzi wa hosteli hiyo ya awali iliyojengwa kwa msaada wa OPEC, umeleta mabadiliko na kuwainua kielimu watoto wa kijiji hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles